read

Aya 98-100: Kaumu Ya Yunus

Kisa

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemtaja Yunus kuwa ni katika Mitume na katika watu wema. Vile vile amemwita kwa jina sahiba wa samaki. Pia akamwita mwenye kughadhibika. Kwa sababu aliwalingania watu wake kwenye imani, lakini hawakumwitikia ndipo akawaombea maangamizo na akawaondokea kwa kukata tamaa na imani yao.

Katika Sura Al-Qalam Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake Muhammad (s.a.w.), avumilie na asifanye haraka ya kuwaombea adhabu watu wake, kama alivyofanya Yunus.

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تَكُنْ كَصَاحِبِ الْحُوتِ إِذْ نَادَىٰ وَهُوَ مَكْظُومٌ {48}

“Basi subiri hukumu ya Mola wako, wala usiwe kama sahiba wa samaki, aliponadi na hali amezongwa.” (68:48).

Watu wa Yunus walikuwa kiasi cha laki moja (100,000). Mwenyezi Mungu anasema:

وَأَرْسَلْنَاهُ إِلَىٰ مِائَةِ أَلْفٍ أَوْ يَزِيدُونَ {147}

“Na tulimtua kwa watu elfu mia moja au zaidi.” (37:147).

Wapokezi na wafasiri wanasema kuwa watu wa Yunus walikuwa wakikaa katika ardhi ya Mousel, na kwamba wao walikuwa wakiabudu masanamu. Nabii Yunus (a.s.) akawakataza kufru hiyo na kuwaamrisha Tawhid, lakini wakang’ang’ania ushirikina wao; kama ilivyokuwa kwa watu wa Mitume wengine.

Baada ya kuondoka Yunus zikaanza dalili za adhabu kutoka mbinguni, basi wakaanza kutubia kwa Mwenyezi Mungu na wakamuomba kwa ikhlasi kuwa awaondolee adhabu. Akafanya hivyo Mwenyezi Mungu akawabakisha mpaka muda wao. Hayo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Kwanini usiweko mji ulioamini na imani yake ikawafaa, isipokuwa kaumu ya Yunus? Walipoamini tuliwaondolea adhabu ya hizaya katika maisha ya dunia na tukawastarehesha kwa muda.

Wafasiri wanasema kuwa watu wa Yunus walivaa magwanda wakatoka jangwani wakiwa pamoja na wanawake, watoto na wanyama. wakatenganishasha baina ya kila mama na mwanawe awe mtu au mnyama. Wakatoa sauti wote, zikapanda sauti zao na ikachanganyika sauti ya watu wanyama. Basi Mwenyezi Mungu akawaondolea adhabu wakarudi majumbani mwao salama salmini.

Ama Yunus alisafiri akafika ufuo wa bahari akakuta kundi la watu kwenye jahazi. Akawaomba ajiunge nao wakakubali. Walipofikia katikati ya bahari, Mwenyezi Mungu aliwapelekea samaki mkubwa akazuia jahazi yao, wakajua kuwa anataka mmoja wao. Wakaafikiana kupiga kura ambayo ilimwangukia Yunus.

Kwa hiyo wakamtupa Yunus au alijitupa yeye mwenyewe baharini na akamezwa na samaki; kama ilivyoelezwa katika Qur’ani.

“Na hakika Yunus ni miongoni mwa Mitume. Alipokimbia katika jahazi iliyosheheni. Akaingia katika kupigiwa kura na akawa katika walioshindwa. Samaki akammeza hali ya kuwa mwenye kulaumiwa.” Yaani mwenye kujilaumu (37: 139-142).

Mwenyezi Mungu akampa ilham samaki kumuhifadhi tumboni1 mwake bila ya kumpa udhia wowote. Yunus akakimbilia kwa Mola wake na kumwomba akiwa tumboni mwa samaki, kama inavyoashiria Qur’ani.

فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَنْ لَا إِلَٰهَ إِلَّا أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنْتُ مِنَ الظَّالِمِينَ {87}

“Basi akaita katika giza kwamba hakuna Mola isipokuwa wewe tu, umetakasika, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu,” yaani mwenye kujidhulumu. (21:87)

Kisha samaki akamtema ufukweni baada ya kukaa tumboni kiasi alichota- ka Mwenyezi Mungu. Wafasiri wanasema Yunus alitoka tumboni kama kifaranga kisicho na manyoya, na Mwenyezi Mungu alimwoteshea mmea wa mung’unya kujifunika nao. Katika hilo Mwenyezi Mungu anasema:

فَلَوْلَا أَنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُسَبِّحِينَ {143}

لَلَبِثَ فِي بَطْنِهِ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ {144}

فَنَبَذْنَاهُ بِالْعَرَاءِ وَهُوَ سَقِيمٌ {145}

وَأَنْبَتْنَا عَلَيْهِ شَجَرَةً مِنْ يَقْطِينٍ {146}

“Lau angelikuwa si katika wanaomtakasa Mwenyezi Mungu angelikaa tumboni mpaka siku ya kufufuliwa. Lakini tulimtupa ufukweni patupu hali ya kuwa mgonjwa, na tukamwoteshea mmea wa mung’unya’ (37: 143- 146).

Baada ya hapo Yunus, alirudi kwa watu wake wakafurahi sana kwa kufika kwake naye akafurahi kwa imani yao.

Lau angelitaka Mola wako, wangeliamini wote waliomo ardhini.

Yaani lau angelitaka Mwenyezi Mungu kuwalazimisha watu imani au kuwaumba tangu mwanzo, wakiwa Waumini, basi duniani kusingelipatikana kafiri hata mmoja. Na angelifanya hivyo, basi kusingekuwa na thawabu wala adhabu na vitendo vya watu vingelikuwa kama matunda tu ya mti. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 7 (6:35). Na tumefafanua zaidi katika Juz. 3 (2:253)

Basi je wewe utawalazimisha watu wawe Waumini?

Yaani hekima ya Mwenyezi Mungu imetaka kwamba hiyari ya kufuata haki au kuipima, iwe mikono mwa watu, ili aweze kupambanuka mwovu na mwema. Na hakuna yeyote anayeweza kupinga matakwa ya Mwenyezi Mungu. Basi kwanini unahuzunika na kusikitika kutokana na ukafiri wao na kukosa kwao imani? Makusudio ni kuwa tahfifu hii anafanyiwa Mtume Mtukufu (s.a.w.).

Maana haya yamekarika kwenye Aya nyingi. Miongoni mwazo ni:

وَمَا أَنْتَ عَلَيْهِمْ بِجَبَّارٍ ۖ {45}

Wala wewe si mwenye kuwatawalia” (50:45)

Na hakuna nafsi inayoweza kuamini isipokuwa kwa idhi ya Mwenyezi Mungu.

Yaani kila hali ya mtu ina sababu, ikiwemo imani na njia ya kuangalia ishara za Mwenyezi Mungu kwa mtazamo safi. Mwenye kuzijua kwa uhakika wake na kwa njia zake, kwa vyovyote ataishia kwenye kuamini hukumu za Mwenyezi Mungu na anavyotaka.

Hapa ndio anakuwa Mwenyezi Mungu ametaka kuamini kwake, kwa sababu yeye ndiye aliyejaalia kuzingatiwa Ishara zake ndio sababu ya kuamini yeye.

Vilevile mwenye kuzipinga, kwa vyovyote ataishia kwenye ukafiri kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu yeye ndiye aliyejaalia kuzipinga Aya ndio sababu ya ukafiri. Lakini amejaalia hiyari mikononi mwa mtu mwenyewe katika kufuata mojawapo ya njia mbili.

Katika maana ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu.

قَدْ أَفْلَحَ مَنْ زَكَّاهَا {9}

وَقَدْ خَابَ مَنْ دَسَّاهَا {10}

“Hakika amefaulu mwenye kuitakasa na amepata hasara mwenye kuitweza.” (91:9-10).

Yaani kwa vyovyote kufaulu kunathibiti kwa mwenye kuisafisha nafsi yake kutokana na hawa na matamanio. Na kufeli kwa vyovyote ni kwa mwenye kuichafua nafsi yake kwa dhambi.

Na hujaalia uchafu kwa wale ambao hawatumii akili.

Makusudio ya uchafu hapa ni ukafiri kwa mkabala wa imani ambayo ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa kupinga Aya za Mwenyezi Mungu na kuacha kuzizingatia, lazima, kunapelekea ukafiri; kama ambavyo kuzinzingatia kunapelekea imani.

Hapo inatubainikia kuwa makusudio ya idhini ya Mwenyezi Mungu kwenye imani ni utambuzi wa dalili na hoja alizoziweka, ikiwa utambuzi wenywee ni msafi usiokuwa na misukumo ya malengo ya maslahi na matamanio ya nafsi.

قُلِ انْظُرُوا مَاذَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَنْ قَوْمٍ لَا يُؤْمِنُونَ {101}

Sema, tazameni ni yapi yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini! Na dalili na maonyo hayawafai watu wasioamini.

فَهَلْ يَنْتَظِرُونَ إِلَّا مِثْلَ أَيَّامِ الَّذِينَ خَلَوْا مِنْ قَبْلِهِمْ ۚ قُلْ فَانْتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُمْ مِنَ الْمُنْتَظِرِينَ {102}

Basi hawangojei isipokuwa siku za watu waliopita kabla yao. Sema, basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wenye kungojea.

ثُمَّ نُنَجِّي رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا ۚ كَذَٰلِكَ حَقًّا عَلَيْنَا نُنْجِ الْمُؤْمِنِينَ {103}

Kisha tunawaokoa Mitume wetu na wale walioamini, ndio kama hivyo inatustahiki kuwaokoa Waumini.

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنْ كُنْتُمْ فِي شَكٍّ مِنْ دِينِي فَلَا أَعْبُدُ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ وَلَٰكِنْ أَعْبُدُ اللَّهَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُمْ ۖ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ {104}

Sema, Enyi watu! Ikiwa mnayo shaka katika dini yangu, basi mimi siwaabudu wale mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, lakini ninamwabudu ambaye anawafisha, na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kuamini.

وَأَنْ أَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ {105}

Na kwamba elekeza uso wako kwenye dini safi, wala usiwe miongoni mwa washirikina.

وَلَا تَدْعُ مِنْ دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَنْفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِنْ فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِنَ الظَّالِمِينَ {106}

Wala usiwaombe wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawakunufaishi wala kukudhuru; kama ulifanya basi wewe utakuwa miongoni mwa madhalimu.
  • 1. Lau wangelitanabahi wale wanaowanasibisha wavumbuzi kwenye Qur’ani wangelisema kuwa samaki anaashiria nyambizi. Angalia Juz.1 (2:2) kifungu cha ‘Qur’ani na sayansi’