read

Aya 30 – 36: Maji Ni Uhai

Maana

Je, hao waliokufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha tukazibandua?

Mwanzoni mwa Juzuu ya kwanza tumefafanua maelezo yenye kichwa cha maneno ‘Qur’an na sayansi,’ tukasema kuwa Qur’an ni kitabu cha dini kinachomwongoza mtu kwenye ufanisi wake wa kidunia na akhera; na wala sio kitabu cha nadharia za falsafa, sayansi au falaki n.k.

Na kwamba kila Aya miongoni mwa aya za Qur’an za kilimwengu au za kihistoria, kama vile visa vya mitume, lengo lake ni kutupa mawaidha na mafunzo au kutuongoza kujua kuweko Mwenyezi Mungu, tuweze kumwamini.

Miongoni mwa Aya za kilimwengu ni hii tuliyo nayo. Humo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja mambo mawili: Kwanza, kwamba sayari za Jua, ikiwemo Jua, Ardhi, Mars, Jupita, Zohali, Zebaki n.k. Zote zilikuwa zimeshikana kama kitu kimoja, kisha Mwenyezi Mungu akazipambanua na kila moja akaifanya ni sayari peke yake.

Wataalamu wameikubali nadharia ya kubanduka Jua na Ardhi, lakini wakatofautiana katika namna ya kubanduka kwake. Qur’an nayo haikufafanua kuhusu aina ya kubanduka kwake. Nasi tunayanyamazia yale aliyoyanyamazia Mungu.

Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai.

Hili ni jambo la pili lilotajwa na Aya. Kwamba maji ndio chimbuko la kila kitu kinachokua; awe ni mtu, mnyama au mmea.

Katika Juz. 12 (11:7) Mwenyezi Mungu anasema: “Naye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita na arshi yake ilikuwa juu ya maji.” Huko tumezungumzia kuwa makusudio ya Arshi ni miliki yake na utawala wake na kwamba maji yalikuwako kabla ya kuumbwa mbingu na ardhi.

Miongoni mwa kauli za Ahlu bayt (a.s.) ni kuwa maji ndio ya kwanza kuumbwa na Mwenyezi Mungu. Ikiwa elimu hivi leo haijaugundua uhakika huu, lakini inawezekana ikaugundua kesho ya karibu au ya mbali.

Amenukuu Abul-hayan Al-andalusi katika Bahrul-muhit, kwamba Hamid amesoma: ‘Tumejalia maji kuwa ni uhai wa kila kitu.’ Kisomo hiki kinatilia nguvu kuwa maji ndiyo yaliyoumbwa mwanzo na ndio chimbuko la kwanza la kila kitu, na kwamba kila kitu kina uhai, kiwe kinakua au hakikui hata kama kwa dhahiri kinaonekana kimeganda.

Je, hawaamini baada ya dalili zote hizi na ubainifu?

Na tukaweka katika ardhi milima ili isiwayumbishe. Na tukaweka humo upana wa njia ili wapate kuongoka.

Mahali pengine imesemwa:

لِتَسْلُكُوا مِنْهَا سُبُلًا فِجَاجًا {20}

“Ili mtembee humo katika njia pana” (71:20)

Imetangulizwa njia ndio ukaja upana. Maana yote nisawa.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameweka njia pana ardhini ili watu wazitumie kwenye makusudio yao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 14: (16:15).

Na tukaifanya mbingu kuwa sakafu iliyohifadhiwa, lakini wanazipuuza ishara.

Kuwa sakafu maana yake ni kama sakafu. Makusudio ya iliyohifadhiwa hapa ni kubakia sayari sehemu yake kwa nguvu ya mvutano. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

وَيُمْسِكُ السَّمَاءَ أَنْ تَقَعَ عَلَى الْأَرْضِ{65}

“Na anazizuia mbingu zisianguke juu ardhi.” (22:65).

Kuzuia kumetegemezwa kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye ndio sababu ya sababu zote. Maana ni kuwa nidhamu hii ya undani katika kuumba mbingu ni dalili mkataa, kwa wenye akili, ya kuweko muumbji, umoja wake, uweza wake, ujuzi na hekima yake. Lakini watu wengi wanazipinga ishara za Mwenyezi Mungu na dalili zake wakipondokea kwenye hawa zao na ladha zao.

Na Yeye ndiye aliyeumba usiku na mchana na jua na mwezi.

Kila kimoja kati ya usiku, mchana, jua na mwezi kina uhusiano mkubwa na binadamu. Mchana ni wa kujishughulisha, usiku ni wa kupumzika na kutulia, jua na mwezi ni kwa ajili ya mwanga, hisabu na faida nyinginezo. Hayo yote ni neema kubwa kwa waja Wake na nguvu ya hoja ya ukuu wa usultani Wake.

Kila kimoja katika anga vinaogoelea.

Kila sayari inazunguka kwa vipimo na harakati zinazooana nayo.

Unaweza kuuliza: Ikiwa tutakadiria kusema kila kimoja basi tungesema ‘kinaogelea,’ sasa kuna wajihi gani wa kusema vinaogelea?

Wafasiri wameleta majibu mengi, lenye nguvu zaidi ni lile linalosema: Kila moja kati ya mwezi na jua kina matilai yake na mashukio yake. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akarudisha dhamiri ya wingi kwa kuzingatia hayo.

Na hatukumjaalia mtu yeyote wa kabla yako kuishi milele. Je, ukifa wewe wao wataishi milelele?

Tabrasi amesema: “Washirikina wa kikuraishi waliposhindwa na Muhammad (s.a.w.) walisema tumngoje afe, ndipo ikashuka Aya hii kuwajibu kuwa hakuna yeyote atakayeokoka na mauti. Je, mtume akifa nyinyi washirikina hamtakufa? Mfumo wa Aya haukatai aliyoyasema Tabrasi.

Kila nafsi itaonja mauti.

Hakuna wa kuyakimbia mauti. Mauti mazuri ni yale ya kufa shahidi kwa ajili ya kuitafuta haki na kuibatilisha batili.

Na tutawajaribu kwa mtihani wa shari na kheri na kwetu mtarejeshwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) huwapa mtihani waja wake kwa wanayoyapenda na wanayoyachukia, ili idhihiri hakika ya kila mtu. Yule atakayeshukuru wakati wa raha, akavumilia wakati wa shida, basi huyo ni katika waumini wenye ikhlasi na atakuwa na malipo ya thawabu. Na yule mwenye kukufuru na akajivuna, basi huyo ni katika wale waliothibitikiwa na adhabu.

Inasemekana kuwa Amirul-mu’minin, Ali, aliugua. Wenzake wakaja kumtazama na wakamuuliza: “Vipi hali yako ewe Amirul-muminin?” Akasema: “Ni shari tu.” Wakasema: “Maneno haya hayasemwi na mtu mfano wako!”

Akasema: “Mwenyezi Mungu anasema: Na tutawajaribu kwa mtihani wa shari na kheri. Kwa hiyo kheri ni afya na kujitosheleza na shari ni ufukara na ugonjwa.”

Pia Amirul-muminin amesema: “Ambaye dunia yake itamnyookea na asijue kuwa anafanyiwa vitimbi, basi imedanganyika akili yake.” Neno mtihani katika Aya ni kutilia mkazo neno tutawajaribu.

Na wanapokuona wale ambao wamekufuru hawakufanyii ila mzaha: “Je, huyu ndiye anayewataja miungu wenu?.Na hao ndio wanaokataa dhikri ya Mwingi wa rehema.

Wamemkataa Mwenyezi Mungu wakaamini mawe. Mtume akawaita kwenye imani ya Mwenyezi Mungu mmoja aliye peke yake na waachane na mawe.

Lakini wakamfanyia masikhara yeye na mwito wake wa haki iliyo wazi, kwamba masanamu yao na mawe yao hayadhuru wala hayanufaishi.

Baadhi yao wamesema: “Hili ni jambo la ajabu kabisa.” Lakini hakuna ajabu, hii ni kawaida ya kila ambaye amechotwa na manufaa na masilahi ya kibinafsi na akakua katika malezi ya kuiga mazingira, mababa na mababu; ni sawa uigizaji huo uwe ni wa kuabudu mawe au kung’ang’ania rai bila ya elimu wala muongozo. Na nisawa malengo yawe ni mali au jaha. Wote hali moja.

خُلِقَ الْإِنْسَانُ مِنْ عَجَلٍ ۚ سَأُرِيكُمْ آيَاتِي فَلَا تَسْتَعْجِلُونِ {37}

Mtu amaeumbwa na haraka. Nitawaonyesha ishara zangu, basi msiniharakishe.

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَٰذَا الْوَعْدُ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {38}

Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

لَوْ يَعْلَمُ الَّذِينَ كَفَرُوا حِينَ لَا يَكُفُّونَ عَنْ وُجُوهِهِمُ النَّارَ وَلَا عَنْ ظُهُورِهِمْ وَلَا هُمْ يُنْصَرُونَ {39}

Lau wangelijua wale ambao wamekufuru wakati ambao hawatauzuia moto na nyuso zao wala migongo yao na wala hawatanusuriwa.

بَلْ تَأْتِيهِمْ بَغْتَةً فَتَبْهَتُهُمْ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ رَدَّهَا وَلَا هُمْ يُنْظَرُونَ {40}

Bali kitawafikia ghafla, na kitawashtua na wala hawataweza kukirudisha wala hawatapewa muda.

وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِنْ قَبْلِكَ فَحَاقَ بِالَّذِينَ سَخِرُوا مِنْهُمْ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ {41}

Na hakika walifanyiwa stihzai Mitume kabla yako, kwa hiyo yakawazinga wale waliofanya miongoni mwao yale waliyokuwa wakiyafanyia sthizai.

قُلْ مَنْ يَكْلَؤُكُمْ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ مِنَ الرَّحْمَٰنِ ۗ بَلْ هُمْ عَنْ ذِكْرِ رَبِّهِمْ مُعْرِضُونَ {42}

Sema ni nani atakayewalinda usiku na mchana na Mwingi wa rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao.

أَمْ لَهُمْ آلِهَةٌ تَمْنَعُهُمْ مِنْ دُونِنَا ۚ لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَ أَنْفُسِهِمْ وَلَا هُمْ مِنَّا يُصْحَبُونَ {43}

Au wao wana miungu watakaoweza kuwakinga nasi. Hao hawawezi kujinusuru wala hawatahifadhiwa nasi.

بَلْ مَتَّعْنَا هَٰؤُلَاءِ وَآبَاءَهُمْ حَتَّىٰ طَالَ عَلَيْهِمُ الْعُمُرُ ۗ أَفَلَا يَرَوْنَ أَنَّا نَأْتِي الْأَرْضَ نَنْقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَا ۚ أَفَهُمُ الْغَالِبُونَ {44}

Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu. Je, hawaoni kuwa tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake; basi je, hao ni wenye kushinda?