read

Aya 101 – 107: Ardhi Watarithi Waja Wangu Walio Wema

Maana

Hakika wale ambao umewatangulia wema kutoka kwetu, hao watatenganishwa na hayo.

Mwenyezi Mungu aliwaahidi wenye takua kuamiliana nao kwa wema. Miongoni mwa wema huo ni kuokoka na moto.

Hawatasikia mvumo wake.

Hii ni kusisitiza watakavyokuwa mbali nao.

Nao watudumu katika yale ambayo nafsi zao zinayatamani.
Watasalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu wakineemeshwa kwenye Pepo yake.

Hiyo fazaa kubwa haitawahuzunisha, sikwambii ndogo tena.

Kwani fazaa zina daraja, kuanzia machungu ya kukata roho, upweke wa kaburini, kisha kutoka makaburini kwa ajili ya hisabu hadi kuingia Jahannam.

Na Malaika watawapokea: Hii ndiyo siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.

Malaika watawapokea kwa takrima na kuwaambia kuwa Mwenyezi Mungu amewakusanya kwenye siku hii aliyowaahidi kwa ufalme wa daima na neema isiyokatika. Aya hizi tatu zinafupilizwa na neno:

هَلْ جَزَاءُ الْإِحْسَانِ إِلَّا الْإِحْسَانُ {60}

“Je, malipo ya hisani si ni hisani tu. (55:60)

Au neno:

لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ {26}

“Kwa wafanyao wema ni wema. Juz.11 (10:26).

Siku tutakapozikunja mbingu mkunjo wa karatasi za vitabu.

Makusudio ya vitabu hapa ni maandishi ya matamko yanayoayaandikwa kwenye karatasi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atazikunja sayari, siku ya Kiyama, pamoja na ukubwa na wingi wake; kama inavyokunjwa karatasi yenye maandishi; kiasi ambacho kila sayari itafanana na herufi au neno lilo kwenye karatasi.

Kama tulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika sisi ni wenye kufanya.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amefananisha ufufuo na kuumba kwa kwanza; kwamba, kama kulivyowezekana kwa kwanza, basi kwa pili pia kuunawezekana. Si muhali kwa Mwenyezi Mungu kutekeleza ahadi yake.

Hilo halimshindi Mwenyezi Mungu; kwani mwenye kuumba ulimwengu basi hawezi kushindwa kuurudisha tena baada ya kuharibika na kutawanyika:

وَهُوَ الَّذِي يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَهُوَ أَهْوَنُ عَلَيْهِ ۚ{27}

“Na Yeye ndiye anayeanzisha uumbaji, kisha ataurudisha. Na hilo ni jepesi zaidi kwake” (30:27).

Tena Mahdi Anayengojewa

Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya ukumbusho kuwa Ardhi watairithi waja wangu walio wema.

Zaburi ni kitabu cha Daud na ukumbusho ni vitabu vya mbinguni vilivyotangulia; kama vile vitabu vya Ibrahim na Musa. Maana yake ni kuwa utawala wa dunia, ingawaje hivi sasa uko mikononi mwa mataghuti waovu, lakini Mwenyezi Mungu atauhamisha uende kwa walio wema. Hilo halina budi. Hapo amani na uadilifu utaenea ardhini na watu wote wataneemeka na kheri za Ardhi na baraka zake.

Kuna Hadithi nyingi zenye maana ya Aya hii; miongoni mwazo ni ile aliy- oipokea Abu Daud katika Kitabu cha Sunan, ambacho ni mojawapo ya Sahihi sita: “Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu:

Lau haitabakia katika dunia isipokuwa siku moja tu, basi Mwenyezi Mungu angeliirefusha siku hiyo mpaka amtume mtu kutoka katika watu wa nyumba yangu (Ahlu bayt) jina lake linafanana na jina langu, na jina la baba yake ni kama la baba yangu, ataijaza ardhi uadilifu baada ya kujazwa dhulma na jeuri”1

Kanuni ya maisha hailikatai hilo, bali inalithibitisha na kulisisitiza. Ikiwa nguvu hivi sasa ziko mikononi mwa unyama wenye kudhuru wa umoja wa mataifa, baraza la usalama n.k. basi hakuna litakalozuia, siku moja kugeuka nguvu hiyo kutoka mikononi mwa madhalimu waovu hadi kwa watu wa haki na uadilifu; bali maumbile yanapenda kujikomboa na dhulma.

Pia kuna misingi isemayo: “Kila kilicho katika ardhi kina harakati, kama ilivyo na harakati ardhi na kwamba kudumu hali ni muhali.” Yote hayo yanapelekea kuwa hatimaye nguvu zitakuwa mikononi mwa wema wanao- faa.

Hakika katika haya kuna ujumbe kwa wafanyao ibada.

Haya ni haya ya kuwa ardhi itarithiwa na waja wema; hata kama ni baada ya muda. Makusudio ya wafanyao ibada hapa ni wale wanaopata mawaidha kwa kuzingatia na kunufaika na maonyo.

Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.). Risala yake ni rehema kwa wa mwanzo na wa mwisho. Huko nyuma tumeeleza mara nyingi kuhusu misingi ya risala hiyo na mafunzo yake.

Inatosha, kuthibitisha hilo, kauli za mwenye risala hiyo; kama vile: “Hakumwamini Mwenyezi Mungu yule ambaye watu hawamwamini. Likikuhuzunisha ovu na likakufurahisha jema, basi wewe ni mumin.”

Ni kwa hisia hizi ndio uadilifu utasimama, amani kuenea na maisha kuwa bora. Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu hilo katika Juz. 7 (6:92).

قُلْ إِنَّمَا يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَٰهُكُمْ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَهَلْ أَنْتُمْ مُسْلِمُونَ {108}

Sema: Hakika umeletwa wahyi kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Je nyinyi mmesilimu?

فَإِنْ تَوَلَّوْا فَقُلْ آذَنْتُكُمْ عَلَىٰ سَوَاءٍ ۖ وَإِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ أَمْ بَعِيدٌ مَا تُوعَدُونَ {109}

Kama wakikataa, basi sema: Nimewatangazia sawasawa. Wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa.

إِنَّهُ يَعْلَمُ الْجَهْرَ مِنَ الْقَوْلِ وَيَعْلَمُ مَا تَكْتُمُونَ {110}

Hakika Yeye anajua kauli ya dhahiri na anajua mnayoyaficha.

وَإِنْ أَدْرِي لَعَلَّهُ فِتْنَةٌ لَكُمْ وَمَتَاعٌ إِلَىٰ حِينٍ {111}

Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.

قَالَ رَبِّ احْكُمْ بِالْحَقِّ ۗ وَرَبُّنَا الرَّحْمَٰنُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ {112}

Akasema: Mola wangu! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasifia.
  • 1. Tumezungumzia kuhusu Mahdi anayengojewa katika Juz. 1( 2:127 - 129) na Juz. 15 (17: 58)