read

Aya 1 – 6: Imewakurubia Watu Hisabu Yao

Maana

Imewakurubia watu hisabu yao nao wamo katika mughafala wanapu- uza.

Makusudio ya hisabu hapa ni siku ya Kiyama, nayo iko karibu na kila mtu, kwa sababu itakuja tu, hata kama muda utakuwa mrefu. Maana yake yanafupishwa na kauli ya Imam Ali: “Usijisahau kwani wewe hujasahauliwa.” Na akasema tena: “Usighafilke kwani wewe hujasahauliwa.” Akasema tena: “Hatua fupi ilioje ya mtu aliye na siku moja tu ambayo hawezi kuizidisha, na mauti yaliyo na haraka yanamuandama mpaka aitoke”

Hawafikii dhikr mpya kutoka kwa Mola wao ila huisikiliza na huku wanaifanyia mchezo.

Wanaikabili haki kwa kuikadhibisha, nasaha za kejeli na hadhari za dharau. Zimeghafilika nyoyo zao na haki, hawajali kitu wala hawahisi majukumu ya kuulizwa hisabu na malipo; sawa na wanyama na wadudu.

Na wale waliodhulumu hunog’ona kwa siri: Ni nani huyu isipokuwa ni mtu tu kama nyinyi.

Washirikina walinong’onezana kuhusu aliyesilimu na kuongoka, kuwa huyo Muhammad, ni nani hata tumtii na kumfuata? Yeye si mtu tu kama watu wengine, anakula chakula na anatembea sokoni? Ama elimu na fadhila basi ni maneno bila maana na miujiza ni uchawi na kuvunga.

Mnauendea uchawi hali nanyi mnaona?

Mnauendea hapa, ina maana ya kukubali, na mnaona ni kwa maana ya mnajua. Si ajabu wao kuzikadhibisha Aya za Mwenyezi Mungu na dalili zake ambazo amekuja nazo Mtume mtukufu (s.a.w.). Kila mwenye kiburi hutafuta visingizio vya aina hii ikiwa hana hoja.

Alisema: Mola wangu anajua yasemwayo mbinguni na ardhini na Yeye ni mwenye kusikia, mwenye kujua.

Walimwambia Mtume (s.a.w.) kuwa yeye ni mchawi akawajibu kuwa Mwenyezi Mungu anajua ukweli wake na anajua kauli yao hii, kwa sababu hakifichiki kwake kitu chochote katika ardhi na katika mbingu. Atawahisabu na atawalipa vile mnavyostahiki.
Hakuna jawabu kwa anayeipinga haki isipokuwa kupelekwa kwenye mahakama ya uadilifu.

Lakina walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua, bali huyo ni mshairi.

Waliikataa wanamangamanga haki wakatafuta visingizio vya kutumia, wakabaki tu. Mwenye Majmaul-bayan anasema: “Hivi ndivyo anavyokuwa yule Mwenye kuhemewa. Anasema ni mchawi, mara ni mshairi, mara anaota. Hana moja analolishikilia. Huku ndio kujipinga kwa dhahiri.”

Basi atuletee ishara kama walivyotumwa wale wa mwanzo.

Washirkina walimwambia Muhammad (s.a.w.): Ukiwa wewe ni Mtume basi tuletee muujiza, kama vile ngamia wa Swaleh, fimbo ya Musa na miujiza mingineyo ya mitume waliopita. Ndio Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema:

Hawakuamini kabla yao watu wa mji tuliouangamiza.

Maana ya jawabu hili ni kuwa, ni kweli kwamba mitume waliotangulia walikuja na miujiza, kama vile ngamia na fimbo, lakini watu wao hawakuwaamini, bali walikataa na wakamakadhibisha, ingawaje wao wenyewe ndio walioitaka. Kwa ajili hiyo tukawaangamiza.

Kwa hiyo inatakiwa enyi washirikina muangalie natija inayofungamana na miujiza sio muujiza wenyewe. Kwa sababu itawatokea hivyo hivyo, ikiwa Mwenyezi Mungu atawakubalia mapendekezo yenu.

Je, wataamini hao.

Yaani wale waliokuwa kabla yao hawakuamini miujiza waliyoipendekeza, vile vile hawa hawataamini miujiza wanayoipendekeza. Natija itakuwa ni kuangamizwa, kama walivyoangamizwa wa kwanza; ambapo hekima yake Mwenyezi Mungu ilipitisha kuwa waangamizwe kwa miujiza waliyoitaka.

وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ إِلَّا رِجَالًا نُوحِي إِلَيْهِمْ ۖ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِنْ كُنْتُمْ لَا تَعْلَمُونَ {7}

Na hatukuwatuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi. Basi waulizeni wenye kumbukumbu, ikiwa nyinyi hamjui.

وَمَا جَعَلْنَاهُمْ جَسَدًا لَا يَأْكُلُونَ الطَّعَامَ وَمَا كَانُوا خَالِدِينَ {8}

Na hatukuwafanya miili isiyokula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.

ثُمَّ صَدَقْنَاهُمُ الْوَعْدَ فَأَنْجَيْنَاهُمْ وَمَنْ نَشَاءُ وَأَهْلَكْنَا الْمُسْرِفِينَ {9}

Kisha tukawatimizia miadi na tukawaokoa wao na tuliowataka na tukawaangamiza waliopita mipaka.

لَقَدْ أَنْزَلْنَا إِلَيْكُمْ كِتَابًا فِيهِ ذِكْرُكُمْ ۖ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {10}

Hakika tumewateremshia Kitabu, ndani yake mna ukumbusho wenu. Je, hamtii akili?

وَكَمْ قَصَمْنَا مِنْ قَرْيَةٍ كَانَتْ ظَالِمَةً وَأَنْشَأْنَا بَعْدَهَا قَوْمًا آخَرِينَ {11}

Na miji mingapi iliyokuwa ikidhulumu tumeiteketeza na tukawaumba baada yao watu wengine.

فَلَمَّا أَحَسُّوا بَأْسَنَا إِذَا هُمْ مِنْهَا يَرْكُضُونَ {12}

Basi walipohisi adhabu yetu mara wakaanza kukimbia.

لَا تَرْكُضُوا وَارْجِعُوا إِلَىٰ مَا أُتْرِفْتُمْ فِيهِ وَمَسَاكِنِكُمْ لَعَلَّكُمْ تُسْأَلُونَ {13}

Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu na maskani zenu mpate kusailiwa.

قَالُوا يَا وَيْلَنَا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ {14}

Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhalimu.

فَمَا زَالَتْ تِلْكَ دَعْوَاهُمْ حَتَّىٰ جَعَلْنَاهُمْ حَصِيدًا خَامِدِينَ {15}

Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya wamefyekwa wamezimika.