read

Aya 107 – 109: Kama Mwenyezi Mungu Akikugusisha Dhara

Maana

Na Mwenyezi Mungu akikugusisha dhara basi hakuna wa kuiondoa isipokuwa yeye.

Mtu anaweza kupata madhara kutokana na yeye mwenyewe; kama vile mtu kujidharau au kuacha kufanya kazi na uwezo anao au kufanya kazi bila ya maandalizi. Madhara ya aina hii hayafai kuyanasibisha kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu ameamrisha kufanya maandalizi kwa kazi yoyote na amekataza aina zote za madhara.

Mara nyingine Mtu anapata madhara kwa sababu ya ufisadi wa jamii anayoishi. Madhara haya vilevile hayafai kuyanasibisha kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amekataza ufisadi na ameamrisha utengeneo.

Au anaweza kudhurika sio kutoka na yeye mwenyewe wala jamii; kama kuzaliwa na upungufu wa maumbile au akili pungufu, kiasi cha kushindwa kujua mambo ya elimu. Au kupigwa na radi n.k. Aina hii ya madhara ndiyo iliyokusudiwa katika Aya, ingawaje aina zote za madhara Mwenyezi Mungu anaweza kuziondoa. Kwa sababu yeye ni Mjuzi, wa kila kitu.

Na kama akikutakia kheri, basi hakuna wa kurudisha fadhila yake. Huifikisha kwa amtakaye katika waja wake.
Tumetangulia kueleza kuwa haifai kunasibisha madhara kwa Mwenyezi Mungu na Mtume moja kwa moja. Ama heri inafaa kuinasibisha kwa Mwenyezi Mungu, ni sawa iwe imetokana na athari ya matendo ya binadamu.

Kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu anataka heri na anaiamrisha. Na yeye ndiye mwenye uweza zaidi kwa mtu.

Naye ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.

Na rehema zake zimeenea kila kitu, kama ilivyo elimu yake na uwezo wake.

Sema: Enyi watu! Haki imekwishawafikia kutoka kwa Mola wenu. Basi anayeongoka hakika anaongoka kwa faida ya nafsi yake tu, na anayepotea anapotea kwa hasara ya nafsi yake tu. Na mimi si mwakilishi juu yenu.

Muhtasari wa maana ya Aya hii uko katika Aya isemayo: “Kila mtu ni rehani ya alichokikimu.” (52:21) Pia umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:104)

Na ufuate yale unayopewa wahyi, na vumilia mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu, na yeye ndiye Mbora wa mahakimu.

Aya hii inaelezea wadhifa wa Mtume katika kufikisha wahyi, kuufanyia kazi na kuvumilia maudhi atakayoyapata katika kazi hiyo mpaka Mwenyezi Mungu aidhihirishe dini yake na neno lake liwe juu. Na haya ni muhimu kwa kila atakayekuwa naibu wa maasum katika kufikisha hukumu za Mwenyezi Mungu na kuzieneza.