read

Aya Ya 45-49: Nuhu Akamwomba Mola Wake

Na Nuh alimwomba Mola wake akasema: Ewe Mola wangu! Hakika mwanangu ni katika watu wangu, na hakika ahadi yako ni haki na wewe ni hakimu bora wa mahakimu wote.

Katika Aya ya 40 Mwenyezi Mungu alimwamrisha Nuh kuchukua watu wake wa nyumbani, isipokuwa yule aliyemkataza; na hakumkataza wala kumwamrisha kumchukua mwanawe, bali alinyamaza kwa hekima yake. Nuh akadhani kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawaokoa watu wake wote wa nyumbani, waasi na watiifu.
Ndio maana akamwomba Mola atekeleze ahadi yake kwa mwanawe, kwa sababu ni katika watu wake. Unaweza kuuliza: Nuh ni mtume na mtume ni maasumu (aliyehifadhiwa na dhambi) itakuwaje adhanie kinyume?

Jibu: Kudhania kinyume hakuharibu isma (kuhifadhiwa na dhambi) ikiwa hakuna kitendo, kwa vile kunafanana na mawazo tu yanayopita kichwani kisha yanaondoka, kama vile hayakuwepo. Hata tukikadiria kuwa maasum amedhania kinyume na hali halisi, basi Mwenyezi Mungu atamfichulia na atamhifadhi na makosa. Hayo tumekwisha yafafanua katika Juz.5 (4:105).

Akasema: Ewe Nuh! Huyo si katika watu wako. Hakika yeye ni mwendo usio mwema.”

Yaani ana mwendo usiokuwa mwema. Mwenyezi Mungu anamwambia Nuh kuhusu mwanawe kuwa nimekuamrisha uchukue watu wako katika Safina ispkokuwa niliokukataza. na yey- ote katika wao niliyekukataza basi ni kwa hekima niliyoipitisha na matakwa yangu yametaka mwanao awe ni miongoni mwa watakaoazama, kwa vile mwendo wake si mzuari. Hakika watu wa Mtume ni wale wema hata kama wako mbali kinasaba na madui zao ni waovu hata kama wako karibu kinasaba.

Maana haya yanatiliwa mkazo na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hakika watu wanaomkurubia zaidi Ibrahimu ni wale waliomfuata” Juz.3 (3:68).

Na hapo ndipo alipochukua Imam Ali (sa) kauli yake: “ Hakika mpenzi wa Muhammad ni yule anayemtii Mwenyezi Mungu hata kama yuko mbali naye kidamu na adui wa Muhammad ni yule anaye muasi Mwenyezi Mungu hata kama yuko karibu naye kiudugu”.

Mshairi naye anasema: Mapenzi ya Salmani kwao, udugu walishibana, Lakini Nuh na mwanawe katu hawakuwiyana

Basi usiniombe usilo na ujuzi nalo mimi ninakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa wajinga.”

Jambo ambalo hakuwa akilijua Nuh ni alivyopitisha Mwenyezi Mungu tangu mwanzo kuwa mwanawe atakuwa miongoni mwa watakaozama, kwa maslahi fulani; na alipomuomba Mola wake akamwambia usiniombe usilolijua, akasema:

Ewe Mola wangu! Hakika mimi ninajikinga kwako kukuombe nisilo na ujuzi nalo1

Yaani sitakuomba tena kuhusu mototo wangu baada ya kunifahamisha uhakika; bali ninaridhia hukumu yako na ulivyopitisha.

Na kama hutanisamehe na kunirehemu nitakuwa katika waliohasirika.

Hii ni kiasi cha unyeneyekevu wa Nuh tu kwa Mwenyezi Mungu, sio kutubia dhambi iliyofanyika. Ndivyo walivyo Mitume na watu wema. Tumelifafanua hilo katika Juz.4 (4:18) kifungu cha ‘Toba na maumbile.’

Ikasemwa: Ewe Nuh! Shuka kwa Salama itokayo kwetu na baraka nyingi juu yako na juu ya umma zilizo pamoja nawe; na zitakuwepo umma tutakazozistarehesha kisha zishikwe na adhabu chungu itokayo kwetu.

Tufani ilipokwisha na washirikina kuangamia, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Nuh ashuke ardhini yeye na wenzake aliokuwa nao kwa salama na baraka za maisha na riziki, waenee huku na huko kisha wazaane na upatikane umma mwingine; kama ilivyokujatokea wakapatikana Ad na Thamud, watastarehe kidogo duniani kisha wakapata adhabu kwa kufru yao na uasi wao.

Kigano Cha Mwezi 10, Muharram

Kinasema kigano kwamba Nuh alishuka kwenye Safina yake siku ya Ashura(10,Muharram) akafunga kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Naye alikuwa amemaliza chakula.

Akachanganya kofi moja la choroko (pojo), kofi moja la adesi na ngano hadi zikawa nafaka saba akazipika, wakala wote mpaka wakashiba. Basi kiganao hiki kikaenea katika miji na watu wakaifanya ni sunna siku ya Ashura.

Hizo ni habari za ghaibu tunazokupa wahyi. Hukuwa ukizijua wewe wala watu wako kabla ya hii. Basi subiri! Hakika mwisho ni wa wacha Mungu.

Msemo unaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.) Baada ya Mwenyezi Mungu kumwelezea kisa cha Nuh, alimwambia kuwa kisa hiki ni wahyi, hukukijua wewe wala maquraish. Kwa hiyo nawe vumilia kwa yatakayokupata kutoka kwa watu wako; kama alivyovumilia Nuh. Kama ambavyo mwisho ulikuwa wake na walioamini pamoja naye, basi vilevile mwisho utakuwa wako na waislam. Kwa sababu siku zote mwisho ni wa wenye kusubiri wenye kumcha Mwenyezi Mungu.

Tufani Imethibiti Kwa Uma Nyinginezo

Masimulizi ya Tufani ya Nuh hayahusiki na vitabu vya dini tu. Watafiti wamegundua mabaki ya mbao zinazoashiria kisa hiki na tarehe yake inarudi kwenye mwaka 2100 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (a.s.).

Wataalamu wengine wasiohusika na dini wamesema kuwa kisa cha Tufani kinajulikana na umma za kale za Wahindi, Wagiriki, Wajapani, Wachina, Wabrazili, watu wa Mexico na wengineo. Wanatofautiana katika masimulizi, lakini wanaafikiana katika madhumuni na kwamaba sababu ilikuwa ni kufuru ya watu na dhulma yao.

وَإِلَىٰ عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا ۚ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ ۖ إِنْ أَنْتُمْ إِلَّا مُفْتَرُونَ {50}

Na kwa A’ad (tulimpeleka) ndugu yao Hud, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye tu. Hamkuwa nyinyi isipokuwa ni wazushi.

يَا قَوْمِ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى الَّذِي فَطَرَنِي ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {51}

Enyi watu wangu! Siwaombi ujira juu ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa yule aliyeniumba, basi hamtumii akili?

وَيَا قَوْمِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُمْ مِدْرَارًا وَيَزِدْكُمْ قُوَّةً إِلَىٰ قُوَّتِكُمْ وَلَا تَتَوَلَّوْا مُجْرِمِينَ {52}

Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake, atawaletea mbingu zenye mvua tele na atawazidishia nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke kuwa waovu.

قَالُوا يَا هُودُ مَا جِئْتَنَا بِبَيِّنَةٍ وَمَا نَحْنُ بِتَارِكِي آلِهَتِنَا عَنْ قَوْلِكَ وَمَا نَحْنُ لَكَ بِمُؤْمِنِينَ {53}

Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi, wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kauli yako na wala sisi hatukuamini wewe.

إِنْ نَقُولُ إِلَّا اعْتَرَاكَ بَعْضُ آلِهَتِنَا بِسُوءٍ ۗ قَالَ إِنِّي أُشْهِدُ اللَّهَ وَاشْهَدُوا أَنِّي بَرِيءٌ مِمَّا تُشْرِكُونَ {54}

Hatuna la kusema ila baadhi ya miungu yetu imekutia balaa. Akasema: Hakika mimi ninamshuhudisha Mwenyezi Mungu na nyinyi shuhudieni kwamba niko mbali na hao mnaowashirikisha.

مِنْ دُونِهِ ۖ فَكِيدُونِي جَمِيعًا ثُمَّ لَا تُنْظِرُونِ {55}

Mkamwacha Yeye. Basi nyote nifanyieni vitimbi tena msinipe muda.

إِنِّي تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّهِ رَبِّي وَرَبِّكُمْ ۚ مَا مِنْ دَابَّةٍ إِلَّا هُوَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهَا ۚ إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ {56}

Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu Mola wangu na Mola wenu. Hakuna mnyama yeyote isipokuwa Yeye amemshika utosi wake. Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka.
  • 1. Zimegongana kauli za wafasiri wengi walivyofahamu, kutokana na Aya, kuwa Mungu anamwambia Nuh, usiniombe na Nuh naye anamwambia Mungu sijakuomba. Wakaleta taawili zao za kuwazia tu. Tuliyoyaeleza yanabainisha kuwa Aya iko wazi haihitaji taawili.