read

Aya 65 – 70: Enzi Yote Ni Ya Mwenyezi Mungu

Maana

Wala isikuhuzunishe kauli yao. Hakika enzi yote ni ya Mwenyezi Mungu.

Enzi hapa ina maana ya nguvu na ushindi.

Walipagawa wakubwa kutokana na mwito wa Mtume Muhammad (s.a.w.) kwenye uadilifu na usawa na kuharamisha dhulma na ukandamizaji. Walipagawa na mwito huu kwa sababu ulikuwa ukiingilia enzi yao na utajiri wao. Kwa hiyo wakajaribu kumzuia na kupambana naye.

Mwanzo wa mapambano yao ulikuwa ni uzushi na kueneza uvumi. Wakasema ni mwenda wazimu, lakini hakuna aliyewaamini, wakasema ni mchawi, lakini hali halisi ikawafanya waongo. Ndipo wakadhamiria kumuua, wakawa wanashauriana katika njia ya kummaliza.

Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake usijali na yale wanayoyasema na wanayoyapanga kuhusu wewe, kwani nguvu na utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu, sio wa jaha wala mali. Yeye ndiye ambaye humtukuza amtakaye na humdhalilisha amtakaye. Na atawaadhibu wale waliokukadhibisha na kukuambia waliyokuambia na hawatapata msaidizi wala mlinzi atakayewakinga na adhabu na ghadhabu za Mwenyezi Mungu.

Yeye ndiye mwenye kusikia uzushi wao juu yako Mjuzi, wa njama wanazozipanga juu yako na yeye anawagonja.

Unaweza kuuliza kuwa Aya hii imefahamisha kuwa ushindi wote ni wa Mwenyezi Mungu peke yake, Kuna Aya isemayo:

وَلِلَّهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ {8}

“Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye enzi na Mtume wake, na Waumini.” (63:8).

Jibu: Enzi ya Mtume na ya Waumini inatokana na Mwenyezi Mungu; wana nguvu za ushindi kutokana na yeye na kwake wanategemea.

Juweni kuwa ni wa Mwenyezi Mungu wote waliomo mbinguni na waliomo ardhini.

Mwenye kuwa na yote hayo ana uwezo wa kumnusuru Mtume wake na kumpa nguvu mbele za maadui zake. Mwenyezi Mungu amesema: waliomo na wala hakusema vilivyomo, kwa sababu mazungumzo yanawahusu washirikina ambao wamemzulia uwongo Mwenyezi Mungu

Na wale wanaomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu hawawafuati kuwa ni washirika, wa Mungu.

Ukiwa unamfuata mtu kwa kuitakidi kuwa yuko sawa na akawa amepotea, basi utakuwa hufuati usawa bali unafuata upotevu. Hivyo ndivyo ilivyo wanaoabudu masanamu kwa kuitakidi kuwa ni washiriki wa Mwenyezi Mungu. Kwa hakika hasa ilivyo, ni wao hawaabudu washirika wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu sio washirika wa Mwenyezi Mungu kiuhakika.

Maana haya yanafafanuliwa na kauli yake Mwenyezi Mungu. Hawafuati ila dhana tu, na hawasemi ila uwongo tu, kauli ya hawasemi ila uwongo tu, inatia nguvu kauli ya hawafuati isipokuwa dhana tu. Umetangulia mfano wa Aya hii na maelezo yake katika Aya 28 ya Sura hii.

Yeye ndiye aliyewafanyia usiku ili mtulie humo na mchana wa kuonea. Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaosikia.

Mchana ni wa kuona ili tujishughulishe kwa kazi na usiku ni giza ili tupumzike kutokana na mihangaiko ya mchana. Ufafanuzi zaidi wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu.

وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ آيَتَيْنِ ۖ فَمَحَوْنَا آيَةَ اللَّيْلِ وَجَعَلْنَا آيَةَ النَّهَارِ مُبْصِرَةً لِتَبْتَغُوا فَضْلًا مِنْ رَبِّكُمْ {12}

“Na tumeufanya usiku na mchana ni ishara mbili, kisha tukaifuta ishara ya usiku na tukaifanya ishara ya mchana ya kuonea ili mtafute fadhla itokayo kwa Mwenyezi Mungu.” (17:12)

Wanasema: Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto! Ametakata na hayo! Yeye ni mkwasi. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Nyinyi hamna dalili kwa hayo. Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua?

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.1 (2:117). Huko tumezungumzia utatu (mungu baba, mungu mwana na roho mtakatifu).

Sema: Hakika wale ambao wanamzulia Mwenyezi Mungu uwongo hawatafaulu katika Akhera ambayo ni bora na yenye kubaki kulinganisha na maisha yetu haya.

Adhabu yao na maangamizi yao yatakuwa makubwa, ikiwa uzushi wao ni katika dhati yake Mwenyezi Mungu na sifa Zake na kumnasibishia washirika mke na mtoto

Ni starehe katika dunia.

Yaani neema waliyonayo washirikina ni starehe duni, hata kama mali yao ni nyingi na wakawa na jaha kubwa, kwa sababu yote hayo ni ya muda mfupi tena yanachanganyika na matatizo. Nayo si lolote yakilinganishwa na neema za Akhera.

Kisha marejeo ni kwetu tena tutawaonjesha adhabu kali, kwa sababu walikuwa wakikufuru Mungu na neema zake na kumkadhibisha Mtume wake.

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ نُوحٍ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ إِنْ كَانَ كَبُرَ عَلَيْكُمْ مَقَامِي وَتَذْكِيرِي بِآيَاتِ اللَّهِ فَعَلَى اللَّهِ تَوَكَّلْتُ فَأَجْمِعُوا أَمْرَكُمْ وَشُرَكَاءَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُنْ أَمْرُكُمْ عَلَيْكُمْ غُمَّةً ثُمَّ اقْضُوا إِلَيَّ وَلَا تُنْظِرُونِ {71}

Na wasomee habari za Nuh alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Ikiwa cheo changu na kukumbusha kwangu Ishara za Mwenyezi Mungu kunawachukiza, basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu, nanyi tengenezeni mambo yenu na washirika wenu, tena mambo yenu yasi- fichikane kwenu, kisha mlitekeleze kwangu wala msinipe nafasi.

فَإِنْ تَوَلَّيْتُمْ فَمَا سَأَلْتُكُمْ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّهِ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ {72}

Lakini mkikengeuka, basi mimi siwaombi ujira. Ujira wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa waislamu.

فَكَذَّبُوهُ فَنَجَّيْنَاهُ وَمَنْ مَعَهُ فِي الْفُلْكِ وَجَعَلْنَاهُمْ خَلَائِفَ وَأَغْرَقْنَا الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۖ فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُنْذَرِينَ {73}

Wakamkadhibisha, basi tukamwokoa na waliokuwa naye katika jahazi na tukawafanya ndio waliobakia. Tukawazamisha waliozikadhibisha Ishara zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa walioonywa.