read

Aya 81-83: Hawatakufikia

Maana

Wakasema: Ewe Lut! Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako. Hawa hawatakufikia.

Arrazi anasema: Malaika walipoona wasiwasi na huzuni ya Lut walimpa bishara zifuatazo:

1. Kwamba wao ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu.

2. Makafiri hwatafikia lile walilolikusudia.

3. Mwenyezi Mungu atawaangamiza.

4. Mwenyezi Mungu atamwokoa yeye na watu wake kutokana na adhabu.

5. Kwamba yeye Lut yuko kwenye Nguzo yenye nguvu, kwa sababu Mungu atamwokoa na watu madhalimu.

Basi ondoka pamoja na watu wako wa nyumbani katika sehemu ya usiku. Wala yeyote katika nyinyi asigeuke nyuma, isipokuwa mke wako, kwani yeye yatamsibu yatakayowasibu.

Malaika walimtaka Lut atoke na watu wake wa nyumbani na kutoangalia nyuma yeyote. Huenda hekima ya hilo ilikuwa ni kutoona muangaliaji jinsi mji wake unavyoangamia asishikwe na hurumma akahuzunika.

Ama mkewe alimwacha, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, pamoja na makafiri kwa sababu yeye ni miongoni mwao. Kwa hiyo naye alikuwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu zake.

Hakika miadi yao ni asubuhi, je asubuhi si karibu?

Haya ni katika maneno ya kuashiria jibu la anayeharakisha adhabu.

Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini.

Dhamiri ya tuliiegeuza ni ya ardhi ya vijiji vya kaumu ya Lut. Baadhi ya tafsiri zinasema kuwa umbali wake na Baytul maqdis ni mwendo wa siku tatu

Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana, yaliyotiwa alama kwa Mola wako.

Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema:

لِنُرْسِلَ عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِنْ طِينٍ {33}

Tuwatupie mawe ya udongo” (51:33).

Yaliyopandana inaweza kuwa ni kupandana hayo yenyewe au kupandana kwa mfululizo wa kushuka. Alama ni alama maalumu ya kumfikia yule anayestahiki. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliteremsha adhabu mbili kwa kaumu ya Lut: Mvua ya mawe na kuzama ardhini.

Na hayo hayako mbali na wenye kudhulumu.

Wafasiri wanasema kuwa wenye kudhulumu hapa ni makafiri wa Makka, kwamba Mwenyezi Mungu aliwaahidi kuwa wao, yatawapata yaliyowapata watu wa Lut, kama wataendelea kumkadhibisha Muhammad (s.a.w.).

Maana haya hayako mbali, pamoja na kujua kuwa kila dhalimu aliyeko mashariki au magharibi anaweza kushukiwa na adhabu kutoka mbinguni au kuadhibiwa ardhini. Kwani mapinduzi yoyote yanayotokea au yatakayotokea, basi matokeo yake ni adhabu kwa dhulma na watu wake na kwa ufisadi na wasaidizi wake.

وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا ۚ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ ۖ وَلَا تَنْقُصُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ ۚ إِنِّي أَرَاكُمْ بِخَيْرٍ وَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ مُحِيطٍ {84}

Na kwa Wamadian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Wala msipunguze kipimo na mizani. Mimi ninawaona mko katika kheri; na mimi nawahofia na adhabu ya siku izungukayo.

وَيَا قَوْمِ أَوْفُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ {85}

Enyi watu wangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao. Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.

بَقِيَّتُ اللَّهِ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ ۚ وَمَا أَنَا عَلَيْكُمْ بِحَفِيظٍ {86}

Alivyowabakishia Mwenyezi Mungu ni bora kwa ajili yenu ikiwa nyinyi ni waumini. Wala mimi si mlinzi wenu.