read

Aya 57 – 60: Yamewajia Mawaidha

Maana

Enyi watu! Hakika yamewafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu, na ponyo la yale yaliyomo vifuani mwenu na mwongozo na rehema kwa waumini.

Sifa hizi mawaidha, ponyo, mwongozo, na rehema ni sifa za Qur’ani Tukufu, na lengo la kuzitaja ni kuwajibu washirikina na kila mwenye kukitilia shaka Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukikataa.

Njia ya majibu hayo ni kwamba Qur’ani inaonya watu kwa mawaidha mazuri, inaponya nyoyo kutokana na hawaa na uchafu, inaogoza watu kwenye lile lililo sawa nayo ni rehma inayomuokoa na mangamizi na adhabu, yule atakayeitumia. Kwa hivyo basi atakayeikataa, atakuwa amekataa misingi hii ambayo ndiyo mihimili ya haki na heri na njia ya uwokovu.

Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake, basi nawafurahi. Hayo ni bora kuliko yale wanayoyakusanya.

Yaani mwenye akili hafurahi kwa mali na starehe za maisha haya ya dunia, isipokuwa anastarehe kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake. Wafasiri wamerefusha maneno sana kuhusu maana ya fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake na wakabainisha tofauti kati ya maneno mawili hayo.

Mfumo wa Aya unafahamisha kuwa makusudio yake hapa ni kuongoza kwenye njia ya heri na kuokoa; sawa na ilivyo fadhila na rehema katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, lingedhamiria kundi katika wao kukupoteza” Juz.5 (4:113).

Kwa hiyo kauli yake ‘kukupoteza’ inafahamisha kuwa makusudio ya fadhila yake na rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni uwongofu au kuthibitisha kwenye huo uwongofu, kwa sababu ndio kinyume cha upotevu. Mfano mwingine ni Aya isemayo: Kisha mligeuka baada ya haya.“Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Zake, mngelikuwa miongoni mwa wenye kuhasirika.” Juz.1 (2:64)

Sema: Je, mwaonaje zile riziki alizowateremshia Mwenyezi Mungu, kisha mkafanya katika hizo nyingine haramu na nyingine halali?

Maana ya Aya hii yako karibu na maana ya Aya iliyo Juz.7 (5:103) ambayo Tafsiri yake imekwishaelezwa.

Maana yanayopatikana ni kwamba Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake kuwaambia washirikina wa Makka ambao walifanya katika wanyama Bahira na Saiba (ngamia aliyezaa mimba kumi na ngamia wa nadhiri), kuwa hebu niambieni.

Ni jambo gani liliwafanya kufanya halali na haramu katika zile riziki alizowapa Mwenyezi Mungu; mpaka mkagawa mafungu haya?
Swali hapo ni la kukanusha; yaani Mwenyezi Mungu hakujalia hivyo kabisa, bali hayo yanatokana na nyinyi wenyewe peke yenu ndio mmeharamisha mliyo yaharamisha.

Sema: Je, Mwenyezi Mungu amewaruhusu au mnamzulia Mwenyezi Mungu uwongo?

Haiwezekani kudai kuwa Mwenyezi Mungu amewaruhusu hivyo, kwa hiyo nyinyi mnamzulia tu.

Nini dhana ya wale wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu juu ya siku ya Kiyama?

Yaani je, wanafikiria wale wanaojihalalishia na kujiharamishia kuwa Mwenyezi Mungu atawaacha kesho bila ya kuwaadhibu kutokana na uwongo na uzushi wao? Kama ni hivyo basi itakuwa hakuna tofauti kati ya mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na mwenye kuasi.

Itakuwaje hivyo na hali Mwenyezi Mungu amesema: “Je, tuwafanye walioamini na kutenda mema kuwa sawa na wafisadi ardhini? Au tuwafanye wenye takua kuwa sawa na waovu?” (38:28). Kusuta huku ni katika ufasaha zaidi wa kushtua na kutoa kiaga.

Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu kwa yale aliyowaneemesha katika akili na sharia inayowaamrisha heri na kuwakataza shari.

Lakini wengi wao hawashukuru.

Yaani hawajui kwa kutumia akili wala kwa hukumu ya sharia.

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِنْ قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ ۚ وَمَا يَعْزُبُ عَنْ رَبِّكَ مِنْ مِثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِنْ ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُبِينٍ {61}

Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur’ani, wala hamtendi kitendo chochote ila sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnaposhughulika nacho. Na hakifichikani kwa Mola wako chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimokatika kitabu kinachobainisha.

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ {62}

Juweni kuwa mawalii wa Mwenyezi Mungu hawana hofu wala wao hawahuzuniki.

الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ {63}

(Hao) ni ambao wameamini na wakawa na takua.

لَهُمُ الْبُشْرَىٰ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۚ لَا تَبْدِيلَ لِكَلِمَاتِ اللَّهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ {64}

Wao wana bishara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hakuna mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa.