read

Aya 90 – 93: Na Tukavusha Bahari Waisrael

Maana

Na tukawavusha bahari wana wa Israel na Firauni na askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui.

Umetangulia mfano wake katika Juz.1 (2:50) na Juz.9 (7: 136).

Mwisho Wa Utwaghuti

Mpaka kulipomfikia kufa maji, akasema nimeamini kwamba hakuna Mola isipokuwa yule wanayemuamini wana wa Israel nami ni miongoni mwa waislam (walionyenyekea).

Jana alikuwa Firauni akisema: Mimi ndiye Mola wenu mkubwa ,na leo anakana. Hali zote mbili hazimfai, si ile ya kwanza wala hii ya sasa. Mlango wa twaa ulipokuwa wazi yeye aliasi, na sasa hakuna nafasi tena ya utiifu wala uasi.

Hivi ndivyo alivyo mtu duni, hujifanya mkubwa wakati wa neema na kujifanya mdogo wakati wa dhiki. Historia huwa inajirudia; yaani desturi ya Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake ambayo ameisharia kwa kusisitiza pale aliposema:

فَلَنْ تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّهِ تَبْدِيلًا ۖ وَلَنْ تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّهِ تَحْوِيلًا {43}

“Basi hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu, wala huta- pata mageuko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.” (35:43).

Israil ya leo, inayokwenda kwa msaada wa ukoloni, inakwenda sawa na desturi ya Firauni hasa.

Firauni alikuwa akiwachinja watoto wa kiume wa Israel na kuwacha watoto wa kike. Leo Israel inafanya hivyo hivyo kwa wapalestina tena zaidi kuliko Firauni.

Firauni alisema:

يَا قَوْمِ أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِنْ تَحْتِي{51}

“Enyi watu wangu, je, ufalme wa Misr si ni wangu na hii mito ipitayo chini yangu?” (43:51).

Israel nayo inasema: Je, Palestina si ni yetu pamoja na mali zake zote, ikiwa ni pamoja na milima ya Golan na ukanda wa Gaza. Firauni alisema:

فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ {24}

“Mimi ndiye Mola wenu mkuu.” (79:24).

Israel na wanaowasaidia wanasema hatuwezi kushindwa sisi

Hazikupita siku nyingi ila ilianza kudhihiri desturi ya Mwenyezi Mungu. Ambapo Elat iliangamia na kuharibiwa vituo vya mabomu na wanaojitoa mhanga, kumemlazimisha Dayan kusema: “Ni lazima Mayahudi wajiandae kupanua uwanja wa makaburi yao.”

Na atasema tu, kama sio leo ni kesho: Nimemwamini yule anayeaminiwa na Waarabu na Waislam; sawa na alivyosema Firauni. Kwa sababu yeye anafuata nyayo zake, basi mwisho wake utakuwa sawa na Firauni tu. Mtu anaweza kusema kuwa vita vya Israael vimekuwa virefu na vyenye kuumiza

Tunaweza kujibu kuwa ni kweli, lakini ushindi wa mwisho ni wa wenye haki, hata kama muda utarefuka kwa kiasi gani. Historia ya zamani na ya karibuni ni shahidi wa hakika hii, kuanzia kwa Firauni na Hamana hadi kwa Hitler na Mussolini.

Je, sasa!

Baada ya kukupata yaliyokupata ndio unasema nimeamini?

Na hali uliasi kabla yake ulipokuwa na hiyari ya kutubia na kurudi kwenye haki, lakini ukafanya dhulma na ukawa miongoni mwa wafisadi.

Kwa hiyo onja malipo ya amali yako kwa kufa maji, na kuangamia.

Basi leo tutakuokoa kwa mwili wako sio kwa roho yako; na mwili wako na tutautupa nchi kavu ili auone yule aliyekuwa akikutukuza.

Ili uwe ishara kwa ajili wa nyuma yako apate mawaidha yule atakayeiweka nafsi yake kwenye ufisadi. Lakini wapi! Ibra ni nyingi lakini mazingatio ni machache, ndio Mwenyezi Mungu akasema: Na hakika watu wengi wameghafilika na ishara zetu.

Nao hawakuhitalifiana mpaka ilipowafikia elimu.

Yaani baada ya kuangamia Firauni, tuliwapa makazi mazuri na ardhi yenye rutuba.

Wafasiri wametofautiana kuhusu mji waliokuwa. wengine wamesema ni Palestina na wengine wakasema ni Misr. Kauli ya Misr ndiyo yenye nguvu kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu. “Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem, na mahazina na mahali pazuri. Kama hivyo, na tukawarithisha hayo wana wa Israel.” (26: 57-59).

Aya hii inaonyesha wazi kuwa Mwenyezi Mungu aliwakalisha wana wa Israel nyumba ya Firauni na wakubwa wake.

Nao hawakuhitalifiana mpaka ilipowafikia elimu.

Makusudio ya elimu hapa nia Tawrat, kama ilivyo teremshwa kwa Musa (a.s.). Ndani yake mlikuwa na habari ya Mtume Muhammad (s.a.w.). Wana wa Israel walikuwa wamoja katika ukafiri na upotevu wao, kabla ya kuteremshwa Tawrat.

Baada ya kuwajia Tawrat wakatofautiana wakati wa Musa na baadae, wengine waliasi zaidi, wakaabudu ndama na wakamwambia Musa tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi, na nenda wewe na Mola wako na mengineyo yaliyosajiliwa na Qur’ani.

Hakika Mola wako atahukumu baina yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakihitalifiana.

Ambapo siku hiyo hakutakuwa na uwongo wala riya au kitu chochote, isipokuwa haki itakayowadhihrikia wote wazi wazi.

فَإِنْ كُنْتَ فِي شَكٍّ مِمَّا أَنْزَلْنَا إِلَيْكَ فَاسْأَلِ الَّذِينَ يَقْرَءُونَ الْكِتَابَ مِنْ قَبْلِكَ ۚ لَقَدْ جَاءَكَ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكَ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ {94}

Ukiwa na shaka juu ya tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao Kitabu kabla yako. Haki imekwishafikia kutoka kwa Mola wako, kwa hivyo kabisa usiwe miongoni mwa wafanyao shaka.

وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّهِ فَتَكُونَ مِنَ الْخَاسِرِينَ {95}

Na kabisa usiwe miongoni mwa wanaokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, usije ukawa miongoni mwa wenye hasara.

إِنَّ الَّذِينَ حَقَّتْ عَلَيْهِمْ كَلِمَتُ رَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ {96}

Hakika wale ambao neno la Mola wako limekwishawathibitikia hawataamini.

وَلَوْ جَاءَتْهُمْ كُلُّ آيَةٍ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ {97}

Ijapokuwa itawajia Ishara, mpaka waione adhabu iumizayo.