read

Aya 1 – 7: Ufufuo

Maana

Katika Aya hizi kuna kutahadharisha kuhusu siku ya Kiyama pamoja na kuashiria vitu na shida za siku hiyo. Vile vile kuwashutumu wale walioghafilika nacho; kisha kutoa dalili ya ufufuo.
Ufafanuzi ni kama ufuatavyo:

1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu. Hakika tetemeko la saa ni jambo kuu.

Makusudio ya saa ni siku ya Kiyama. Kimeitwa hivyo kwa sababu kila mtu atakifikia; kama anavyosema Mulla Sadra katika kitabu Al-Asfar.

Maana ya tetemeko la kiyama ni kuharibika ulimwengu ikiwa ni pamoa na ardhi yake na mbingu yake. Hizo zitachanganyika na pia bara na bahari na vizuizi vitaondoka. Miili itatoka makakburini kama picha isiyo na roho.

Siku mtakapoiona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshae na kila mwenye mimba ataiharibu mimba yake. Na utawaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.

Hiki ni kinaya cha vituko vya siku ya Kiyama na shida zake; ambapo hakutakuwa na mnyonyeshaji wala mwenye mimba sku hiyo. Yaani, lau angelikuwako mwenye kunyonyesha basi angelimsau mwanawe na mwenye mimba angelizaa. Na watu wote watagongana huku na huko kama walevi.

Mjadala Wakijinga Na Upotevu

2. Na miongoni mwa watu wako wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya elimu.

Mtu yeyote atakuwa ni mmoja wapo kati ya wawili: Ama atakuwa hajui au atakuwa ni mjuzi. Huyo mjuzi naye yuko katika hali mbili: Ama atakuwa ni mwenye insafu au atakuwa mpotevu. Mwenye insafu ni yule anayesema yale anayoyajua na kuyanyamazia asiyoyajua. Mwenyezi Mungu ameueleza wadhifa wa asiyejua kwa kusema:

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِنْ كُنْتُمْ لَا تَعْلَمُونَ {7}

“Basi waulizeni wenye kumbukumbu, ikiwa nyinyi hamjui.” (21:7).

Ikiwa atauepuka wadhifa huu, basi atakuwa amehusika na kauli ya Imam Ali (a.s.): “Yu mjinga, anatangatanga gizani bila ya mwongozo.”

Huu ndio ujinga alioukusudia Mwenyezi Mungu kwenye kauli yake hii na pia kauli itakayokuja kwenye Aya ya 8 ya Sura hii: “Na katika watu wapo wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilmu wala uongufu wala Kitabu chenye nuru.”

Hajui njia ya kumjua Mwenyezi Mungu, lakini anabishana kuhusu Mungu, huku akisema: lau Mwenyezi Mungu angelikuwako tungelimuona. Kwa mantiki haya, anataka kufasiri mada kwa isiyokuwa mada, kuona kwa macho kile kinachonekana kwa akili tu na kumgusa kwa mkono muumba wa mbingu na ardhi.

Huyu hana tofauti na yule anayetaka kufanya mtihani wa nadhariya ya ‘ushahidi ni wa mwenye kudai na kiapo ni kwa mwenye kukanusha’ kwenye kiwanda. Au kutaka kufanya mtihani wa kuendesha gari kutokana na hisia zake.

Wakati nikiandika maelezo haya nimekumbuka tulipokua Najaf tukisoma, kiasi cha miaka arobaini iliyopita. Siku moja tulipokuwa kwenye darasa tukisiliza mhadhara wa mwalimu, mmoja wa wanafunzi akamkatiza mwalimu na akatoa ushahidi usiokuwa na uhusiano wowote na maudhui kwa umbali wala karibu. Basi mwalimu akaachana naye akawaangalia wanafunzi wengine na akasema:

“Hapo zamani kulikuwa na mtu mmoja mwenye akili punguani, jina lake ni Bau. Siku moja alipita barabarani akaona watu wamekusanyika. Akauliza, kulikoni? Akaambiwa fulani ameanguka kutoka juu ya nyumba, amaevunjikavunjika viungo hatujui kama ataishi na watu wake hawana la kufanya.
Basi Bau akasema: “Mimi nina suluhisho, mfungeni kamba mumkaze sawasawa kisha avutwe mpaka juu ya nyumba kule alikotokea, atapona tu.” Watu walipomcheka, alitoa hoja kwamba mwaka jana fulani alianguka kisimani, wakamfunga kamba na wakamtoa, akasalimika.”

Mantiki haya hasa ndiyo ya yule anayekana kuweko Mungu kwa vile hamuoni. Ulimwengu huu na nidhamu yake anauona, lakini bado anadai kuwa haufahamishi kuwako aliyeutengeneza na kuuwekea nidhamu.

Sisi tunaamini ushahidi na majaribio, lakini tunaamini vilievile kuwa majaribio haya hayawezi kuwa kwenye kila kitu, bali yanakuwa kwenye baadhi ya vitu vya kimaada. Ama vitu vya kiroho na vya kibinadamu vina njia nyingine ya kujua.

Tunasema hivi tukiwa na uhakika kwamba hivi viwili vinakwenda pamoja vikikamilishana na kwamba mtu anahitajia maada. Misimamo kama vile haki na kheri haina budi iwe na athari inayoonekana, vinginevyo ingelikuwa ni matamshi tu yasiyokuwa na maana yoyote.

Lakini hii haimaanishi kuwa ndio njia ya maarifa peke yake; bali inatofautiana kwa kutofautiana vitu. Kwa hiyo ushahidi na majaribio ni sababu ya kujua vitu vya kimaada na akili ni sababu ya kujua vinginevyo visivyokuwa maada.

Tumezungumzia kuhusu maarifa na sababu zake katika Juz. 1(2:3-5)

Kwa ufupi ni kuwa mwenye kusema: Simwamini Mungu mpaka nimuone, amekiri yeye mwenyewe kwamba hataki kumwamini Mwenyezi Mungu, hata kama ataletewa dalili elfu na moja. Maana yake ni kuwa anakubali kuwa yeye ni mjinga mwenye kiburi.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu hawezi kuonekana kwa macho na kwamba njia ya kujua haikomei kwenye macho tu. Mwenyezi Mungu anamtaka binadamu afanye utafiti, uchunguzi, mjadala na mdahalo, lakini kielimu na kuchunga haki, sio kiujinga na kiupofu.

Na anamfuata kila shetani muasi.

Kila anayeweza kuvunga na kuficha hakika yake, basi huyo ni shetani. Shetani asi ni yule ambaye vitendo vyake na kauli zake zote zimejaa ufisadi. Shetani huyu akiingia kwenye akili ya mtu tu humuongoza kwenye upotevu na maangamizi. Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Ameandikiwa kwamba anayemtawalisha shetani, basi huyo hakika atampoteza na atamwongoza katika adhabu ya moto mkali.

Upotevu na adhabu ya moto hawezi kuepukana nayo yule mwenye kufuata wapotevu na wafisadi, ambao wanayapotoa maneno ya Mwenyezi Mungu, wakihalalisha na kuharamisha kwa hawa zao na matakwa yao.

3 Enyi watu ikiwa mna shaka ya kufufuliwa, basi kwa hakika tuliwaumba kutokana na udongo.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumhadharisha yule anayebishana kuhusu Mwenyezi Mungu bila ya elimu, sasa anataja dalili za ufufuo ambao mjinga anauifikiria kuwa hauwezekani.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amezileta dalili hizi kwa mifano yenye kuhisiwa, nayo ni kuwa: Hakika Mwenyezi Mungu amemuumba mtu kutokana na mchanga moja kwa moja, au kupitia kitu kingine.

Alimuumba Adam, baba wa watu, moja kwa moja kutokana na mchanga na akatuumba sisi wana wa Adam kupitia kitu kingine. Kila mmoja wenu anakuwa kutokana na manii na damu navyo vinatokana na chakula ambacho kinatokana na mchanga na maji. Kwa hiyo mchanga ndio msingi wa kupatikana mtu, kisha kutokana na tone la manii; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

أَلَمْ يَكُ نُطْفَةً مِنْ مَنِيٍّ يُمْنَىٰ {37}

“Je, hakuwa ni tone la manii lililoshushwa?” (75:37).

Kisha kutokana na pande la damu. Tone la manii linageuka kuwa kipande cha damu iliyoganda, kisha kutokana na pande la nyama. Pande la damu nalo linabadilika kuwa pande la nyama lenye umbo na lisilokuwa na umbo. Yaani baadhi yake imetimia umbo na sehemu haijatimia. Ili tuwabainishie uwezo wetu wa kufufua na mengineyo.

Na tunaliweka katika matumbo ya kizazi mpaka muda uliowekwa wa kuzaliwa mtoto.

Kisha tunawatoa hali ya kuwa mtoto mchanga kisha mfikie kukomaa kwenu. Kukomaa ni kukamilika mtu nguvu za kimwili na kiakili.

Na wapo miongoni mwenu wanaokufa kabla ya kukomaa au baada ya kukomaa kabla ya uzee na umri mbaya.

Na wapo miongoni mwenu wanorudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa hata asijue kitu baada ya kuwa anakijua.

Ni uzee na ukongwe, udhaifu wa kimwili, kiakili na kumbukumbu. Inapodhoofika akili matamanio yanachukua nafasi na kuzidi kufanya mambo ya kipuuzi.

Mabadiliko haya ya kukua kwa binadamu, kutoka hali duni hadi hali ya juu; kutoka mchanga hadi manii, kisha pande la damu, la nyama, utoto hadi kukomaa, yanafahamisha waziwazi kwamba binadamu ana nguvu na maandalizi yatakayompeleka kwenye ukamilifu na ubora, ikiwa hakutakuwa na vizuizi vya kuzuia kufikia lengo hili.

Na unaiona ardhi imekufa, lakini tunapoyateremsha maji juu yake, husisimka na kututumka na kumea kila aina ya mimea mizuri.

Maji yakishuka kwenye ardhi iliyokufa hutaharaki na kupumua kwa uhai, kisha inatoa aina kwa aina za mimea inayovutia macho na yenye ladha kwa walaji.

Hakuna mwenye shaka kwamba ardhi ni maandalizi ya kuukabili uhai, lakini mpaka kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu kila kitu kinaishia kwenye kauli yake ‘kuwa na kinakuwa’ Baadhi ya masufi wanasema: Makusudio ya ardhi iliyokufa ni ujinga, maji ni elimu na aina mbalimbali za mimea ni sifa za ukamilifu za Mwenyezi Mungu.

Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ni haki na kwamba hakika yeye ndiye Mwenye kuhuisha wafu na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu na kwamba saa itakuja hapana shaka kwa hilo na kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini.

Hayo ni ishara ya mambo yalivyo. Maana ya kuwa Mwenyezi Mungu ni haki ni kwamba hukumu na ufalme ni wake yeye peke yake bila ya kushirikiana na yeyote na kwamba hakuna kupatikana isipokuwa kutokana na yeye.

Hiyo ikiwa na maana kwamba yeye ndiye mwanzishaji na mrudishaji na ufufuo utakuwako tu kama ulivyokuwako uumbaji; bali huo uumbaji ni nyenzo na njia ya kufikia ufufuo ambao ndio lengo la malengo yote.

Kwa sababu mtu anarejea kwa muumba wake kuhisabiwa na kulipwa na pia hapo ndio pa kubakia, lakini kule kuumbwa kwa kwanza kuliisha. Kwisha ni nyenzo ya kubakia.

Hapa ndio tunakuta tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ {56}

“Na sikuumba majini na watu ila waniabudu. (51:56).

Yametangulia maelezo ya ufufuo katika Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz. 1 (2:28-29) kifungu cha ‘Ufufuo,’ Juz. 5 (4:85-87) kifungu cha ‘Njia mabalimbali za kuthibitisha marejeo (ufufuo) na Juz. 13 (13: 5-7) kifungu cha ‘Wanaoamini maada na maisha baada ya mauti.’

وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يُجَادِلُ فِي اللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُنِيرٍ {8}

Na katika watu wapo wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu wala uongufu wala Kitabu chenye nuru.

ثَانِيَ عِطْفِهِ لِيُضِلَّ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۖ لَهُ فِي الدُّنْيَا خِزْيٌ ۖ وَنُذِيقُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَذَابَ الْحَرِيقِ {9}

Anayegeuza shingo yake ili awapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya na siku ya Kiyama tutamuonjesha adhabu ya kuungua.

ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ يَدَاكَ وَأَنَّ اللَّهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِلْعَبِيدِ {10}

Hayo ni kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yako na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.

وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يَعْبُدُ اللَّهَ عَلَىٰ حَرْفٍ ۖ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ ۖ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انْقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ {11}

Na katika watu wapo wanaomwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni. Ikimfika kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amepata hasara ya dunia na Akhera; hiyo ndiyo hasara iliyo wazi.

يَدْعُو مِنْ دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَضُرُّهُ وَمَا لَا يَنْفَعُهُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الضَّلَالُ الْبَعِيدُ {12}

Anaomba, badala ya Mwenyezi Mungu, kile kisichomdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotelea mbali.

يَدْعُو لَمَنْ ضَرُّهُ أَقْرَبُ مِنْ نَفْعِهِ ۚ لَبِئْسَ الْمَوْلَىٰ وَلَبِئْسَ الْعَشِيرُ {13}

Anamuomba yule ambaye hakika dhara iko karibu zaidi kuliko nafuu yake. Hakika ni mlinzi mbaya na ni rafiki mbaya.

إِنَّ اللَّهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۚ إِنَّ اللَّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ {14}

Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema katika bustani zipitazo mito chini yake. Hakika Mwenyezi Mungu hufanya ayatakayo.