read

Aya 19 – 25: Mahasimu Wawili

Maana

Hawa mahasimu wawili waliohasimiana kwa ajili ya Mola wao.

Kuna maelezo katika Tafsir At-Tabari kwamba Abu dharr alikuwa akiapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba Aya hii imeshuka kwa ajili ya watu sita katika makuraishi; watatu miongoni mwao ni waumini nao ni Hamza bin Abdul-Muttalib, Ali bin Abu Twalib na Ubayda bin Al-Harith.

Na watatu ni katika washirikina nao ni: Utba na Shayba, watoto wa Rabia na Walid bin Utba. Uhasama baina yao ulikuwa katika vita vya Badr walipobariziana; na Mwenyezi Mungu akawapa nusra waumini kuwashinda washirikina.

Jamaa katika wafasiri wamesema kwamba makusudio ya waliohasimiana ni kikundi cha waumini na kikundi cha makafiri ambao ni mayahudi, wanaswara, wasabai, majusi na washirikina. Kwa sababu wote hao wametajwa katika Aya iliyotangulia na kila kundi linasema lina haki kuliko jingine.

Vyovyvote iwavyo ni kwamba uhasama katika dini unatokea baina ya wanaoamini.

Basi waliokufuru watakatiwa nguo za moto na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayochemka. Kwayo vitayeyushwa vilivyo matumboni mwao na ngozi. Na yatakuwako makomeo ya chuma kwa ajili yao. Kila wanapotaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo, na onjeni adhabu ya kuungua.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria uhasama wa waumini na makafiri anataja kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu mwisho wake ni Peponi na mwenye kumkufuru mwisho wake ni Jahannam, mwisho mbaya kabisa.
Na kwamba watu wake watavaa kivazi cha moto na watamiminiwa maji ya moto ambayo yatayeyusha mafuta, nyama matumbo na ngozi. Pia nguzo za chuma zitakuwa vichwani mwao kuwazuia kutoka kila wanapojaribu kukimbia. Inawezekena kukimbia hukumu ya Mwenyezi Mungu na matakwa yake? Umepita mfano wake katika Juz. 13 (14: 49 – 50) kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi’

Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walioamini na wakatenda mema katika bustani zipitiwazo na mito chini yake. Watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu na lulu na mavazi yao humo ni hariri.

Makafiri watakuwa na mavazi ya moto, makomeo ya chuma, maji ya moto na waumini wenye ikhlasi watapata pepo yenye neema, mito yenye kinywaji cha ladha, nguo za hariri na vipambo vya dhahabu na lulu.

Na wataongozwa kwenye maneno mazuri.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria kwenye chakula na kinywaji chao, anataja kauli zao ambazo ni nzuri; mfano Alhamdulillah. Na kuongozwa kwenye njia ya mwenye kuhimidiwa. Hiyo ni njia yenye kunyooka waliyoifuata katika maisha ya dunia, ikawapeleka kwenye neema ya Akhera.

Hakika wale waliokufuru na wakawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti mtakatifu ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawa- sawa, kwa wakaao humo na wageni.

Washirikina wa kikuraishi walikuwa wakiwazuilia watu kuiingia kwenye Uislamu, kuhiji na kufanya umra kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo ameifanya ni mahali pa kuendewa na watu na mahali pa amani. Umepita mfano wake katika Juz. 1 (2:125).

Na kila atakayefanya upotofu humo kwa dhulma tutamwonjesha adhabu chungu.

Yaani atakayeacha yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu na akamfanyia uovu anayeikusudia nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu, basi Mungu atamwadhibu adhabu kubwa.

وَإِذْ بَوَّأْنَا لِإِبْرَاهِيمَ مَكَانَ الْبَيْتِ أَنْ لَا تُشْرِكْ بِي شَيْئًا وَطَهِّرْ بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْقَائِمِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ {26}

Na tulipomwekea Ibrahim mahala penye ile nyumba kwamba usinishirikishe na chochote na uitwaharishe nyumba yangu kwa ajili ya wanozunguka na wakaazi na wanaorukui na wanaosujudi.

وَأَذِّنْ فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالًا وَعَلَىٰ كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِنْ كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ {27}

Na watangazie watu Hijja; watakujia kwa miguu na juu ya kila mnyama aliyekonda kutoka kila njia ya mbali.

لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فِي أَيَّامٍ مَعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُمْ مِنْ بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ {28}

Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalum juu ya wanyama hawa aliowaruzuku.

ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ {29}

Basi kuleni katika hao na mumlishe mwenye shida aliye fukara, kisha wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao na waizunguke sana nyumba ya kale.