read

Aya 113 – 114: Abu Twalib Na Kuwatakia Msamaha Washirikina

Kushuka Aya

Watu wamesema mengi kuhusu Uislamu wa Abu Twalib, ami yake Mtume (s.a.w.). Kauli zimetofautiana na viko vitabu vya zamani na karibuni kuhusu suala hilo. Vile vile maudhui haya yaliwahi kutolewa katika kurasa za gazeti la Majallatul-Arabi Na 108 na 110.

Wanaosema kuwa alisilimu, wametoa dalili kwa yale aliyopambana nayo kutoka kwa vigogo vya maquraish na kauli zake katika kumsifu Mtume kishairi n.k. Ama wale waliosema kuwa alikuwa mshirikina, walitoa dalili kwa riwaya inayosema kuwa Aya mbili hizi zilishuka kuhusiana na Abu Twalib.

Nilipofika hapa kufasiri, nilifuatilia riwaya na kauli katika vitabu vya zamani na vya sasa kuhusu sababu za kushuka Aya mbili hizi, nikatoka na natija kuwa wapokezi na wafasiri wametofautiana kwenye kauli tatu kuhusu sababu za kushuka Aya hizi.

Kauli Ya Kwanza

Kuwa jamaa katika Waumini walisema, tuwatakie msamaha wafu wetu washirikina; kama alivyomtakia msamaha Ibrahim baba yake, ndipo zikashuka Aya mbili hizi.

Haya yametajwa na Tabari, Razi na Abu Hayan Al-andalusi. Vile vile mwenye Tafsiri Al-manar na wengineo.

Kauli hii ina nguvu kuliko kauli nyingine, kwa sababu katika Aya hizo kuna matamko yanayofahamisha hivyo; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu “… na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina ijapokuwa jamaa …”

Kwa hiyo kukatazwa waumini kuwatakia msamaha jamaa zao, washirikina, kunatambulisha kuwa wao walikuwa wakiwatakia msamah au walijaribu kufanya hivyo.

Vile vile kauli isemayo: “Na haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake …”

Hilo ni jawabu la kauli ya waumini waliposema: Kama alivyomtakia msamaha Ibrahim baba yake.

Kauli Ya Pili

Kwamba Mtume (s.a.w.) alikwenda kwenye kaburi la mama yake akalia, na kumtaka idhini Mola wake amwombee msamaha, ndipo zikashuka Aya mbili hizo. Kauli hii wameitaja wale tuliowanukuu kwenye kauli ya kwanza.

Kauli hii inaizidi ile isemayo kuwa zilishuka wakati wa kufa Ami yake Abu Twalib. Kwa sababu Abu Twalib alikufa Makka katika mwaka wa huzuni miaka mitatu kabla ya Hijra, na Sura ya Tawba yenye Aya hizo mbili ilishu- ka Madina mwaka wa 9 Hijra – miaka 12 tangu kufa AbuTwalib.

Kauli Ya Tatu

Kwamba Aya mbili hizi zilishuka kwa Abu Twalib kwa madai ya kwamba Mtume alimwambia Ami yake, AbuTwalib akiwa karibu ya kukata roho: “Ewe Ami sema: “Lailaha illa llah” lakini hakusema, Mtume akasema: “Nitakuombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu maadamu sijakatazwa”

Kauli hii imejibiwa na kundi la maulama kwa kauli mbili: Kwanza, kuwa Aya mbili, kama tulivyodokeza, zilishuka baada ya kufa Abu Twalib.

Pili, kwamba Abu Twalib alikufa baada ya kusilimu na kuufanyia ikhlasi Uislamu wake. Tazama kitabu Al-Ghadiri cha Aminiy J7 Uk 369 chapa ya mwaka 1967.

Hali Halisi

Kama tukiachana na kauli za wafasiri na wapokezi, tukaiweka itikadi ya Abu Twalib kutegemea alivyokuwa, kulingana na mambo yalivyo, basi natija itakuwa kwamba Abu Twalib alikuwa akiamini utume wa Muhammad (s.a.w.) katika kauli zake zote na vitendo vyake. Na huo ndio Uislamu hasa.

Mtume aliinukia akiwa ni yatima wa baba na mama – Baba yake alikufa akiwa yuko tumboni na inasemekana kuwa alikuwa mtoto mchanga. Mama yake akafa akiwa na miaka sita. Akabaki katika malezi ya babu yake, Abdul Muttwalib, kiasi cha miaka minane.

Babu yake alipofikiwa na mauti alimkabidhi kwa Abu Twalib. Abu Twalib hakuwa ndiye mtoto mkubwa wa Abdul Mutwalib, wala hakuwa na mali nyingi isipokuwa alikuwa ndiye mwenye heshima, mwenye hulka nzuri na mkarimu sana kuliko ndugu zake wote.

Kwa hiyo Abu Twalib akamlea vizuri; akampenda sana kuliko watoto wake; alitunga kasida ndefu na fupi kumsifu; alikuwa akitabaruku naye na akimtegemea wakati wa balaa kutokana na karama zilizodhihiri kwake.

Imepokewa kutoka kwa Ibn Asakir, kwamba watu wa Makka walipatwa na kahati; akatoka Abu Twalib na Muhammad akiwa ni kijana akaomba mvua kwa uso wake. Ikabubujika mvua na ardhi ikarutubika.

Ismail Haqqi anasema katika Rawhilbayaan katika kufasiri (12:45): “Abu Twalib alimlea na kumhami Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na kumtetea katika uhai wake”.

Ilivyo ni kwamba yeye ni miongoni mwa waliokuwa na imani kama ilivyotangulia kuelezwa.

Je, Kuna Siri Gani?

Ikiwa Abu Twalib anampenda Muhammad, anajitolea kwa nafsi yake na kuwa tayari kufa ili amsaidie, kutegemea ukweli wake na msimamo wake, naye aliona aliyoyaona katika karama zake, kabla ya utume na baada ya utume, kwa nini basi asiamini utume wake?

Ikiwa ni kweli madai ya kuwa Abu Twalib si Mwislamu basi itabidi kuweko na siri iiyomzuia kuwa Mwislamuu Je, ni siri gani hiyo? Je, Abu Twalib, aliyekuwa akimjua kiuhakika Muhammad, alimwona na mambo yanayopingana na Utume? Hapana! Mwenye kudai hivyo si Mwislamu kabisa!

Kisha itakuwaje Muhammad (s.a.w.) aweze kuwakinaisha wachunga ngamia na wale waliokuwa hawajui chochote zamani, lakini ashindwe kumkinaisha ami yake, Abu Twalib ambaye alikuwa akimjua chimbuko lake?

Je, Abu Twalib alikuwa na akili ndogo kuliko Bedui wa jangwani, au alikuw ana tamaa iliyomzuia kusilimu, kama walivyozuilika wenye tamaa? Matamanio ambayo yangeweza kumzuia Abu Twalib kuingia Uislamu ni moja kati ya mambo mawili: Ama kuhofia mali yake na utajiri wake, na ilivyo ni kwamba Abu Twalib aliishi maisha ya kifukara na alikufa fukara. Au itakuwa ni kuhofia kuondokewa na uongozi katika nyumba ya Hashim nk, na ni kinyume cha hivyo.

Ikiwa sababu hizo mbili hazipo, na tukiunganisha kukosekana sababu na mambo yanayoelekeza Uislamu wake, ambayo ni kumpenda kwake Muhammad na kujua uhakika wake, basi natija ni kwamba Abu Twalib sio tu kuwa alisilimu bali ni katika waislamu wa mwanzo.

Vile vile ikiwa itabatilika kauli kuwa Aya mbili zilimshukia Abu Twalib na haikuthibitika riwaya sahihi kwamba zilishuka kwa sababu ya mama wa Mtume, basi itabakia kauli ya kwanza, kwamba ziliwashukiwa watu waliokuwa au waliojaribu kuwaombea msamaha watu wao; na dhahiri ya Aya mbili inaliweka wazi hilo.

Maana

Haimfalii Mtume na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina ijapokuwa ni jamaa,

Imeelezwa katika Tafsir Tabari haya yafuatayo; ninanukuu: “Watu katika maswahaba wa Mtume (s.a.w.) walisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Katika mababa zetu wako waliokuwa na ujirani mwema, wakiunga udugu, wakisadia na kutekeleza madeni; je, tuwatakie msamaha? Akasema: Kwa nini isiwe hivyo, nami nitamtakia msamaha baba yangu, kama Ibrahim alivyomtakia msamaha baba yake. Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hiyo.”

Utauliza kuwa itakuwaje Mtume (s.a.w.) atoe idhini kwa masahaba zake kuwatakia maghufira baba zao washirki na ikiwa ni haramu?

Jibu: Kila kitu ni halali mpaka kikatazwe; na wakati Mtume alipotoa idhini kuombea msamaha hakukuwa kumekatazwa; baada ya kukatazwa, aliwakataza.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anabainisha sababu za kukataza kwa kusema:

Baada ya kuwabainikia kuwa wao ni watu wa motoni.

Aya hii inatufahamisha kuwa mtu anahukumia ukafiri wake na imani yake kutokana na dhahiri ya hali yake, na kwamba ambaye dhahiri yake ni ukafiri basi haifai kumtakia msamaha wala kumrehemu.

Utauliza: Ikiwa kuwaombea msamaha washirikina ni haramu, kwanini Mtume aliwaombea msamaha watu wake walipomvunja meno na wakamchana uso wake? Imethibitika kwamba yeye alisema: “Ewe Mola Wangu! Wasamehe watu wangu, kwani wao hawajui.”

Wafasiri wengi wamelijibu swali hii kwamba Aya imekataza kutakiwa msamaha washirikina waliokufa, sio waliohai wanaotarajiwa imani yao.

Jibu tunaloliona ni kwamba kutaka msamaha kwa Mtume (s.a.w.) kulikuwa ni kusamehe haki yake ya kibinadamu, sio kusamehe haki ya Mwenyezi Mungu na maghufira kwa ushirikina.

Na, hakuna mwenye shaka kwamba inafaa kwa mtu kusamehe haki yake, inayomhusu yeye tu, kwa mwislamu na kafiri.

Swali la pili, Ibrahim alikuwa akimlingania baba yake kwenye imani na kumhimiza na kumwahidi kumtakia msamaha; kama asemavyo Mwenyezi Mungu:

إِلَّا قَوْلَ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ لَأَسْتَغْفِرَنَّ لَكَ وَمَا أَمْلِكُ لَكَ مِنَ اللَّهِ مِنْ شَيْءٍ ۖ {4}


“… Ila kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Hakika nitakuombea msamaha, wala similiki chochote kwa ajili yako mbele za Mwenyezi Mungu…”(60:4)

Naye alitekeleza ahadi yake hii na akamwombea msamaha kwa kusema:

رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ {41}


“Ewe Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wawili na waumini, sikuyakusimamahisabu.”(14:41)

Sasa vipi Ibrahim (a.s.) alimtakia msamaha baba yake, ambapo kumtakia msama mshirikina hakufai? Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amejibu swali hilo kwa kusema:

Na haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila ni kwa sababu ya ahadi aliyofanya naye, lakini ilipompambanukia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye.

Yaani Ibrahim (a.s.) alimtakia msamaha baba yake kwa vile tu, alimwahidi kuwa atamwamini Mungu. Alipovunja ahadi na kumbainikia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu alijiepusha naye.

Sio mbali kuwa dua ya Ibrahim (a.s.) kwa baba yake, ni sawa na dua ya Muhammad (s.a.w.) kwa watu wake washirikina; yaani kusamehe haki yake ya kibinadamu, sio haki ya Mwenyezi Mungu na kutakia msamaha ushirikina.

Hilo linatambulika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu.

Hakika Ibrahim alikuwa Mpole sana wa moyo mvumilivu.

Mpole wa moyo ni yule mnyenyekevu na mvumilivu ni yale anayesamehe akiwa na uwezo. Na, Ibrahim alisamehe kauli ya baba yake:

لَئِنْ لَمْ تَنْتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ ۖ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا {46}


“Usipokoma nitakupiga mawe, na niondokelee mbali kwa muda mhache.” (19:46)

وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُضِلَّ قَوْمًا بَعْدَ إِذْ هَدَاهُمْ حَتَّىٰ يُبَيِّنَ لَهُمْ مَا يَتَّقُونَ ۚ إِنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {115}


Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwapoteza watu baada ya kuwaongoza; mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo Hakika Mwenyezi Mungu anajua kilakitu.

إِنَّ اللَّهَ لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۚ وَمَا لَكُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ {116}


Hakika Mwenyezi Mungu ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, huhuisha na hufisha; nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipokuwa MwenyeziMungu.