read

Aya 83 – 89: Hawakumuamini Musa

Maana

Basi hawakumwamini Musa, isipokuwa baadhi ya vijana katika watu wake, kwa sababu ya kumwogopa Firauni na wakubwa wao asiwatie msuko suko.

Baada ya Musa kutupa fimbo na Mwenyezi Mungu kudhihirisha haki mikononi mwake, waliamini wachawi na watu wengi. Lakini kabla ya tukio la fimbo, walioamini ni vijana tu, katika Waisrael. Kwa sababu vijana walikuwa na wanaendelea kuwa ni wenye hamasa kwa kila jipya.

Lakini walimwamini Musa huku wakimhofia Firauni na pia wakubwa wa Waisrael, wasiwatie msuko suko kwa kuwaadhibu ili waikatae dini yao. Baadhi ya wanaotafuta maslahi katika Mayahudi walikuwa wakila njama na Firauni dhidi ya watu wao; kama ilivyo watu wa dini kila wakati na kila mahali.

Na hakika Firauni alikuwa jeuri katika nchi, na kwa hakika alikuwa miongoni mwa walipita kiasi katika na utaghuti wake.

Na Musa akasema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye, ikiwa nyinyi ni waislamu.

Musa hakuwa na chochote isipokuwa haki, na Firauni alikuwa na kila kitu, isipokuwa haki. Alikuwa akimkandamiza na kumtesa kila anayemwamini Musa. Musa akawa anawaambia watu wake, mimi sina nguvu wala nyinyi hamna nguvu za kumzuwiya Firauni na dhulma yake, isipokuwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, na vilevile kutegemea ahadi yake kwamba mwisho ni wa wenye kumcha Mwenyezi Mungu, kwa hiyo tegemeeni mambo yenu kwake Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamtii yeye.

Aliwatajia sifa tatu: Imani ambayo ni kusadikisha moyoni. Ya pili ni Uislam ambao makusudio yake hapo ni kufuata na kusalim amri kwa Mwenyezi Mungu, ya tatu ni kumtegemea Mwenyezi Mungu, nako ni kufanya Ikhlasi na kutegemeza mambo yote kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Mwenye kukusanya sifa hizi atakuwa pamoja na Mwenyezi Mungu.

Wakasema: Tumemtegemea Mwenyezi Mungu, na mambo yote tumemwachia yeye. Ndiye anayejua hali yetu na maslahi yetu, na yeye ni mweza juu ya kila jambo.

Ewe Mola wetu! Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na watu madhalimu.
Makusudio ya madhalimu hapa ni makafiri ambao ni Firauni na watu wake. Na misukosuko ni adhabu, kwa maana ya kuwa, usitujaalie ni mahali pa adhabu yao.

Na utuokoe kwa rehma yako na watu makafiri.

Makafiri hapa ni hao madhalimu ambao ni Firauni na watu wake ambao waliwakandamiza Waisrael. Makusudio ya kuokoka hapa ni kuokoka na dhulma yao na ukandamizaji wao. Kwa hiyo Aya hii ni tafsir ya Aya iliyo kabla yake.

Na tukampa wahyi Musa na Harun: watengezeeni watu wenu majumba Misr.

Yaani msiondoke hapo Misr na mfanye maskani kwa ajili ya Waisrael watakapokimbilia na kujilinda.

Na mzifanye nyumba zenu zenye kuelekea upande mmoja.

Yaani nyote mkae kwenye mtaa mmoja.

Imesemekana kuwa maana yake ni ‘mzifanye nyumba zenu ni mwahala mwa ibada,’ lakini tafsir ya kwanza ina nguvu kuliko kuwa majumba yawe miskiti kwa sababu majumba sio miskiti, miskiti ni ya ibada na majumba ni ya kukaa.

Na simamisheni Swala, kwa sababu ndiyo mambo ya Ikhlas na inaziku- sanya nyoyo kwenye hisiya ya umoja.

Na wape bishara waumini ya kuokoka na Firauni na wakubwa wake wa nchi katika dunia na kupata Pepo akhera.

Maneno yameelekezwa kwa Musa, kwa sababu yeye ndiye asili ya ujumbe, na kwa Harun kwa sababu yeye ni mfuasi wake.

Na Musa akasema: “Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali nyingi katika maisha ya dunia.

Aya hii ilishuka wakati ambao watu hawakuwa wakijua chochote kuhusu yaliyomo katika makaburi ya mafir’aun. Kisha wachimbaji wagunduzi wakagundua mali na vipambo vilivyoelezwa na Qur’ani. Huu ni ushahidi usiokuwa na shaka yeyote kwamba Qur’ani ni wahyi utokao kwa anayejua ghaibu.

Hivyo wanawapoteza watu na njia yako.

Yaani natija ya kuneemeshwa kwao na Mwenyezi Mungu kwa vipambo na mali, ni kumwasi badala ya kumtii.

Mola wetu! Ziangamize mali zao.

Mtu anaweza kudhani kuwa katika dua, Nabii Musa alimtaka Mwenyezi Mungu kuzuwiya utajiri wa wapotevu, ili wasizidi upotevu, lakini lililokatazwa ni ufisadi ambao ameukataza Mwenyezi Mungu. Tumelifafanua hilo katika Juz. 6 (5:66) kifungu cha ‘riziki na ufisadi.’

Na zitie shida nyoyo zao.

Imesemekana kuwa makusudio ni kuzifunga nyoyo zao wabaki katika miji yao ili waone kwa macho maangamizi ya mali zao. Pia ikasemekana ni kuzifunika nyoyo. Lakini tuonavyo sisi ni kuwa makusudio ni shida. Yaani Musa (a.s.) alimwomba Mwenyezi Mungu kuleta shida katika nyoyo zao.

Tafsiri hii inanasibiana na ombi lake Musa (a.s.) la kuangamizwa mali zao.

Na hawataamini mpaka waione adhabu yenye kuumiza.”
Jumla hii inaungana na ‘wawapoteze waja wako’. Yaani mwisho wa neema ya Mwenyezi Mungu kwa Firauni ni kuwapoteza watu na kutoamini mpaka waione adhabu, wakati ambao haitafaa imani. Hapana mwenye shaka kwamba Musa (a.s.) hakuomba haya yote ila baada ya kukata tamaa na kuongoka kwao.

Akasema Mwenyezi Mungu, maombi yenu yamekubaliwa. Yaani mambo ya kuangamizwa mali ya Firauni na wakubwa wake wa nchi na shida na masaibu kwenye nyoyo zao.

Basi muwe na msimamo katika njia hiyo ya jihad ya kuilingania haki. wala msifuate njia ya wale wasiojua ukubwa wa Mwenyezi Mungu na hekima yake.

Imefaa hapa kukatazwa ambaye hafanyi dhambi (maasum). Kwa sababu makatazo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu si kwa mwingine. Ni kawaida aliye mkubwa kumwamuru aliye chini yake kwa namna yoyote alivyo.

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنْتُ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ {90}

Na tukawavusha bahari wana wa Israel na Firauni na askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui mpaka kulipomfikia kufa maji, akasema: Nimeamini kwamba hakuna Mola isipokuwa yule wanayemuamini wana wa Israel nami ni miongoni mwa waislam (walionyenyekea).

آلْآنَ وَقَدْ عَصَيْتَ قَبْلُ وَكُنْتَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ {91}

Je, sasa! Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa wafisadi.

فَالْيَوْمَ نُنَجِّيكَ بِبَدَنِكَ لِتَكُونَ لِمَنْ خَلْفَكَ آيَةً ۚ وَإِنَّ كَثِيرًا مِنَ النَّاسِ عَنْ آيَاتِنَا لَغَافِلُونَ {92}

Basi leo tutakuokoa kwa mwili wako ili uwe ishara kwa ajili wa nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Ishara zetu.

وَلَقَدْ بَوَّأْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ مُبَوَّأَ صِدْقٍ وَرَزَقْنَاهُمْ مِنَ الطَّيِّبَاتِ فَمَا اخْتَلَفُوا حَتَّىٰ جَاءَهُمُ الْعِلْمُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ {93}

Nao hawakuhitalifiana mpaka ilipowafikia elimu. Hakika Mola wako atahukumu baina yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakihitalifiana.