read

Ngamia Wa Mwenyezi Mungu Aya 64-68

Maana

Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu, ni ishara kwenu, basi mwacheni ale katia ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya isije ikawaangamiza adhabu iliyo karibu.

Imekwishatangulia tafsiri yake katika Juz.8 (7:73).

Wakamchinja. Basi Swaleh akasema: Stareheni katika mji wenu kwa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyokadhibishwa.

Swaleh (a.s.) aliwaamrisha waachane naye ngamia, lakini wakamchinja, basi akawaonya kushukiwa na ahabu kwa muda wa siku tatu.
Ibn Abbas anasema kuwa Mungu aliwapa muda huu kuwahimiza imani na kutubia, lakini wao waling’ang’ania ukafiri wao, kwa sababu hawakumwamini Swaleh na ahadi yake.

Ilipofika amri yetu tulimwokoa Swaleh na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu kutokana na hizaya ya siku hiyo. Hakika Mola wako ni mwenye nguvu mwenye kushinda.

Baada ya siku tatu, ilishuka adhabu, wakaokoka wauminii na wakaangamia makafiri, baada ya kuwasimamia hoja. Huu ndio mwisho wa kila mwenye kuzama katika upotevu na ufisadi.

Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao.

Hapa amesema ukulele ukawaangamiza na katika Juz.8 (7:78) amesema na mtetemeko ukawaangamiza. Maana ni kuwa ukelele ulileta mtetemeko na hofu katika nyoyo zao.

Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! Hakika Thamud walimkufuru Mola wao. Ehee! Thamud wamepotelea mbali.

Yani jinsi walivyoondoka haraka ni kama kwamba hawakukaa majumbani mwao, na wala hawakuzifaidi mali zao na watoto wao.
Hawakuicheka dunia bali imewacheka wao. Mwenye akili ni yule anayepata somo kutokana na mwengine.

وَلَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَىٰ قَالُوا سَلَامًا ۖ قَالَ سَلَامٌ ۖ فَمَا لَبِثَ أَنْ جَاءَ بِعِجْلٍ حَنِيذٍ {69}

Na wajumbe wetu walimjia Ibrahim na bishara, wakasema: Salaam! Naye akasema: Salaam! Hakukaa ila akaleta ndama aliyeokwa.

فَلَمَّا رَأَىٰ أَيْدِيَهُمْ لَا تَصِلُ إِلَيْهِ نَكِرَهُمْ وَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً ۚ قَالُوا لَا تَخَفْ إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمِ لُوطٍ {70}

Alipoona mikono yao hamfikii, aliwatilia shaka na akawahofia. Wakasem: usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut.

وَامْرَأَتُهُ قَائِمَةٌ فَضَحِكَتْ فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِنْ وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ {71}

Na mkewe kasimama wima akacheka. Tukampa bishara ya Is-haq na baada ya Is-haq, Ya’qub.

قَالَتْ يَا وَيْلَتَىٰ أَأَلِدُ وَأَنَا عَجُوزٌ وَهَٰذَا بَعْلِي شَيْخًا ۖ إِنَّ هَٰذَا لَشَيْءٌ عَجِيبٌ {72}

Akasema: Miye! Hivi nitazaa na hali mimi ni kikongwe na huyu mume wangu ni mzee? Hakika hili ni jambo la ajabu!

قَالُوا أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللَّهِ ۖ رَحْمَتُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ ۚ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَجِيدٌ {73}

Wakasema: Unastajabu amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake iko juu yenu enyi watu wa nyumba hii Hakika yeye ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa.