read

Aya 15 -18: Ajinyonge

Lugha

Wengi wamesema kuwa makusudio ya mbingu hapa ni dari ya nyumba, kukata ni kujinyonga na hila yake ni huko kujinyonga kwake. Kwa hiyo maana yatakuwa: Anayedhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru katika dunia na Akhera, basi na afunge kitanzi ajinyonge aone je huko kujinyonga kutamuondolea ghadhabu yake?

Maana

Wafasiri wengi wamesema kuwa dhamiri ya ‘hawatamnusuru’ inamrudia Muhammad (s.a.w.) na maana yawe: Anayedhani katika washirikina kuwa Mwenyezi Mungu hatamnusuru Mtume wake Muhammad (s.a.w.), basi na amnyonge aone kama Mwenyezi Mungu hatamnusuru Mtume wake.

Lakini dhahiri ya mfumo wa Aya inaonyesha kuwa dhamiri inamrudia huyo anayedhani, kwa sababu Muhammad (s.a.w.) hakutajwa katika Aya. Na maana yanakuwa:

Ambaye ameshukiwa na balaa na akachukia kadha ya Mwenyezi Mungu na kadari yake, akakata tamaa kwamba Mwenyezi Mungu atamsaidia duniani na kumpa thawabu akhera kwa sababu ya kuvumilia kwake, atakayekuwa hivyo basi hatakuwa na la kufanya isipokuwa kujinyonga kwa kujifunga kamba kwenye dari ya nyumba yake; kisha aangalie je, hilo ndilo suluhisho?

Mwenye akili anapotokewa na balaa, hufanya juhudi na bidii kuiondoa huku akitaka msaada kwa Mwenyezi Mungu, akifaulu ni sawa, la sivyo humwachia Mwenyezi Mungu mambo yote huku akingoja fursa.

Na namna hiyo tumeiteremsha kuwa ni Aya zilizo wazi na kwamba Mwenyezi Mungu humuongoza anayetaka.

Dhamiri katika iliyoteremshwa inarudia Qur’an. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) humwongoza anayetaka kuongoka kwa Kitabu chake na humwongoza kwenye wema wa nyumba mbili yule anayetafuta mwongozo kwake na kwa Mtume wake.

Na mwenye kutafuta upotevu na ufisadi ataipata njia yake kwa wafisadi na wapotevu.

Hakika wale ambao wameamini na ambao ni mayahudi na wasabai na wanaswara na wamajusi na wale washirikishao, hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya kila kitu.

Wasabai wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, lakini wanaamini kuwa baadhi ya nyota zina athari katika kheri na shari, wamajusi wanaabudu moto kwa kusema kuwa kheri inatokana na nuru na shari inatokana na giza na wanaswara ni wakristo.

Mwenyezi Mungu anayajua makundi yote haya sita na atayapambanua kesho siku ya Kiyama na kumlipa kila mmoja kwa vile alivyofanya. Kafiri atamwingiza motoni na mumin atamwingiza Peponi. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 1 (2:117).

Je huoni kuwa vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini na jua na mwezi na nyota na milima na miti na wanyama.

Wamesema jamaa katika wafasiri kwamba makusudio ya kusujudi wanyama mimea n.k. Ni kutii amri yake na kwamba yeye anawafanyia vile atakavyo.

Katika Juz. 15 (17:44) tumeeleza kuwa makusudio ya kusujudi vitu visivyo na harakati, miti na mimea ni kule kufahamisha kwake kuweko muumba wake na utukufu wake. Mulla Sadra katika kitabu Al-Asfar anasema: “Vitu vyote vina akili, vinamfahamu Mola wake na kumjua muumba wake, vinasikia maneno yake na kufuata amri yake”

Haya hayako mbali, akili inakubali na dhahiri ya nukuu inalithibitisha. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَإِنْ مِنْ شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَٰكِنْ لَا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ ۗ {44}

“Na hapana kila kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake, lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake.” Juz. 15 (17:44).

Sayansi itagundua hakika hii hivi karibuni au baadaye.

Na wengi miongoni mwa watu wanamwamini na wanamsujudia. Na wengi miongoni mwao imewastahili adhabu.

Hao ni wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu wanaowadharau wale wanaomwamini Mungu. Ilikuwa inafaa kwa mwenye kitabu Al-Asfar, awavue wanaomkana Mungu katika viumbe.

Na anayetwezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumheshimu.

Kabisa! Hakuna wa kumuinua aliyeangushwa na kudhalilishwa na Mwenyezi Mungu, wala hakuna wa kumdhalilisha aliyetukuzwa na kuenziwa na Mwenyezi Mungu, na hakuna utukufu mbele ya Mwenyezi Mungu ila kwa wenye takua.

Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo kuwatukuza wema na kuwatweza wapotevu na wafisadi.

Baada ya hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ana desturi katika viumbe vyake haiachi; nayo ni kuwa mwenye kufuata nji ya maangamizi ataangamia, na mwenye kufuata njia ya usalama atasalimika. Njia ya usalama mbele ya Mwenyezi Mungu ni imani ya kweli na matendo mema; na njia ya kufedheheka na kupuuzwa ni unafiki na ufisadi katika ardhi.

هَٰذَانِ خَصْمَانِ اخْتَصَمُوا فِي رَبِّهِمْ ۖ فَالَّذِينَ كَفَرُوا قُطِّعَتْ لَهُمْ ثِيَابٌ مِنْ نَارٍ يُصَبُّ مِنْ فَوْقِ رُءُوسِهِمُ الْحَمِيمُ {19}

Hawa mahasimu wawili waliohasimiana kwa ajili ya Mola wao. Basi waliokufuru watakatiwa nguo za moto na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayochemka.

يُصْهَرُ بِهِ مَا فِي بُطُونِهِمْ وَالْجُلُودُ {20}

Kwayo vitayeyushwa vilivyo matumboni mwao na ngozi.

وَلَهُمْ مَقَامِعُ مِنْ حَدِيدٍ {21}

Na yatakuwako makomeo ya chuma kwa ajili yao.

كُلَّمَا أَرَادُوا أَنْ يَخْرُجُوا مِنْهَا مِنْ غَمٍّ أُعِيدُوا فِيهَا وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ {22}

Kila wanapotaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo; na onjeni adhabu ya kuungua.

إِنَّ اللَّهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِنْ ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا ۖ وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ {23}

Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walioamini na wakatenda mema katika bustani zipitiwazo na mito chini yake. Watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu na lulu na mavazi yao humo ni hariri.

وَهُدُوا إِلَى الطَّيِّبِ مِنَ الْقَوْلِ وَهُدُوا إِلَىٰ صِرَاطِ الْحَمِيدِ {24}

Na wataongozwa kwenye maneno mazuri na kuongozwa kwenye njia ya mwenye kuhimidiwa.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَيَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاءً الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِ ۚ وَمَنْ يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍ بِظُلْمٍ نُذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ {25}

Hakika wale waliokufuru na wakawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti mtakatifu ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawa sawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakayefanya upotofu humo kwa dhulma tutamwonjesha adhabu chungu.