read

Aya 71 – 73: Habari Za Nuh

Maana

Na wasomee habari za Nuh.

Anaambiwa Mtume Muhammad (s.a.w.) awasomee washirikina wa Makka.

Alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Ikiwa cheo changu na kukumbusha kwangu Ishara za Mwenyezi Mungu kunawachukiza, basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu, nanyi tengenezeni mambo yenu na washirika wenu, tena mambo yenu yasifichikane kwenu, kisha mlitekeleze kwangu wala msinipe nafasi.

Mtume Muhammad (s.a.w.) aliwaonya watu wake katika washirikina wa Makka akawatahadharisha na adhabu kali, lakini wakachukia mawaidha yake na maonyo yake. Bado aliendelea kuwalingania, wakachukizwa na cheo chake na wakajaribu kumuua.

Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha awasomee habari za Nuh ambaye aliwaonya watu wake, wakachukia maonyo yake na cheo chake, sawa na ilivyo kwake yeye Muhammad na washirikina wa Makka.

Muhtasari habari za Nuh alizowasomea washirikina wa Makka ni kwamba Nuh alishaindana na waliomkadhibisha na akawaambia kuwa mimi ninamtegemea Mwenyezi Mungu na nitawashinda; hata kama nyinyi ni wengi na wenye nguvu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ameniahidi kunipa ushindi naye havunji ahadi yake. Ama vitisho vyenu kwangu haviwezi kunizuwiya kuendelea na mwito wa Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo lililobaki kwenu ni kupanga njama kwa kadiri mtakavyoweza, muwakusanye wale wasiokuwa Mwenyezi Mungu, uonyesheni uadui mnavyotaka, endeleeni kuniudhi na yafanyeni hayo.

Lakini mkikengeuka, basi mimi siwaombi ujira.

Yaani kama mtapinga mwito wangu, basi mimi sijali upinzani wenu, kwa sababu hakuna manufaa yoyote nitakayoyakosa wala madhara nitakayopata.

Ujira wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu sio kwenu nyinyi, kwani hakika mimi ninamfanyia yeye sio nyinyi.

Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa waislamu.”

Mimi nimetii na kutekeleza ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa njia zake. Baada ya hapo nishauri yenu mkisilimu au mkikufuru.

Wakamkadhibisha, basi tukamwokoa na waliokuwa naye katika jahazi na tukawafanya ndio waliobakia. Tukawazamisha waliozikadhibisha Ishara zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa walioonywa.

Hivyo ndivyo unavyokuwa mwisho wa wanaopinga. Wanaangamia na Waumini wanaokoka na kuchukua mahali pa wanaokadhibisha walioangamia. Basi anagalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walioonywa. Anaambiwa Mtume Muhammad (s.a.w.) awaonye washirikina wa Makka yasije yakawapata yaliyowapata watu wa Nuh. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (7:72).

ثُمَّ بَعَثْنَا مِنْ بَعْدِهِ رُسُلًا إِلَىٰ قَوْمِهِمْ فَجَاءُوهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا بِمَا كَذَّبُوا بِهِ مِنْ قَبْلُ ۚ كَذَٰلِكَ نَطْبَعُ عَلَىٰ قُلُوبِ الْمُعْتَدِينَ {74}

Kisha baada yake tukatuma Mitume kwa watu wao. Nao wakawajia kwa Ishara zilizo wazi. Lakini hawakuwa ni wenye kuamini waliyokuwa wameyakadhibisha kabla. Hivyo ndivyo tunapopiga muhuri juu ya nyoyo za wapetukao mipaka.

ثُمَّ بَعَثْنَا مِنْ بَعْدِهِمْ مُوسَىٰ وَهَارُونَ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ بِآيَاتِنَا فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُجْرِمِينَ {75}

Kisha tukapeleka baada ya hao Musa na Harun kwa Firauni na waheshimiwa wake kwa ishara zetu. Wakafanya kiburi nao walikuwa watu wenye makosa.

فَلَمَّا جَاءَهُمُ الْحَقُّ مِنْ عِنْدِنَا قَالُوا إِنَّ هَٰذَا لَسِحْرٌ مُبِينٌ {76}

Basi ilipowafikia haki kutoka kwetu walisema: Hakika huu ni uchawi ulio wazi.

قَالَ مُوسَىٰ أَتَقُولُونَ لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَكُمْ ۖ أَسِحْرٌ هَٰذَا وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُونَ {77}

Musa akasema: Mnasema juu ya haki ilipowafikia, je huu ni uchawi? na wachawi hawafanikiwi!

قَالُوا أَجِئْتَنَا لِتَلْفِتَنَا عَمَّا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا وَتَكُونَ لَكُمَا الْكِبْرِيَاءُ فِي الْأَرْضِ وَمَا نَحْنُ لَكُمَا بِمُؤْمِنِينَ {78}

Wakasema: Je, umetujia ili utuondoe katika yale tuliyowakuta nayo baba zetu. Ili ukubwa uwe wenu nyinyi wawili katika nchi, na sisi hatuwaamini nyinyi.

وَقَالَ فِرْعَوْنُ ائْتُونِي بِكُلِّ سَاحِرٍ عَلِيمٍ {79}

Akasema Firauni: Nileteeni kila mchawi mjuzi.

فَلَمَّا جَاءَ السَّحَرَةُ قَالَ لَهُمْ مُوسَىٰ أَلْقُوا مَا أَنْتُمْ مُلْقُونَ {80}

Basi walipokuja wachawi, Musa akawaambia: “Tupeni mnavyotupa

فَلَمَّا أَلْقَوْا قَالَ مُوسَىٰ مَا جِئْتُمْ بِهِ السِّحْرُ ۖ إِنَّ اللَّهَ سَيُبْطِلُهُ ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا يُصْلِحُ عَمَلَ الْمُفْسِدِينَ {81}

Walipotupa, Musa akasema: Mlioleta ni uchawi, hakika Mwenyezi Mungu ataubatilisha. Hakika Mwenyezi Mungu hafanikishi vitendo vya wafisadi.

وَيُحِقُّ اللَّهُ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ {82}

Na Mwenyezi Mungu anaihakikisha haki kwa maneno yake, ingawa watachukia wenye makosa.