read

Aya 128 – 129: Kwa Waumini Ni Mpole

Maana

Hakika amewajia Mtume kutokana na nyinyi wenyewe.

Msemo huu anaambiwa kila mwanadamu anayetafuta uhakika na kutaka kuongozwa kwake. Mtume ni Muhammad bin Abudullah (s.a.w.), aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kwa watu wote kuwaokoa na ujinga na upotevu na kuwaongoza kwenye njia ya haki na heri.

Analotakiwa kufanya mwenye kutaka njia ya heri na haki ni kuangalia kwa ufahamu tu sera ya Muhammad (s.a.w.) na desturi yake na Kitabu alichokuja nacho kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Walimwamini mamilioni tangu zamani na sasa, wakiwemo maulama na wanafalsafa walioacha dini ya mababa na mababu, wakakubali Uislamu baada ya kutulia akili zao na nyoyo zao na kumuona Mtume wake mtukufu, kama alivyomsifu Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:

Yanamhuzunisha yanayowataabisha, anawahangaikieni sana, kwa Waumini ni mpole, mwenye huruma.

Anahuzunika kwa kila baya linalomfika yeyote aliye ardhini; hata kama ni mnyama; mwenye kuhangaikia uwongofu na wema wa watu wote. Ama upole wake na rehema yake imewaenea watu wote:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ {107}


“Nasihatukukutumailauwerehemakwawalimwengu wote.”(21:107).

Na miongoni mwa Hadith zake ni: “Mimi ni rehema niliyetolewa zawadi”

“Wenye huruma huwarehemu Mwenyezi Mungu.” “Wahurumieni walio katika ardhi watawahurumia walio katika mbingu”.

Utauliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema kwa Waumini ni Mpole mwenye huruma. Na katika Aya nyingine anasema: Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote; yaani waumini na wasiokuwa waumini. Sasa zinaungana vipi Aya mbili?

Jibu: Makusudio ya kauli yake “Nasi hatukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote,” ni kuwa dini ya Muhammad ni dini ya ubinadamu na sharia yake ni rehema kwa watu wote. Lau kama watu wangelifuata na wakaitumia ardhi ingelijaa heri na uadilifu.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: “Kwa waumini ni Mpole,” maana yake ni kwamba yeye ni Mpole sana na mwenye huruma kwa anayeamini haki na akajizuia kuwaudhi watu.

Ama anayewafanyia uadui na kuichezea haki yeye anamchukulia ugumu wala hamfanyii upole.

Hii nidyo dini ya utu na rehema. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekataza upole katika kutekeleza hadi (adhabu) kwa wakosaji. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ ۖ وَلَا تَأْخُذْكُمْ بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ {2}


“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni, kila mmoja katikawao,mijeledimiawalaisiwashikehurumakwaajiliyaokatikahukumu yaMwenyeziMungu

(24:2)

Anasema Ibin Al-Arabi katika Kitabu Futahahtuli-Makkiyya J2 “Makusudio ya waumini ni wenye kuamini haki na batili, sio wenye kuamini haki tu.” Lakini haya ni katika mambo ya kisufi.

Basi wakikengeuka, sema: Anitoshelezeaye ni Mwenyezi Mungu, hakuna Mola (apasaye kuabudiwa) ila yeye tu; kwake ninategemea; naye ndio bwana wa Arshi tukufu.

Hio ndiyo kazi ya Mtume – kufikisha tu. Mwenye kuongoka ni faida yake na mwenye kupotea ni hasara yake mwenyewe.

Mtume (s.a.w.) alikuwa na yakini kabisa kwamba Mwenyezi Mungu anamtosha, na ndiye anayempa nguvu za ushindi wake, kwa sababu anamtegemea yeye peke yake.

Tutamalizia Sura hii kwa alivyomalizia Mwenye Tafsir Al-Manar, aliposema:

“Ama uteuzi wake Mwenyezi Mungu mtukufu kwa Bani Hashim, ni kwa kuwa walikuwa wanatofautiana na Maquraishi wote kwa fadhila na ukarimu. Hashim ndiye aliyekuwa mwenye msafara wa Maquraish ambao aliuchukulia ahadi kuuwahami kutoka kwa Kizair wa Roma katika msafara wa kaskazi; na kutoka serikali ya Yemen katika msafara wa kusi.

Yeye ndiye wa mwanzo kuwalisha mafukara na mahujaji wote mkate na mchuzi, Na alimpa malezi ya ukarimu mtoto wake, Abdul-Muttwalib. Kwa ujumla ni kuwa Bani Hashim walikuwa ni wenye tabia njema kuliko Maquraish wote, walikuwa hawana kiburi wala ubinafsi.

Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa Aya ya mwisho kushuka ni hii: “Anitoshelezeaye ni Mwenyezi Mungu, hakuna Mola (apasaye kuabudiwa) ila yeye tu; kwake ninategemea; naye ndio bwana wa Arshi tukufu”