read

Aya 26 -29: Itwaharishe Nyumba Yangu

Maana

Na tulipomwekea Ibrahim mahala penye ile nyumba kwamba usin- ishirikishe na chochote na uitwaharishe nyumba yangu kwa ajili ya wanozunguka na wakaazi na wanaorukui na wanaosujudi.

Makusudio ya wakaazi ni wakaazi wa Makka na viunga vyake; na wanorukui wakisujudi ni wanaoswali.

Makuraishi walikuwa wakiabudu masanamu na wakisimamia Al-Kaaba. Baada ya Mwenyezi Mungu kumtuma Muhammad (s.a.w.) walianza kuwa na uadui naye na kila anayemwamini, tena wakawazuilia waislamu kuizunguka (tawaf) na kuswali hapo; kama ilivyoelezwa kwenye Aya iliyotangulia. Pamoja na hayo Makuraishi walikuwa wakidai kwamba wako kwenye dini ya Ibrahim (a.s.).

Ndio Mwenyezi Mungu akabatilisha madai yao haya, kwamba yeye ndiye mwenye nyumba hiyo na alimpa wahyi kuwa aijenge na aifanye ni mahsusi kwa ibada ya wanaompwekesha Mungu wanaokaa hapo na wanaopita na pia kuwaweka mbali nayo washirikina na mizimu yao.

Haya ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Na uitwaharishe nyumba yangu’ lakini makuraishi waliipindua Aya, wakaijaza masanamu nyumba ya Mwenyezi Mungu, wakaihalalishia washirikina na wafisadi na wakawazulia nayo watu wa tawhid na wema.

Na watangazie watu Hijja; watakujia kwa miguu na juu ya kila mnyama aliyekonda kutoka kila njia ya mbali.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha kipenzi chake awaite watu kuhiji kwenye msikiti mtakatifu baada ya kusimamisha misingi yake na kutimia jengo. Akamwahidi kuwa watu watamwitikia na watamjia kwa kila hali; kutembea kwa miguu na kupanda ngamia au farasi waliokonda tena kutoka mbali, sikwambii karibu.

Ili washuhudie manufaa yao.

Hijja ni ibada pekee inayochanganya manufaa ya kidini na ya kidunia. Ama ya kidini ni kumtii Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza faradhi ya Hijja, kutubia na kutambua haiba ya Mwenyezi Mungu na utukufu. Ibn Al- Arabi anasema katika Kitabu Futuhatul- Makkiyya:

“Siku moja nilikuwa nikitufu Al-Kaaba nikaiona kama kwamba imenyanyuka kutoka ardhini, wallah, ikaniambia maneno niliyoyasikia: njoo uone nitakavyokufanyia, mara ngapi hadhi yangu unaiweka chini na ya binadamu unaiinua juu?.

Nasi tunasema kwa uhakika: hakuna yeyote anayefanya sa’yi au tawaf katika nyumba ya Mwenyezi Mungu kwa ikhlas ila atahisi aina ya kitu kama hiki.

Na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalum juu ya wanyama howa aliowaruzuku, ambao ni ngamia ng’ombe na mbuzi na kondoo.

Kumtaja Mwenyezi Mungu kwenye wanyama ni kinaya cha kuchinja, kwa sababu kusoma Bismillah ni wajibu katika kuchinja. Makusudio ya siku maalum ni siku za kuchinja katika Hijja, kama inavyofahamisha Aya.

Mafakihi wametofautiana katika idadi ya siku hizo: Shia wamesema ni nne, mwanzo wake ni siku ya Idul-adh’ha na mwisho wake ni tarehe kumi na tatu ya Dhul-hijja. Mafakihi wa madhehbu mengine wamesema ni tatu kwa kuishia tarehe kumi na mbili. Ufafanuzi uko katika kitabu chetu Alfiqh ala madhahibil-khamsa1

Razi anasema kuwa maulama wengi wanatofautisha baina ya siku maalum na siku za kuhisabiwa zilizotajwa katika Juz. 2 (2:203) na wanaona kuwa siku maalum ni siku kumi za mwezi wa Dhul-hijja na za kuhisabiwa ni siku za kuchinja.

Basi kuleni katika hao na mumlishe mwenye shida aliye fukara.

Wameafikiana mafakihi kuhusu wajibu wa kumlisha fukara mnyama wa Hijja na wakatofautina katika wajibu wa mwenyewe kula. Sisi tuko pamoja na wale wanaosema kuwa si wajibu kwa mwenyewe kula. Ni vile atavyoona, akipenda atakula na akipenda ataitoa sadaka yote. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Kuleni katika hao’ ni kwa ajili ya kuondoa fikra ya uharamu wa kula; ambapo wakati wa jahiliya walikuwa hawali wanyama hao wawachinjao wakidai kuwa ni haramu kwao. Ndipo Mwenyezi Mungu akawazindua kosa lao hilo.

Kisha wajisafishe taka zao.

Haijuzu kwa aliye kwenye Hijja akiwa kwenye ihram (Vazi maalum la Hijja) kunyoa, kukata kucha au kujipaka manukato; bali mafakihi au wengi wao wamesema kuwa hata kuua vidudu vya mwilini, kama vile chawa pia ni haramu. Zikiisha zile siku za Ihram basi inakuwa ni halali kwake yale yaliyokuwa ni haramu, basi hapo atanyoa, kukata kucha n.k. Ndipo kwa hili ameshiria Mwenyezi Mungu aliposema:

Kisha wajisafishe taka zao.

Na watimize nadhiri zao, ikiwa wameweka nadhiri siku za Hijja au kabla. Kwa sababu watu wengi huweka nadhiri ya kutoa sadaka ikiwa Mwenyezi Mungu atawaruzuku Hijja.

Na waizunguke sana nyumba ya kale. Kwa sababu ndio nyumba ya kwanza kuwekewa watu kwa ajili ya ibada.

Mwenyezi Mungu ameleta tamko la ‘sana’ kwa sababu ni Sunna kufanya tawaf mara nyingi; kama ambavyo pia ni Sunna kuswali sana. Kuna Hadithi mashuhuri kutoka kwa Mtume wa rehema, aliposema: “Kuizunguka Al-Kaaba ni Swala.’

ذَٰلِكَ وَمَنْ يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَهُ عِنْدَ رَبِّهِ ۗ وَأُحِلَّتْ لَكُمُ الْأَنْعَامُ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ ۖ فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ وَاجْتَنِبُوا قَوْلَ الزُّورِ {30}

Ndivyo hivyo! Na anayeitukuza miiko ya Mwenyezi Mungu hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake. Na mmehalalishiwa wanyama howa ila wale mliosomewa. Basi jiepusheni na uchafu wa mizimu na mjiepushe na kauli ya uzushi.

حُنَفَاءَ لِلَّهِ غَيْرَ مُشْرِكِينَ بِهِ ۚ وَمَنْ يُشْرِكْ بِاللَّهِ فَكَأَنَّمَا خَرَّ مِنَ السَّمَاءِ فَتَخْطَفُهُ الطَّيْرُ أَوْ تَهْوِي بِهِ الرِّيحُ فِي مَكَانٍ سَحِيقٍ {31}

Kwa kumtakasia imani Mwenyezi Mungu bila ya kumshirikisha. Na anayemshrikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukampeleka mahala mbali.

ذَٰلِكَ وَمَنْ يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّهِ فَإِنَّهَا مِنْ تَقْوَى الْقُلُوبِ {32}

Ndivyo hivyo! Na anayezitukuza nembo za Mwenyezi Mungu. Basi hiyo ni katika takua ya nyoyo.

لَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ إِلَىٰ أَجَلٍ مُسَمًّى ثُمَّ مَحِلُّهَا إِلَى الْبَيْتِ الْعَتِيقِ {33}

Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda uliowekwa kisha mahali pake ni nyumba ya kale.

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ جَعَلْنَا مَنْسَكًا لِيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُمْ مِنْ بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۗ فَإِلَٰهُكُمْ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا ۗ وَبَشِّرِ الْمُخْبِتِينَ {34}

Kila umma tumeujaalia mihanga ya ibada, ili wamtaje Mwenyezi Mungu katika vile alivyowaruzuku katika wanyama howa. Basi Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, Kwa hiyo jisalimisheni kwake. Na wabashirie wanyenyekevu.

الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَالصَّابِرِينَ عَلَىٰ مَا أَصَابَهُمْ وَالْمُقِيمِي الصَّلَاةِ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنْفِقُونَ {35}

Ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka na walio na subira kwa yale yaliyowasibu, na wanao-simamisha Swala, na wanatoa katika tulivyowaruzuku.
  • 1. Kimefasiriwa kwa kiswahili kwa jina la Fiqh katika madhebu tano - Mtarjumu