read

Aya 74 – 82: Kisha Tukawapelekea Mitume Baada Yake

Maana

Kisha baada yake tukatuma Mitume kwa watu wao. Nao wakawajia kwa Ishara zilizowazi. Lakini hawakuwa ni wenye kuamini waliyokuwa wameyakadhibisha kabla.

Yaani baada ya Nuh tulipeleka Mitume kwa watu wao, kama Ibrahim, Hud, Swaleh na wenginio, wakiwa na dalili na miujiza, lakini miujiza hii haikuwatoa kwenye ushirikina, kuwageuza kwenye imani ya umoja wa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Wao waliyakadhibisha hayo kabla kuwajia Mitume na hoja zilizo wazi, kwa hivyo waliendelea na kukadhibisha kwao huku hata baada ya kuwajia Mitume na kuwaonya.Kwa maneno mengine ni kuwa hawakunufaika na elimu ya Mitume na mwongozo wao.

Uongofu Na Upotevu

Hivyo ndivyo tunapopiga muhuri juu ya nyoyo za wapetukao mipaka.

Unaweza kuuliza, ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyepiga muhuri juu ya nyoyo zao, basi vipi atawaadhibu?

Jibu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaka uongofu uwe na njia yake maalum ambayo ni kufuata Mitume yake. Na upotevu nao uwe na njia yake ambayo ni kufuata matamanio. Kwa hiyo mwenye kufuata njia ya Mitume atafikia kwenye uongofu kwa vyovyote vile, na mwenye kufuata matamanio atafikia kwenye upotevu, sawa na alivyojaalia Mwenyezi Mungu kwamba mwenye kujitupa kutoka juu atakufa na mwenye kujitupa baharini akiwa hajui kuogelea atakufa maji tu.

Kwa kufangamanisha njia hizo mbili na matakwa ya Mwenyezi Mungu ndio ikawa Mwenyezi Mungu ndiye aliyepiga muhuri hizo njia mbili. Yamekwisha elezwa maelezo hayo mara nyingi. Kwa ibara mbali mbali.

Kisha tunapeleka baada ya hao Musa na Harun kwa Firauni na waheshimiwa wake kwa Ishara zetu.

Yaani baada ya Mitume waliokuja baada ya Nuh, tulimtuma Musa na Harun na miujiza, kama vile fimbo kugueka nyoka na mkono kuwa mweupe.

Kusema kwake Mwenyezi Mungu ‘na tukawapelekea’ inafahamisha wazi kuwa Harun ni Mtume sawa na nduguye Musa. Inasemekana kuwa Harun ni mkubwa wa Musa kwa miaka mitatu.

Wakafanya kiburi kukubali haki nao walikuwa watu wenye makosa.

Kila anayepinga kukubali haki basi ni mwenye makosa.

Basi ilipowafikia haki kutoka kwetu ambayo ni miujiza aliyoidhihirisha Mwenyezi Mungu mikononi mwa Musa (a.s.), walisema:

Hakika huu ni uchawi ulio wazi.

Kama hivyo walisema washirikina wa Kiquraish kuhusu Mtume Muhammad (s.a.w.) alipowajia na Qur’ani na muujiza wake. Ni muhali kabisa kupona muongozaji na uzushi wa wafisadi.
Na uzushi wenyewe unakwenda na wakati. Hapo mwanzo watu walikuwa wakiamini mchawi, kwa hiyo kiongozi mwema alikuwa akiitwa mchawi, ama leo ambapo hakuna imani ya uchawi wanamwita ni mvurugaji.

Musa akasema: Mnasema juu ya haki ilipowafikia, je huu ni uchawi?

Vipi iwe hivyo haki ina lengo la kuwaongoza watu ambapo uchawi unapo- tosha hali halisi na kuwapoteza watu na wachawi hawafanikiwi! Je, anaweza kufanikiwa mwenye kiini macho.

Wakasema: Je, umetujia ili utuondoe katika yale tuliyowakuta nayo baba zetu.

Huu ni mchezo anaoucheza kila mwenye ufisadi ambao una maslahi kwake. Suala ni kuhofia maslahi tu, sio suala la mababa na masanamu. Dalili ya hilo ni kauli yao anayoisimulia Mwenyezi Mungu: Ili ukubwa uwe wenu nyinyi wawili katika nchi.

Hiyo ni kauli ya Firauni na wakuu wake wa nchi kumwambia Musa na ndugu yake Harun. Walikuwa na maana ya kuwa lengo ni kunyang’anywa ufalme wa Misr sio ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Ndipo wakasema: Na sisi hatuwamini nyinyi. Bali tutapigana kulinda manufaa yetu na vyeo vyetu.

Akasema Firauni: Nileteeni kila mchawi mjuzi, naye hajui matekeo ya hayo.

Basi walipokuja wachawi, Musa akawaambia: Tupeni mnavyotupa. Alisema hivi kwa kuwapuuza wao, uchawi wao na Firauni wao. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwaahidi ushindi.

Walipotupa, Musa akasema: Mlioleta ni uchawi, hakika Mwenyezi Mungu ataubatilisha.

Huo wenyewe ni batili tangu mwanzo, lakini Mwenyezi Mungu atadhihirisha ubatilifu wake kwa watu. Ama fimbo ya Musa haipatwi na ubatil- ifu kwa sababu ni haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hafanikishi vitendo vya wafisadi.

Na Mwenyezi Mungu anaihakikisha haki kwa maneno yake ambayo ni hoja mkataa. Ingawa watachukia wenye makosa, kwa sababu chuki yao haiwezi kusimamisha matakwa ya Mwenyezi Mungu.

فَمَا آمَنَ لِمُوسَىٰ إِلَّا ذُرِّيَّةٌ مِنْ قَوْمِهِ عَلَىٰ خَوْفٍ مِنْ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِمْ أَنْ يَفْتِنَهُمْ ۚ وَإِنَّ فِرْعَوْنَ لَعَالٍ فِي الْأَرْضِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الْمُسْرِفِينَ {83}

Basi hawakumwamini Musa, isipokuwa baadhi ya vijana katika watu wake, kwa sababu ya kumwogopa Firauni na wakubwa wao asiwatie msuko suko. Na hakika Firauni alikuwa jeuri katika nchi, na kwa hakika alikuwa miongoni mwa waliopita kiasi.

وَقَالَ مُوسَىٰ يَا قَوْمِ إِنْ كُنْتُمْ آمَنْتُمْ بِاللَّهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِنْ كُنْتُمْ مُسْلِمِينَ {84}

Na Musa akasema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye, ikiwa nyinyi ni waislamu.

فَقَالُوا عَلَى اللَّهِ تَوَكَّلْنَا رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا فِتْنَةً لِلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ {85}

Wakasema: Tumemtegemea Mwenyezi Mungu. Ewe Mola wetu! Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na watu madhalimu.

وَنَجِّنَا بِرَحْمَتِكَ مِنَ الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ {86}

Na utuokoe kwa rehema yako na watu makafiri.

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ وَأَخِيهِ أَنْ تَبَوَّآ لِقَوْمِكُمَا بِمِصْرَ بُيُوتًا وَاجْعَلُوا بُيُوتَكُمْ قِبْلَةً وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۗ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ {87}

Na tukampa wahyi Musa na Harun: watengezeeni watu wenu majumba Misr. Na mzifanye nyumba zenu zenye kuelekea upande mmoja. Na simamisheni swala Na wape bishara waumini.

وَقَالَ مُوسَىٰ رَبَّنَا إِنَّكَ آتَيْتَ فِرْعَوْنَ وَمَلَأَهُ زِينَةً وَأَمْوَالًا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا رَبَّنَا لِيُضِلُّوا عَنْ سَبِيلِكَ ۖ رَبَّنَا اطْمِسْ عَلَىٰ أَمْوَالِهِمْ وَاشْدُدْ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُوا حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ {88}

Na Musa akasema: Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali nyingi katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanawapoteza watu na njia yako. Mola wetu! Ziangamize mali zao. Na zitie shida nyoyo zao. Na hawataamini mpaka waione adhabu yenye kuumiza.

قَالَ قَدْ أُجِيبَتْ دَعْوَتُكُمَا فَاسْتَقِيمَا وَلَا تَتَّبِعَانِّ سَبِيلَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ {89}

Akasema Mwenyezi Mungu, maombi yenu yamekubaliwa. Basi muwe na msimamo wala msifuate njia ya wale wasiojua.