read

Aya 77- 80: Huzuni Ya Lut

Maana

Na wajumbe wetu walipomfikia Lut, aliwahuzunikia na akawaonea dhiki.

Ujumbe uliondoka kwa Ibrahim (a.s.) kuelekea kwa Lut (a.s.).

Katika Juz.8 (7:80) tulitaja kuwa Lut ni mtoto wa ndugu yake Ibrahim na kwamba yeye alikuwa mashariki mwa Jordan na kaumu yake ndio watu wa kwanza kuwaingilia kimwili wanaume badala ya wanawake. Na hili walikuwa wakilifanya dhahiri bila ya uficho wowote. Mwenye kukataa walikuwa wakimshika kwa nguvu; hata kama ni mgeni mheshimiwa.

Kwa hiyo walipokuja wajumbe wa Mwenyezi Mungu kwa Lut, kwa sura za kibinadamu, alihofia watu wake wasiwakosee heshima, huku akiwa hawezi kuwazuia.

Basi akawa anaona uchungu Na akasema: Hii ni siku ngumu.

Na wakamjia kaumu yake mbiombio.

Yaani walikuja nyumbani kwa Nuh haraka wakidhani kuwa siku hii ni kama nyingine na kabla ya haya walikuwa wakifanya maovu hawakufkiria mwisho wake.

Akasema: Enyi kaumu yangu! Hawa binti zangu wao wametakasika zaidi kwenu.

Makusudi ya binti zake ni binti wa umma wake; kwa sababu mtume ni kama mzazi kwa umma wake. Maana ni kuwa oweni wanawake na mstarehe kwa halali na wema na muache ulawiti kwa sababu hiyo ni kazi ya shetani. Basi mcheni Mwenyezi Mungu.

Anawahofisha na Mungu, na hilo wanalipuuza watu wa ufuska na uovu.

Wala msinifedheheshe mbele ya wageni wangu. Ikiwa hamumuogopi Mwenyezi Mungu basi angalau muone haya, msinifedheheshe mbele ya wageni. Hivi hakuna mtu muongofu miongoni mwenu? mwenye akili atakayewazuia hayo mnayotaka?
Wakasema: Umekwishajua hatuna haki juu ya binti zako Yaani hatuwataki Na hakika unajua tunayoyataka.

Yaani unajua kuwa sisi hatupendelei mabinti, tunataka wanaume na unajua kuwa sisi hatutishwi na huyo Mungu wako. Binadamu anafikia kiwango hiki cha kiburi akiwa amejiachia, akipinga misimamo na kukosa majukumu.

Kuna watu leo walio mfano wa kaumu Lut katika ushenzi na kiburi tena ni wengi. Miongoni mwao wamo walezi na waalimu wa mashule na vyuo vikuu.

Na sisi hatuna shaka kwamba kuna watu wa dini ambao ni waovu mara elfu kuliko hao. Lakini la kusisitiza ni kuwa lau kusingelikuweko na watu wanaolingania kwenye dini na misimamo, basi ulimwengu ungelikuwa mbaya kuliko ulivyo hivi sasa.

Akasema: Lau ningelikuwa na nguvu kwenu au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!

Baada ya Lut kukata tamaa na watu wake, alitamani lau angelikuwa na nguvu za kuwazuia au kupata msadizi. Alitamani hivi akiwa hajui kwamba nusura ya Mwenyezi Mungu iko nyumbani kwake na kwamba umebakia wakati mchache sana wa kuangamia wafisadi.

قَالُوا يَا لُوطُ إِنَّا رُسُلُ رَبِّكَ لَنْ يَصِلُوا إِلَيْكَ ۖ فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِنَ اللَّيْلِ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنْكُمْ أَحَدٌ إِلَّا امْرَأَتَكَ ۖ إِنَّهُ مُصِيبُهَا مَا أَصَابَهُمْ ۚ إِنَّ مَوْعِدَهُمُ الصُّبْحُ ۚ أَلَيْسَ الصُّبْحُ بِقَرِيبٍ {81}

Wakasema: Ewe Lut! Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako. (Hawa) hawatakufikia. Basi ondoka pamoja na watu wako wa nyumbani katika sehemu ya usiku. Wala yeyote katika nyinyi asigeuke nyuma, isipokuwa mke wako, kwani yeye yatamsibu yatakayowasibu. Hakika miadi yao ni asubuhi, je asubuhi si karibu?

فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِنْ سِجِّيلٍ مَنْضُودٍ {82}

Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini. Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana.

مُسَوَّمَةً عِنْدَ رَبِّكَ ۖ وَمَا هِيَ مِنَ الظَّالِمِينَ بِبَعِيدٍ {83}

Yaliyotiwa alama kwa Mola wako. Na hayo hayako mbali na wenye kudhulumu.