read

Aya 30 -35: Miiko Ya Mungu Na Nembo Zake

Maana

Ndivyo hivyo! Na anayeitukuza miiko ya Mwenyezi Mungu hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake.

Kutukuza kuko aina nyingi kutegemea na anayetukuzwa na namna ya kutukuzwa inayokubaliana naye.

Hakuna kitu kinachokubaliana na kumtukuza muumba isipokuwa kumtii na kufuata amri yake katika kila jambo. Atakayemtii Mwenyezi Mungu na akafuata amri zake na kuacha makatazo yake, basi atakuwa ametukuza na kuadhimisha miiko yake na nembo zake. Taadhima hii au utiifu huu unamwinua aliyeutenda kwa muumba wake, sio kuwa unamwinua muumbaji, kwa sababu Yeye hawahitajii walimwengu.

Ndio maana akasema:‘Hiyo ni kheri yake mbele ya Mola wake’ yaani kutukuza hukumu za Mwenyezi Mungu kwa kumtii ni kheri ya huyo mtiifu.

Na mmehalalishiwa wanyama howa ila wale mliosomewa.

Mwenyezi Mungu amemharamishia anayehiji kuwinda akiwa katika Ihram yake, pengine anaweza akadhania kuwa ameharamishiwa kula nyama ya wanyama wa kufugwa. Ndio akabainisha kuwa hakuna uhusiano baina ya mawili hayo; na kwamba walioharamishwa ni mfu na waliochinjiwa mizimu. Angalia Juz. 6 (5:3).

Basi jiepusheni na uchafu wa mizimu.

Jiepusheni nayo na msiiabudu, kama mnavyojiepusha na uchafu, kwa sababu yote ni uchafu, ndio maana ikafasiriwa uchafu wa mizimu, ingawaje kuna herufi min, ambayo hapa imekuwa ya kueena na sio ya baadhi, kama inavyokuwa mara kwa mara.

Na mjiepushe na kauli ya uzushi.

Kauli ya uzushi inachanganya kila lilioharamishwa; iwe ni uongo, kusengenya, shutuma na ufyosi. Uzushi mbaya zaidi ni kuleta ushahidi wa uongo, kwa sababu unanyima haki ya Mungu na ya watu. Mtume (s.a.w.) anasema: “Uzushi umelinganishwa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu,” kisha akasoma Aya hii.

Kwa kumtakasia imani Mwenyezi Mungu bila ya kumshirikisha.

Yaani kushikamana na dini ya haki na kuachana na dini potofu. Bila ya kumshirikisha ni msisitizo wa hayo. Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 15 (17:107).
Na anayemshrikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukampeleka mahala mbali.

Hiki ni kinaya cha dhambi ya shirki kwamba haifanani na dhambi yoyote, na kwamba adhabu ya mshirikina haishindwi na adhabu yoyote. Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an na Sunna za Mtume ataona kuwa mshirikina ana dhambi kubwa zaidi kuliko mlahidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Inawezekana siri ya hilo ni kuwa mlahidi hathibitishi upungufu wa muumba, kwa sababu yeye hakubali kabisa kuwa yuko. Hii pia ni dhambi kubwa, hilo halina shaka, lakini dhambi ya mshirikina ni kubwa zaidi, kwa sababu ni kumshirikisha muumba kwa upande mmoja na ni kuthibitisha upungufu kwa muumba kwa upande wa pili.

Ndivyo hivyo! Na anayezitukuza nembo za Mwenyezi Mungu. Basi hiyo ni katika takua ya nyoyo.

Nembo za Mwenyezi Mungu na miiko yake zina maana moja. Tumezungumzia kuhusu miiko katika Aya iliyotangulia. Hakuna mwenye shaka kwamba hawatii amri za Mwenyezi Mungu isipokuwa wenye takua na ikhlasi.

Miongoni mwa kutukuza nembo za Mwenyezi Mungu na kutii hukumu yake ni kuchinja mnyama aliyenona asiye na kasoro yoyote siku za Hijja. Mtume (s.a.w.) anasema: “Hafai aliye kiguru, wala aliyekonda, wala aliyetobolewa sikio wala aliyekatwa sikio wala aliyevunjika pembe.”

Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda uliowekwa.

Katika hao ni hao wa kuchinjwa kwenye Hijja. Muda uliowekwa ni wakati wa kuchinjwa. Maana ni kuwa mwenye kuhiji anaruhusiwa kunufaika na maziwa na mgongo wa mnyama wa kuchinja mpaka wakati wa kuchinja.

Katika Tafsiru-Razi imeelezwa kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alimpitia mtu akimkokokota mnyama na yeye mwenyewe amechoka. Mtume akamwambia: “Mpande.” Yule mtu akasema: “Huyu ni wa kuchinja kwa ajili ya Hijja ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!” Akasema Mtume: “Ole wako, mpande!”

Anaendelea kusema Razi: “Abu Hanifa hajuzishi hilo, akatoa hoja kuwa haijuzu kumkodisha kwa hiyo haijuzu kumpanda.” Razi akamjibu Abu Hanifa kwamba hoja hii ni dhaifu, kwa sababu, mjakazi aliyezaa na mmiliki wake hauzwi, lakini inajuzu kunufaika naye.

Kisha mahali pake ni nyumba ya kale.

Yaani mahali pake pa kuchinjwa ni nyumba ya Mwenyezi Mungu takatifu na makusudio yake ni haram yote ikiwemo Mina. Katika Hadith imeelezwa. Mina yote ni machinjioni.

Kila umma tumeujaalia mihanga ya ibada.

Makusudio ya mihanga ya ibada hapa ni kuchinja wanyama kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu, Ili wamtaje Mwenyezi Mungu katika vile alivyowaruzuku katika wanyama howa, iliyokuja moja kwa moja. Maana ni kuwa hakuna bid’a (uzushi) katika kuchinja mnyama, ilikuweko katika dini zilizotangulia.

Basi Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Kwa hiyo msimtaje mwengine katika dhabihu zenu.

Kwa hiyo jisalimisheni kwake.Yaani fuateni amri yake na mumfanyie ikhlasi katika kauli na vitendo.

Na wabashirie wanyenyekevu, ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na walio na subira kwa yale yaliyowasibu, na wanaosimamisha Swala na wanatoa katika tulivyowaruzuku.
Mpe habari njema ya Pepo, ewe Muhammad, yule anayemnyenyekea Mwenyezi Mungu, akamwogopa akawa na uthabiti kwenye dini wakati wa raha na dhiki, akamwabudu bila ya unafiki wala ria na akatoa mali yake katika kumtii Mungu na kutaka radhi yake. Hakuna shaka kwamba mwenye kukusanya sifa hizi atakuwa na daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu na ya watu.

وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُمْ مِنْ شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ ۖ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرْنَاهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ {36}

Na ngamia wa kunona tumewafanyia kuwa ni miongoni mwa nembo za Mwenyezi Mungu, kwao mna kheri. Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanaposimama safu. Na wanapoanguka ubavu, basi kuleni na mlisheni aliyekinai na aombaye. Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mpate kushukuru.

لَنْ يَنَالَ اللَّهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَٰكِنْ يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنْكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ ۗ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ {37}

Nyama zao hazimfikii wala damu zao, lakini inamfikia takua kutoka kwenu. Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyowaongoa. Na wabashirie wenye kufanya mema.