read

Aya 96-99: Musa

Maana

Alipomaliza, Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kutaja yaliyowapata watu wa Nuh, Hud, Swaleh, Lut, Na wa Shuaib, ameashiria kwa Firaun na kaumu yake. Na lengo ni mazingatio na mawaidha.

Kwa muhtasari Aya hizi nne zinazungumzia kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimtumma Mussa (a.s.) kwa Firauni na watu wake kwa hoja na dalili zilizo wazi. Miongoni mwazo ni fimbo na mkono, lakini Firauni aling’angania ukafiri na utaghuti; kama alivyowalazimisha watu wake wamfuate na wafuate amri zake.

Mwisho wa wafuasi na anyefuatwa ukawa ni laana na maangamizi hapa duniani na Akhera.

Lau Firaun asingepata wafuasi na wasaidizi, basi asingeweza kujasiri na kusema:

أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ {24}

“Mimi ndiye Mola wenu mkubwa” (79:24)

na

مَا عَلِمْتُ لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرِي {38}

“Simjiu kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi” (28:38)

Mfisadi na mpotezaji yoyote hawezi kujitokeza ila baada ya kupata wafuasi.

Tabia ya binadamu iko hivyo wakati wowote, linalobadilika ni jina na mfumo tu. Zamani kulikuwa na Firauni na Namrud, leo ni majeshi ya ushirika na mashirika kama vile ARAMCO n.k. Ama wafuasi na wasaidizi ni wale wanaokabidhiwa majukumu na kuonekana ndio watukufu baina ya watu.

ذَٰلِكَ مِنْ أَنْبَاءِ الْقُرَىٰ نَقُصُّهُ عَلَيْكَ ۖ مِنْهَا قَائِمٌ وَحَصِيدٌ {100}

Hizo ni habari za miji tunazokusimulia, mingine bado ipo na mingine imefyekwa.

وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَٰكِنْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ۖ فَمَا أَغْنَتْ عَنْهُمْ آلِهَتُهُمُ الَّتِي يَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ شَيْءٍ لَمَّا جَاءَ أَمْرُ رَبِّكَ ۖ وَمَا زَادُوهُمْ غَيْرَ تَتْبِيبٍ {101}

Nasi hatukuwadhulumu, lakini wao wamejidhulumu wenyewe. Na miungu yao waliyokuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, haikuwafaa kitu ilipofika amri ya Mola wako, na haikuwazidishia isipokuwa maangamizi.

وَكَذَٰلِكَ أَخْذُ رَبِّكَ إِذَا أَخَذَ الْقُرَىٰ وَهِيَ ظَالِمَةٌ ۚ إِنَّ أَخْذَهُ أَلِيمٌ شَدِيدٌ {102}

Na ni kama hivyo kushika kwa Mola wako anapoishika miji inapokuwa imedhulumu. Hakika kushika kwake ni kuchungu, kukali.