read

Aya 24 – 29: Leteni Dalili Zenu

Maana

Au wamejifanyia miungu mingine badala yake. Sema leteni dalili yenu.

Kila mtu huwa anasema, mwenye kudai ni lazima alete ushahidi; hata kama yule anayeelekezewa madai ni mtu duni; sikwambii akiwa ni mshirika wa Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake. Basi iko wapi dalili?

Hii Qur’an ni ukumbusho wa walio pamoja nami na ukumbusho wa waliokuwa kabla yangu.

Vitabu vyote vya mbinguni vinaamrisha Tawhid na kukataza shirki. Ikiwa shirki haina dalili ya kiakili wala ya kinakili, basi chimbuko lake ni ujinga na upofu.

Lakini wengi wao hawajui haki kwa hiyo wanapuuza. Hii ni kukemea ujinga wao na upotevu wao.

Na hatukumtuma kabla yako Mtume yoyote ila tulimpa wahyi kwam- ba hapana Mungu isipokuwa mimi, basi niabuduni mimi tu.

Aya hii ni ubainifu na tafsiri ya Aya iliyo kabla yake. Ya kwanza inasema kuwa hakuna athari yoyote ya shirki katika vitabu vya Mwenyezi Mungu na hii inasema kuwa hakutumwa mtume yeyote isipokuwa kwa ajili ya tawhidi na kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu katika ibada.

Na wanasema, Mwingi wa rehema ana mwana. Ametakasika na hayo! Bali hao ni waja wa waliotukuzwa.

Mayahudi au kikundi katika wao walisema kuwa Uzayr ni mwana wa Mungu, Wanaswara (wakiristo) wakasema Masih ni mwana wa Mungu; na baadhi ya makabila ya kiarabu yakasema kuwa Malaika ni mabinti wa Mungu.

Ndio Mwenyezi Mungu akawarudi wote hao, kwamba mliowataja ni waja sio watoto, tena wao wana daraja na cheo mbele ya Mola wao.

Ajabu ni yale yaliyoelezwa katika Tafsiri At-Tabari, akiwanukuu waliosema kuwa Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu: “Mwenyezi Mungu alimuoa jini akamzalia Malaika.” Hili ameliashiria Mwenyezi Mungu katika kauli yake:

وَجَعَلُوا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجِنَّةِ نَسَبًا ۚ {158}

“Na wameweka mahusiano ya nasaba baina Yake na majini” (37:158).

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akabainisha sababu ya daraja ya Uzayr, Masih na Malaika mbele yake, kwa kusema:

Hawamtangulii kwa neno nao wanafanya kwa amri yake.

Yaani wao hawatumii rai wala kiasi.

Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao.

Yaliyo mbele yao ni fumbo la vitendo vyao vya sasa na yaliyo nyuma yao ni vitendo vyao vilivyopita. Maana ni kuwa Yeye Mwenyezi Mungu anayajua vizuri matendo yao ya kheri na makusudio yao mazuri; naye atawalipa ujira wao kwa yale mazuri waliyoyafanya.

Wala hawamuombei yeyote ila yule anayemridhia Yeye.

Hii ni kumrudi yule anayemwabudu Mtume, walii au Malaika kwa tamaa ya kuombewa kwa Mungu. Kwa maana kwamba waja waliotukuzwa watawaombea wale wenye kuridhiwa na Mwenyezi Mungu sio washirikina walioghadhibikiwa.

Nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea pamoja na kuwa wana ikhlasi na vyeo mbele ya Mwenyezi Mungu.

Na yeyote miongoni mwao atakayesema: mimi ni mungu, badala yake, basi tutamlipa Jahannamu. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.

Hao waja wema waliotukuzwa, lau mmoja atadai kuwa yeye ni mungu badala ya Mwenyezi Mungu au ni mshirika wake, basi malipo yake yatakuwa ni Jahannamu, kama washirikina wengine, bila ya kuwa na tofauti yoyote.

أَوَلَمْ يَرَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ كَانَتَا رَتْقًا فَفَتَقْنَاهُمَا ۖ وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ ۖ أَفَلَا يُؤْمِنُونَ {30}

Je, hao waliokufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha tukaziambua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai. Je, hawaamini?

وَجَعَلْنَا فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَنْ تَمِيدَ بِهِمْ وَجَعَلْنَا فِيهَا فِجَاجًا سُبُلًا لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ {31}

Na tukaweka katika ardhi milima ili isiwayumbishe. Na tukaweka humo upana wa njia ili wapate kuongoka.

وَجَعَلْنَا السَّمَاءَ سَقْفًا مَحْفُوظًا ۖ وَهُمْ عَنْ آيَاتِهَا مُعْرِضُونَ {32}

Na tukaifanya mbingu kuwa sakafu iliyohifadhiwa, lakini wanazipuuza ishara.

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ فِي فَلَكٍ يَسْبَحُونَ {33}

Na Yeye ndiye aliyeumba usiku na mchana na jua na mwezi. Kila kimoja katika anga vinaogoelea.

وَمَا جَعَلْنَا لِبَشَرٍ مِنْ قَبْلِكَ الْخُلْدَ ۖ أَفَإِنْ مِتَّ فَهُمُ الْخَالِدُونَ {34}

Na hatukumjaalia mtu yeyote wa kabla yako kuishi milele. Je, ukifa wewe wao wataishi milelele?

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَنَبْلُوكُمْ بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ {35}

Kila nafsi itaonja mauti. Na tutawajaribu kwa mtihani wa shari na kheri na kwetu mtarejeshwa.

وَإِذَا رَآكَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ يَتَّخِذُونَكَ إِلَّا هُزُوًا أَهَٰذَا الَّذِي يَذْكُرُ آلِهَتَكُمْ وَهُمْ بِذِكْرِ الرَّحْمَٰنِ هُمْ كَافِرُونَ {36}

Na wanapokuona wale ambao wamekufuru hawakufanyii ila mzaha: Je, huyu ndiye anayewataja miungu wenu? Na hao ndio wanaokataa dhikri ya Mwingi wa rehema.