read

Aya 9 – 11: Kuhusu Mtu

Maana

Na kama tukimwonjesha mtu rehma inayotoka kwetu, kisha tukamwondolea, hakika yeye hukata tamaa akakufuru.

Makusudio ya kuonjeshwa hapa ni kupewa. Mtu anaporuzukiwa afya njema, mali inayomtosha na familia nzuri, kisha akapatwa na jambo lolote baya, basi hukata tamaa na kuanza kukufuru na kutokuwa na shukrani hata na neema iliyobakia.

Na kama tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyompata, bila shaka husema, taabu zimeniondokea. Hakika yeye ndiye mwenye kufurahi sana akijitapa.

Akitoka kwenye uzito kwenda kwenye wepesi na kutoka kwenye hofu hadi amani, basi huanza kujisahau.

Tumekwishaeleza mara nyingi kwamba Mwenyezi Mungu anategemezewa yeye matukio yote kwa kuwa yeye ndiye sababu ya kwanza ya mambo, kwamba ndiye muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.

Hapana budi kudokeza kwamba Qur’ani inamwangalia mtu kulingana na itikadi yake na tabia yake. Anaamini nini na anafanya nini? Mtazamo huu unalazimiana na tabia ya Qur’ani, kama Kitabu cha dini na mwongozo. Ni kwa msingi huu ndipo anapohukumiwa mtu kuwa ni mwema au mwovu.

Na inajulikana kuwa itikadi ambayo Qur’ani inalingania ni kumwamini Mwenyezi Mungu na Mitume yake na siku ya mwisho, na matendo iliyoamrisha ni yale yaliyomo mema.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ {7}

“Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe.” (98:7).

Kwa maneno mengine ni kuwa Uislamu unamwelekeza mtu kwenye malengo ambayo anapaswa kushikamana nayo. Kama akiyawacha malengo hayo, basi Qur’ani inamwita mtu huyo kwa majina mabaya; kama vile dhalimu, mwenye hasara, kafiri, mjinga, mwenye kupetuka mipaka, mwenye inadi n.k. Kwa hakika sifa hizi hazielezei tabia ya mtu na umbile lake, isipokuwa ni tafsiri ya tabia yake katika baadhi ya misimamo yake.

Qur’ani inatufahamisha kuwa kila sifa iliyotajwa inaambatana na tukio fulani. Imemsifu mtu kuwa ni mwenye kukata tamaa pale anapopatwa na majanga, mwenye furaha akiwa amejitosheleza na mwenye fazaa akipatwa na madhara. n.k.

Watu wengi, hawaijui hakika hii. Wanadhani kuwa sifa hizi zimekuja katika Qur’ani kuelezea umbile la mtu alivyo, na wakawa wanamsifu nazo mtu kinyume na kinavyoeleza Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kama ingelikuwa kweli dhana yao hii, basi isingelifaa Mwenyezi Mungu kumwaadhibu kafiri na aliyepetuka mipaka, kwa sababu ni umbile lake kufanya hivyo. Pia kauli yake:

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ {70}

“Na hakika tumewatukuza binadamu.” (17:70),

ingelikuwa ni kuutukuza ukafiri na dhulma. Mwenyezi Mungu ametakata na hayo kabisa.

Kwa hiyo basi makusudio ya mtu katika kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kama tukimwonjesha mtu”, ni yule asiyemwamini Mwenyezi Mungu au anayemwamini kinadharia tu, sio kimatendo. Kwa sababu anayemwamini kikweli kweli, humtegemea yeye tu, katika hali zote na anamshukuru wakati wa faraja na wa dhiki. Anamwogopa na kumnyenyekea akiwa tajiri na kuwa na subira akiwa fukara. Kwa sababu imani ni nusu mbili: nusu ya hofu na nusu ya kutarajia.

Linalosisitiza kuwa lengo la mtu hapa ni yule tuliyemtaja, ni kauli yake Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila kuweko na maneno mengine:

Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema, hao watapata msamaha na ujira mkubwa.
Waliofanya subira katika masaibu na madhara kwa kumwamini Mwenyezi Mungu kutumai kupata thawabu na radhi yake na wakatenda mema katika shida na raha. Hiyo ndiyo nembo ya wenye itikadi na msimamo. Kwa sababu itikadi ikituwa kwenye moyo wa mtu, inakuwa kama roho, haimbanduki mpaka kufa.

فَلَعَلَّكَ تَارِكٌ بَعْضَ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ وَضَائِقٌ بِهِ صَدْرُكَ أَنْ يَقُولُوا لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ كَنْزٌ أَوْ جَاءَ مَعَهُ مَلَكٌ ۚ إِنَّمَا أَنْتَ نَذِيرٌ ۚ وَاللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ {12}

Basi pengine utaacha baadhi ya yale uliyopewa wahyi. Na kifua chako kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema, mbona hakuteremshiwa hazina? au wakaja naye Malaika? Hakika wewe ni muonyaji tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu.

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ فَأْتُوا بِعَشْرِ سُوَرٍ مِثْلِهِ مُفْتَرَيَاتٍ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {13}

Au wanasema ameizua? Sema, basi leteni Sura kumi zilizozuliwa mfano wa hii na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.

فَإِلَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكُمْ فَاعْلَمُوا أَنَّمَا أُنْزِلَ بِعِلْمِ اللَّهِ وَأَنْ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَهَلْ أَنْتُمْ مُسْلِمُونَ {14}

Na wasipowaitikia, basi jueni ya kwamba imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana Mola isipokuwa Yeye, basi je, nyinyi ni Waislamu?