read

Aya 101 – 106: Ishara Na Maonyo Hayatoshi

Maana

Sema, Angalieni yaliyomo mbinguni na ardhini.

Kwa mnasaba wa kutaja imani katika Aya iliyotangulia, hapa Mwenyezi Mungu anaamrisha kuangalia ulimwengu na maajabu yake. Kwa sababu hiyo ndiyo njia ya kumjua Mwenyezi Mungu na kumwamini. Zimekwishatangulia Aya nyingi zenye mfano huu.

Na ishara zote na maonyo hayawafai watu wasioamini.

Kila dalili ya haki huwa inamuonya kwa adhabu anayeihalifu, na kila Mtume atokaye kwa Mwenyezi Mungu huwa na dalili ya ujumbe wake. Lakini dalili na Mitume haifai kitu isipokuwa kwa yule ambaye haki kwake ni kitu kilichompotea, anaichukua popote atakapoipata, hata kama ni kwa kupoteza maisha.

Ama yule ambaye haangalii katika dini, haki na utu, isipokuwa maslahi yake na manufaa yake tu, basi huyo ni adui wa dalili, hoja Mitume na hata viongozi wema.

Basi je, hawangojei isipokuwa mfano wa siku za watu waliopita kabla yao?

Siku za watu ni siku za utawala wao au siku za misukosuko yao. Na waliopita kabla yao hapa ni watu wa Nuh, A’d na Thamud na wanaongojea ni wale waliomkadhibisha Muhammad (s.a.w.) kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Sema, basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi kati- ka wenye kungojea.

Kisha tunawaokoa Mitume wetu na wale walioamini.

Jumla hii inaungan na jumla iliyokadiriwa, kuwa imepita desturi ya Mwenyezi Mungu kuwapeleka Mitume kwa watu kuwapa bishara na kuwaonya. Baadhi wanawaamini na wengine wanawakidhibisha. Huangamizwa wanaopinga kisha wanaokoka Mitume na waliowaamini. Mwenye Tafsir Al-Manar anasema hii ni miongoni mwa muujiza wa ufasaha wa Qur’ani. Muujiza wenyewe ni kutajwa jumla moja inayofahamisha jumla kadhaa ambazo hazikutajwa.

Ndio kama hivyo inatustahiki kuwaokoa waumini.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema kuwa yeye anaokoa waumini, hapa anasema huko kuokolewa ni haki yao. Na kwamba ni juu ya Mwenyezi Mungu kuwapatia haki yao hiyo. Hili ni jibu wazi la wale waliosema kuwa Mwenyezi Mungu ni haki yake kumwadhibu mtiifu na kumpa thawabu muasi, kama ilivyosemwaa katika kitabu Al-Mawaqif Juz 8.

Sema, Enyi watu! Ikiwa mnayo shaka katika dini yangu, basi mimi siwaabudu wale mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, bali ninamwabudu Mwenyezi Mungu ambaye anawafisha nyinyi na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kuamini.

Mtume Muhammad (s.a.w.) amekwishaitekeleza amana ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake, akawafikishia ujumbe wa Mola wao.Wakamwitikia waliomwitikia na wakakataa waliokataa.Mwenyezi Mungu amemwamrisha awambie wale waliong’ang’ania ushirikina, kwamba kama mnashaka na dini yangu, basi mimi siabudu masanamu yasiyokuwa na akili, kama mnayoyafanya, isipokuwa ninamwabudu Mola mwenye uweza, mwadilifu, mwenye hekima na Mjuzi. Na yeye ndiye anayezichukua roho zenu. Basi ni nani anayefaa kutiliwa shaka?

Huu ni miongoni mwa mifumo ya kulingania kwa hekima na mawaidha mazuri.

Na kwamba elekeza uso wako kwenye dini ya kweli wala usiwe miongoni mwa washirikina.

Makusudio ya uso hapa nia nafsi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ameniamrisha kumwelekea yeye nikiwa mwislam kwa kufuata nyayo za Mitume wengine kwa kauli na vitendo.

Wala usiwaombe wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawakunufaishi wala kukudhuru, kama ukifanya basi hapo utakuwa miongoni mwa madhalimu.
Ni muhali kwa Mtume kumwomba mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Isipokuwa makusudio hapa ni kumpa habari anayeomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kuwa yeye ni miongoni mwa waliopata hasara.

Ilivyo ni kuwa Aya hizi tatu za mwisho zina maana moja kwa ibara tofauti. Nayo ni kuamrisha imani na kukataza ushirikina. Aya ya kwanza imeamrisha imani na kuashiria kuwa dini ya Tawhid haifai kuitilia shaka na kwamba dini yenye wasiwasi na shaka ni ile ya ushirikina na kuabudu sanamu.

Aya ya pili imeamrisha imani pamoja na kuashiria kuwa Uislam ndiyo dini isiyokuwa kombo kombo, kinyume na dini nyingine. Na Aya ya tatu ikamrisha imani na kutoa ishara kuwa ambaye atafuata dini nyingine isiyokuwa Uislam, basi ni katika madhalim waliojidhulumu wenyewe.

Ni desturi ya Qur’ani kukariri na kulisisitiza kila linaloambatana na itikadi na misingi yake.

وَإِنْ يَمْسَسْكَ اللَّهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِنْ يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ ۚ يُصِيبُ بِهِ مَنْ يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {107}

Na Mwenyezi Mungu akikugusisha dhara basi hakuna wa kuiondoa isipokuwa yeye. Na kama akikutakia kheri, basi hakuna wa kurudisha fadhila yake. Huifikisha kwa amtakaye katika waja wake, Naye ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَكُمُ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ۖ وَمَا أَنَا عَلَيْكُمْ بِوَكِيلٍ {108}

Sema, Enyi watu! Haki imekwishawafikia kutoka kwa Mola wenu. Basi anayeongoka hakika anaongoka kwa faida ya nafsi yake tu, na anayepotea anapotea kwa hasara ya nafsi yake tu. Na mimi si mwakilishi juu yenu.

وَاتَّبِعْ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ وَاصْبِرْ حَتَّىٰ يَحْكُمَ اللَّهُ ۚ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ {109}

Na ufuate yale unayopewa wahyi, na vumilia mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu, na yeye ndiye Mbora wa mahakimu.