read

Aya 87-90: Historia Ya Ukomunisti Na Ubepari

Maana

Wakasema: Ewe Shuaib! Je, Swala yako inakuamuru, tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu au kufanya tupendavyo katika mali zetu?

Kila asiyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, huifanya swala ni ya kudharau na kuifanyia stizai pamoja na hao wanaoswali. Bila shaka yoyote Shuaib alikuwa ni katika wanaoswali.
Alipowaamuru watu wake kutupilia mbali masanamu, na kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuwakataza chumo la haramu, ndio wakaanza kumdharau na kusema: Hivi swala yako ya kipuuzi unayoiswali ndiyo inakufanya utuamrishe tuache ada zetu tulizowakuta nazo mababa zetu na mababu zetu jadi na jadi; tena unatukataza tuache kuchumma mali vile tupendavyo?

Hakika wewe ndiwe mpole, mwongofu!

Yaani, kweli wewe una akili kwa haya uyasemayo?

Aya hii inakusanya mambo yafuatayo:-

1. Risala ya mitume haiko kwenye nembo peke yake, bali inakusanya maisha ya kijamii na kumpangia binadamu uhuru wake na matumizi yake na kumwekea mipaka ya kutomwingilia mwingine, vilevile kumzuia kufanya tendo lolote baya litakaloleta madhara kwa mtu binafsi na kwa jamii. Dalili wazi juu ya hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya 85 ya sura hii: “wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao. Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu”

2. Aya imefahamisha kuwa maadui wakubwa wa mitume na wenye kuswali ni wale wanaotafuta mali kwa hadaa na utapeli na kutumia vipato vya watu vile wanavyotaka; kama yanavyofanya mashirika mengi ya ulanguzi na unyonyaji.

3. Vilevile Aya inafahamisha kwamba ubepari una mizizi ya kihistoria.

Ushahidi wa hilo ni mwingi sana. Kwa mfano huu ubepari unaotaka kila mtu awe na uhuru wa kupata utajiri vile atakavyo, iwe ni kwa uporaji au kwa lolote lile. Hilo linafafanuliwa na kauli ya waliomdodosa Shuaib: “Au kufanya tupendavyo katika mali zetu” Makusudio sio kula na kuvaa watakavyo; isipokuwa ni kuwatumia watu katika kupata mali vile wapendavyo.

Kama ambavo historia imeonyesha kuwa siasa za Ubepari zilianza zamani, vilevile inafahimisha historia kuwa Ukomonisti nao ulianza zamani. Imeelezwa katika uchunguzi wa mwanahistoria W.L. Dewarnet kwamba watafiti walipata ubao wa Sumeria ambao tarehe yake inarudi kwenye mwaka 2100, kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, ukisema kuwa Serikali ndiyo inayopanga mwelekeo wa kiuchumi.

Katika Babilon, mnamo mwaka wa 1750, kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, Sheria ya Hamurabi ndiyo iliyokuwa ikipanga bei za kila kitu. Na katika zama za Batholomeo, serikali ndiyo iliyokuwa ikimiliki ardhi na kuongoza kilimo na mengimeyo.

Uislamu haukubaliani na siasa za ubepari wala za ukomonisti kwa maana yake yaliyo mashuhuri; isipokuwa unakubaliana na kila linalotatua matati- zo ya maisha bila ya kuwapunguzia watu vitu vyao. Angalia kifungu, ‘Tajiri ni wakili sio mweneyewe’ katika kufasiri Juz. 4 (3:182)

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ni dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu?

Imetangulia Aya kama hii katika Aya 28 ya sura hii.

Na ameniruzuku riziki njema itokayo kwake?

Baada ya Shuaib kuwaamrisha watu wake wachume kihalali na kuwakataza haramu, aliwapa hoja ya riziki aliyoruzukiwa na Mwenyezi Mungu, inayotosheleza mahitaji yake yote, pamoja nakuwa yeye yuko mbali na haramu.

Kwa hiyo basi sababu za riziki nzuri sio haramu. Ni jambo lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu afungue mlango wa riziki kisha awanyime waja wake. Kauli yake: Na ameniruzuku riziki njema, inaonyesha alikuwa na maisha mazuri.

Wala sipendi kuwakhalifu nikafanya yale ninayowakataza.

Lau angelifanya hivyo wao wangelikuwa na hoja juu yake. Na katika sharti za mtume ni kuwa sifa zake zote ziwe ni za kuvutia sio za kufukuza. Na ilivyo ni kuwa anayesema asiyoyafanya basi atakimbiwa.

Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyoweza.

Na mtengenezaji huwaonya watu kwa vitendo vyake kabla ya maneno yake. Na kuendeleza mwito wake huku akivumlia adha na mashaka. Ndio maana Shuaib na mitume wengineo walikuwa wakila kutokana na kazi ya mikono yao na walikuwa wakivumilia adha kutoka kwa makafiri na wapinzani.

Na taufiki yangu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu. Kwake ninategemea na kwake naelekea.

Yaani kwamba yeye ataendelea kutekeleza risala yake kwa hali yoyote itakavyokuwa, akiwa anamtegemea Mwenyezi Mungu, kutaka msaada wake na kumrejea yeye katika mambo yake.

Na enyi watu wangu! Kupingana nami kusije kukawapelekea yakawasibu kama yaliyowasibu kaumu ya Nuh au kaumu ya Hud au kaumu ya Swaleh, na kaumu ya Lut si mbali nanyi.
Yaani uadui wenu kwangu usije ukawasababishia adhabu. Kwani hakuna watu waliomfanyia uadui mtume wao ila huwashukia wao adhabu. Ushahidi wa hayo ni mitume waliotajwa. Ni kama mfano wa anayeambiwa: Usimuudhi baba yako usije ukapatwa na hasira za Mwenyezi Mungu.

Na muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.

Umepita mfano wake pamoja na tafsir yake katika Aya ya 52 na 61 ya Sura hii.

Hakika Mola wangu ni Mwenye kurehemu Mwenye upendo.

Mwenye kurehemu anayemtaka maghufira na Mwenye upendo kwa kuwaneemesha waja wake, kuwapa nasaha na kuapa muda ili wapate kurejea.

قَالُوا يَا شُعَيْبُ مَا نَفْقَهُ كَثِيرًا مِمَّا تَقُولُ وَإِنَّا لَنَرَاكَ فِينَا ضَعِيفًا ۖ وَلَوْلَا رَهْطُكَ لَرَجَمْنَاكَ ۖ وَمَا أَنْتَ عَلَيْنَا بِعَزِيزٍ {91}

Wakasema: Ewe Shuaib! Hatufahamu mengi ya hayo unayoyasema; na sisi tunakuona kwetu ni mdhaifu. na lau si jamaa zako, bila shaka tungelikurujumu. Wala wewe si Mtukufu kwetu.

قَالَ يَا قَوْمِ أَرَهْطِي أَعَزُّ عَلَيْكُمْ مِنَ اللَّهِ وَاتَّخَذْتُمُوهُ وَرَاءَكُمْ ظِهْرِيًّا ۖ إِنَّ رَبِّي بِمَا تَعْمَلُونَ مُحِيطٌ {92}

Akasema: Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu? Na Yeye mmemuweka nyuma ya migongo yenu? Hakika Mola wangu ni mwenye kuyazunguka yote mnayoyatenda.

وَيَا قَوْمِ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنِّي عَامِلٌ ۖ سَوْفَ تَعْلَمُونَ مَنْ يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَمَنْ هُوَ كَاذِبٌ ۖ وَارْتَقِبُوا إِنِّي مَعَكُمْ رَقِيبٌ {93}

Enyi watu wangu! Fanyeni muwezavyo, mimi ninafanya. Karibuni mtajua ni nani itakayemfika adhabu itakayomfedhehesha na nani aliye mwongo. Na ngojeni nami ninangoja pamoja nanyi.

وَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا شُعَيْبًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِنَّا وَأَخَذَتِ الَّذِينَ ظَلَمُوا الصَّيْحَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دِيَارِهِمْ جَاثِمِينَ {94}

Ilipofika amri yetu tulimwokoa Shuaib na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu. Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao.

كَأَنْ لَمْ يَغْنَوْا فِيهَا ۗ أَلَا بُعْدًا لِمَدْيَنَ كَمَا بَعِدَتْ ثَمُودُ {95}

Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! (watu wa) Madyan wamepotelea mbali; kama walivyopotelea mbali (watu wa) Thamud.