read

Aya 108 – 112: Hakika Mungu Wenu Ni Mmoja Tu

Maana

Sema: Hakika umeletwa wahyi kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Je nyinyi mmesilimu?

Mwenyezi Mungu alimwarisha Mtume wake awaambie washirikina kuwa Mwenyezi Mungu ameniletea wahyi kwamba Yeye ni mmoja tu hana mshirika katika kuumba kwake na wala katika ujuzi wake.

Ulimwengu huu na maajabu yake na kanuni zake unashuhudia kwa uwazi juu ya umoja, uweza na ukuu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Basi kwa nini hamuamini na kufuata amri yake? Kwanini mnadanganyika kuacha kumwabudu Yeye na kwenda kuabudu mawe yasiyodhuru wala kunufaisha?

Kama wakikataa, basi sema: Nimewatangazia sawasawa.

Baada ya kuwalazimu hoja ya kufikisha na maonyo, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu awaambie kuwa nimekishatekeleza wajibu wangu na nikafikisha risala ya Mola wangu. Kwa hiyo haukubaki udhuru wowote kwenu.

Wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyoahidiwa.

Mimi nina yakini na adhabu yenu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameiahadi na kuwahadhirisha nayo, na ahadi yake Mwenyezi Mungu ni ya kweli na adhabu yake pia ni kali zaidi, lakini sijui itakuwa lini. Ni sawa iwe karibu au mbali, lakini ina wakati wake. Ngojeni nami niko pamoja nanyi katika wenye kungojea.

Hakika Yeye anajua kauli ya dhahiri na anajua mnayoyaficha.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:7).

Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.

Sijui kuna hekima gani ya kupewa kwenu muda na kucheleweshewa adhabu. Je Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaka kumdhirisha kila mmoja hakika yake, aweze kutubia mwema na aendelee mouvu au ametaka mustarehe siku zilizobakia kwenye umri wenu? Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye.

Akasema (Muhammad): Mola wangu! Hukumu kwa haki.

Yaani idhihirishe haki na uwanusuru watu wake kwa wale wanaoipinga.

Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasema kuwa masanamu yenu ni miungu na madai yenu kwangu kuwa ni mzushi.

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wewe ni mtukufu kwa kila anayekuzulia. Wema ni wa yule anayekufuata, akachukua athari yako na akamwambia mzushi, kama vile ulivyosema wewe:

Na Mola wetu ni Mwingi wa rehema aombwaye msaada juu ya mnayoyasifia.”