read

Aya 16 – 23: Je, Vitendo Vyake Mwenyezi Mungu Mtukufu Vina Malengo?

Maana

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa mchezo.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:191). Huko tumenukuu kauli kuhusiana na kuwa je, vitendo vya Mwenyezi Mungu vinakuwa na sababu ya malengo au kwake Mwenyezi Mungu hakuna ubaya wala hana wajibu wa chochote?

Kama tungelitaka kufanya mchezo tungelijifanyia sisi wenyewe, kama tungekuwa ni wafanyao mchezo.

Mchezo na upuuzi ni muhali kwa yule anayekiambia kitu kuwa na kikawa. Ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: ‘Lau tungelitaka ... kama tungekuwa ni wafanyao mchezo’ yaani hatukataka wala hatufanyi. Lau angelitaka kufanya mchezo – kukadiria muhali sio muhali – angelijifanyia kwa namna yoyote inayolingana na cheo chake; sio katika namna ya waja; kama kucheza na wanawake na watoto.

Bali tunaitupa haki juu ya batili ikaivunja na mara ikatoweka.

Makusudio ya haki hapa ni ukweli na uhakika kwa mkabala wa mchezo alioukanusha Mwenyezi Mungu Mtukufu na makusudio ya batili hapa ni upuzi na mchezo.

Baada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kusema hatufanyi mchezo sasa anasema kuwa vitendo vyake kwake ni uhakika na ukweli si mchezo na upuzi; bali ukija upuzi na mchezo kutoka popote anauvunjilia mbali. Vipi ataliridhia lile asiloliridhia kwa mwingine?

Na ole wenu kwa mnayoyasifia nayo Mwenyezi Mungu na kumbandika sifa za kutengeneza.

Ni vyake vilivyoko mbinguni na ardhini na walioko mbele yake hawafanyi kiburi wakaacha kumwabudu wala hawachoki.

Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya walioko mbele yake, ni Malaika. Tunavyofahamu sisi ni kuwa makusudio ni kila mwenye cheo na jaha mbele ya Mwenyezi Mungu, awe Malaika au mtu.

Wanamsabihi usiku na mchana wala hawanyonyog’onyei.

Yaani hawachoki, bali wanadumu kwenye twaa katika kauli na vitendo wala hawamtuhumu Mwenyezi Mungu kwa kumsawirisha au kumpa sifa za kutengeneza.

Au wamepata miungu katika ardhi inayofufua.

Yaani kila anayeabudiwa na washirikina, hawezi kuhui wafu wala hawafufui wafu walio makaburini, bali Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayehui na kufisha.

Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi zingefisidika. Ametasika Mwenyezi Mungu, Mola wa arshi, na hayo wanayoyazua.

Tazama tuliyoyaandika kwenye Juz. 5 (4:48) Kifungu ‘Dalili ya umoja na utatu.’

Mwenye kujua ni hoja kwa asiyejua Yeye hahojiwi kwa ayatendayo na wao ndio wanaohojiwa kwa wayatendayo.

Baadhi wametoa dalili kwa Aya hii kwamba hakuna ubaya kwa Mungu wala hawajibikiwi na jambo lolote. Anaweza kumwadhibu mtiifu na kumlipa thawabu muasi. Lakini hii inapingana na uadilifu wake, hekima na rehema yake.

Usahihi hasa ni kuwa maana ya Aya ni Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kuwa ni mwadilifu kwa dhati yake, haijuzu kwa yeyote kumwingilia kwa kauli yake na vitendo vyake. Kwa sababu haijuzu kuambiwa mwadilifu, kwa nini umefanya uadilifu? Na mkweli, kuambiwa kwa nini umesema kweli? Kama ambavyo haifai kwa asiyejua utabibu kumwambia tabibu hodari, kwa nini unatoa dawa hii?

Mfano wa maswali haya unafaa kwa aliye kifani wake. Ama asiyejua kitu, analotakiwa ni kufanya juhudi ya kumtafuta mjuzi na kuhakikisha ujuzi wake kutokana na dalili na alama. Akishapata uhakika basi inakuwa ni wajibu kwake kumfuata kwa yale aliyo na ujuzi nayo; sawa na mgonjwa anavyomfuata tabibu.

Walikwishasema wahenga: “Ajuaye ni hoja kwa asiyejua.” Ikiwa mambo ni hivi kwa kiumbe pamoja na kiumbe mwenzake. Itakuwaje kwa kiumbe pamoja na muumba wa mbingu na ardhi?
Siku moja mwanafunzi alimuuliza mwalimu wake: “Kwa nini tuko na kwa nini tunaishi?”

Mwalimu akamwambia mwanafunzi wake: “Kwa nini ewe mwanangu unajilazimisha na mambo yasiyokuwa na mwanzo wala mwisho? Kwa nini usiamini dini ikastarehe nafsi yako na uawache yale usiyoyaweza, ufuate unayoyaweza? Wewe ni mmoja wa maelfu ya mamilioni ya watu na mji wako uanaoishi ni moja ya maelfu ya miji. Ardhi tunayoishi ni moja ya mamilioni ya sayari na ulimwengu ulio na sayari zote hizo, hatujui kuwa kuna mfano wake unaouzidia. Je, sehemu moja inaweza kudhibiti yote hayo? Je, tone moja linaweza kuihoji bahari?

Mwanangu! Mimi sisemi kuwa usifanye uchunguzi na kupeleleza, kwani kutafuta hakika ni miongoni mwa sababu za kupatikana binadamu, lakini maadamu akili yako ni ndogo kuweza kufahamu hakika hiyo, basi ngoja mpaka uzidi kupata ufahamu na utambuzi. Mwisho ukishindwa, liache jambo kama lilivyo. Kwa sababu udogo wa akili yako kufahamu jambo, haimaanishi kuwa jambo hilo ni mchezo na upuzi; isipokuwa inamaanisha kuwa hujalifahamu; kwa hiyo muachie aliyeumba vyote vilivyoko.”

أَمِ اتَّخَذُوا مِنْ دُونِهِ آلِهَةً ۖ قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ ۖ هَٰذَا ذِكْرُ مَنْ مَعِيَ وَذِكْرُ مَنْ قَبْلِي ۗ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ الْحَقَّ ۖ فَهُمْ مُعْرِضُونَ {24}

Au wamejifanyia miungu mingine badala yake. Sema, leteni dalili yenu. Hii ni ukumbusho wa walio pamoja nami na ukumbusho wa waliokuwa kabla yangu. Lakini wengi wao hawajui haki kwa hiyo wanapuuza.

وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ قَبْلِكَ مِنْ رَسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ {25}

Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimpa wahyi kwamba hapana Mungu isipokuwa mimi, basi niabuduni mimi tu.

وَقَالُوا اتَّخَذَ الرَّحْمَٰنُ وَلَدًا ۗ سُبْحَانَهُ ۚ بَلْ عِبَادٌ مُكْرَمُونَ {26}

Na wanasema, Mwingi wa rehema ana mwana! Ametakasika na hayo! Bali hao ni waja waliotukuzwa.

لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُمْ بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ {27}

Hawamtangulii kwa neno nao wanafanya kwa amri yake.

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ وَهُمْ مِنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ {28}

Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamuombei yeyote ila yule anayemridhia. Nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea.

وَمَنْ يَقُلْ مِنْهُمْ إِنِّي إِلَٰهٌ مِنْ دُونِهِ فَذَٰلِكَ نَجْزِيهِ جَهَنَّمَ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ {29}

Na yeyote miongoni mwao atakayesema: mimi ni mungu, badala yake, basi tutamlipa Jahannamu. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.