read

Aya 1 – 4: Kitabu Na Aya Zake

Maana

Alif Laam Raa.

Meelezo yake ni kama ya mwanzo wa Sura Baqara, Juz.1 (2:1) Mwenye kutaka arudie huko.

Hiki ni kitabu ambacho Aya zake zimepangwa kiuhakika, kisha zikafafanuliwa kutoka kwa mwenye hekima mwenye habari.

Makusudio ya Kitab hapa ni Qur’ani. Maana ni kuwa hii Qur’ani maana yake yako wazi na imepangwa vizuri. Haina upungufu wala makosa. Kwa sababu inatokana na mpangaji wa mambo anayoyaweka kwa misingi ya elimu na hekima.

Baadhi ya wajuzi wanasema kuwa Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili. Kitabu cha kiulimwengu ambacho ndio huu ulimwengu na kitabu cha kurasa ambacho ni hii Qur’ani. Kila kimoja kwa upande wake, kimepang- wa vizuri na kwa ukamilifu.

Wanazuoni wa dini mbali mbali wamezungumzia utukufu na umuhimu wa Qur’ani. Nimenukuu baadhi ya kauli zao katika kitabu changu Al-Islam Wal-Aql (uislam na akili) sehemu ya Utume.

Wakati nikifasiri Aya hii, imetokea sadfa ya kusoma makala inayohusiana na Kitabu kinachoitwa Muhammad cha mtaalam wa kifaransa anayeitwa Marksem Roudinseim. Iliyotolewa na gazeti la Al-Misriya la tarehe. 22, Desemba 1968.

Katika hiyo makala anasisitiza kuwa Qur’ani imewanukulia vizazi vinavyokuja kuhusu binadamu aliyekandamizwa jinsi alivyo jikakamua kutoka katika dhulma na ukandamizaji. Nayo imevipa silaha yenye nguvu ya kupambana na madhalim na wanafiki. Anaendelea kusema mtaalam huyo. “Hakika uislam ni itikadi na mfumo wa maisha na ni mtazamo kamili wa ulimwengu na binadamu.”

Kwamba msimuabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi kwenu ni muonyaji mbashiri ninayetoka kwake.

Makusudio ya mimi ni Muhammad (s.a.w.), muonyaji ni kuonya adhabu kwa anayeasi na mbashiri ni anayetoa habari njema ya thawabu kwa mtiifu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema kuwa Qur’ani ni Kitabu kili- chopangwa vizuri na kufafanuliwa, katika Aya hii anazungumzia Tawhid na kumfanyia ikhlas Mwenyezi Mungu peke yake katika ibada. Vilevile kuwa Muhammad (s.a.w.) ni muonyaji na mtoaji habari njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na kwamba mumtake maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.

Yaani mumwabudu Mwenyezi Mungu, mumwamini Muhammad (s.a.w.) na utume wake, mtake maghufira na mtubie. Tofauti ya kuomba maghfira na kutubia ni: kuomba maghufira ni kutaka kusamehewa yaliyopita, bila ya kuangalia chochote kijacho. Ama kutubia ni kuomba msamaha yaliyopita na kuahidi kutotenda tena maasi.

Atawastarehesha starehe nzuri mpaka muda maalum na atampa kila mwenye fadhila fadhila yake.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuamrisha Ikhlas, kuamini utume wa Muhammad (s.a.w.), kuomba maghfira na kutubia, anataja kwamba malipo ya watiifu katika dunia sio kung’ongolewa kama walivyoong’olewa makafiri waliokuwa kabla yao; bali atawabakisha mpaka muda wao. Ama malipo yao huko akhera ni thawabu kwa kila mtu kulingana na matendo yake, yawe mengi au machache.
Na ikiwa mtakengeuka basi mimi nawahofia adhabu ya siku kubwa kutokana na vituko vyake na shida yake, nayo ni malipo ya kila mwenye kuikataa haki.

Marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mwenye uwezo juu ya kila kitu.
Na kwa uwezo wake atawafufua wafu, awakusanye kwa ajili ya hisabu na amlipe kila mmoja stahiki yake. Ni muweza kwa waja wake wote.

أَلَا إِنَّهُمْ يَثْنُونَ صُدُورَهُمْ لِيَسْتَخْفُوا مِنْهُ ۚ أَلَا حِينَ يَسْتَغْشُونَ ثِيَابَهُمْ يَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ {5}

Sikilizeni! Hakika wao wanakunja vifua vyao ili wamfiche. Sikilizeni! Wanapojigubika nguo zao anajua wanayoyaficha na wanayoyadhihirisha. Hakika yeye ni Mjuzi, wa yaliyomo vifuani.