read

Aya 94 –97: Ikiwa Una Shaka

Maana

Ukiwa na shaka juu ya tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao kitabu kabla yako.

Makusudioya wale wasomao Kitabu ni maulama wa Injil na Tawrat na kinachoulizwa ni kisa cha Musa na Mitume wengine kulingana na Qur’ani. Hiyo ni kwa kuangalia mfumo wa maneno.
Kwa sababu Aya zilishuka kuhusu kisa cha Musa na Firauni. Unaweza kuuliza, kuna wajihi gani katika kauli yake Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake.“Ukiwa na Shaka” pamoja na kujua kuwa Mtume hana shaka katika hilo, vipi iwe hivyo na hali yeye amevumilia adha nyingi katika kufikisha ujumbe wake kiasi ambacho hakuwahi kuna nacho Mtume mwingine au kiongozi yoyote.

Jibu: wajihi ni kumwambia Mtume Muhammad (s.a.w.) yule anayetia shaka yale yaliyotajwa na Qur’ani kuhusu kisa cha Musa na Mitume wengine, aulize Ulamaa wa watu wa Kitab wasio na upendeleo. Kwani hilo ni lenye kuthibiti katika Tawrat na Injil kama ilivyoeloezwa katika Qur’ani.

Haki imekwishafikia kutoka kwa Mola wako, kwa hivyo kabisa usiwe miongoni mwa wafanyao shaka. Na kabisa usiwe miongoni mwa wanaokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, usije ukawa miongoni mwa wenye hasara.

Yaani fikisha ujumbe ewe Muhammad kwa yule mwenye kutia shaka au kuikanusha haki iliyoteremshwa kwako, basi yeye ni miongoni mwa wenye kuadhibiwa siku ya Kiyama, hali ya kupata hasara.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameyatolea ibara makatazo haya kwa kumkataza Mtume kutokana na shaka na uongo, ili Mtume Muhammad (s.a.w.) aseme kwa watu: Mimi ni mtu mfano wenu na ni mmoja miongoni mwenu, kama nitatia shaka au kukanusha, basi nitahisabiwa na nitaadhibiwa; kama vile mtu yeyote yule atakayetia shaka au kukadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu.

Mfumo huu ni fasaha na wenye kufaulu zaidi katika kuilingania haki ambayo mbele yake inakuwa sawa kwa watu wote

Hakika wale ambao neno la Mola wako limekwishawathibitikia hawataamini, Ijapokuwa itawajia Ishara, mpaka waione adhabu iumizayo.

Makusudio ya neno la Mola wako hapa ni adhabu; yaani hakika wale ambao Mwenyezi Mungu atawaadhibu ni wale wasioiamini haki kwa hali yoyote hata kama ataletewa hoja elfu; isipokuwa kama ataiona adhabu. Na ilivyo ni kwamba imani ya namna hii haifai kitu kwa sababu ni sawa na imani ya Firauni wakati alipoangamia majini; kama iliyoelezwa hivi punde katika kufasiri Aya 90 ya Sura hii.

فَلَوْلَا كَانَتْ قَرْيَةٌ آمَنَتْ فَنَفَعَهَا إِيمَانُهَا إِلَّا قَوْمَ يُونُسَ لَمَّا آمَنُوا كَشَفْنَا عَنْهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَتَّعْنَاهُمْ إِلَىٰ حِينٍ {98}

Kwanini usiweko mji ulioamini na imani yake ikawafaa, isipokuwa kaumu ya Yunus? Walipoamini tuliwaondolea adhabu ya hizaya katika maisha ya dunia na tukawastarehesha kwa muda.

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَآمَنَ مَنْ فِي الْأَرْضِ كُلُّهُمْ جَمِيعًا ۚ أَفَأَنْتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ {99}

Lau angelitaka Mola wako, wangeliamini wote waliomo ardhini. Basi je wewe utawalazimisha watu wawe Waumini?

وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَنْ تُؤْمِنَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّهِ ۚ وَيَجْعَلُ الرِّجْسَ عَلَى الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ {100}

Na hakuna nafsi inayoweza kuamini isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na hujaalia uchafu kwa wale ambao hawatumii akili.