read

Aya 36 -37: Ngamia Wanono

Maana

Na ngamia wa kunona tumewafanyia kuwa ni miongoni mwa nembo za Mwenyezi Mungu, kwao mna kheri.

Neno ‘Budna’ ni ngamia hasa; kama ilivyoelezwa katika Tafsiri Razi, na Baydhawi. Hufananishwa naye ng’ombe katika hukumu si katika jina.

Hali yoyote iwayo, mtu ni natija ya mambo mengi, yakiwemo mazingira anayoishi. Waarabu, kwa karne nyingi, wakati wa jahiliya na baadaye, wameishi pamoja na ngamia na alikuwa ni sehemu ya maisha yao; wakila nyama yake, kunywa maziwa yake , kuvaa manyoya yake, kubebea mizigo kutoka mji mmoja hadi mwingine n.k. Tazama Juz. 14 (16: 6).

Kwa ajili hii ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamtaja kwenye Aya kadha, kwa tamko la kiujumla; kama vile wanyama howa, au kwa tamko mahususi; kama ilivyo katika Sura 88 na hii Aya tuliyo nayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaneemesha waja wake kwa ngamia na akamfanya ana manufaa mengi; yakiwemo kujikurubisha mja kwa Mwenyezi Mungu kwa kumchinja katika nyumba yake takatifu. Kuleta ibara ya nembo kwa dhabihu hii ni kufahamaisha kuwa hiyo ni twaa na ibada bora zaidi.

Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanaposimama safu.

Katika masharti ya kuchinja ni kusoma Bismillah na kuelekezwa chinjo upande wa Qibla, na ngamia kuwa na aina yake ya kuchinjwa (nahr) ambayo ni maalum kwa ngamia:
Anachomwa kisu au kitu chochote chenye ncha kwenye maungio ya shingo na kifua, akiwa ngamia amesimama au kupiga magoti au amelala ubavu, kwa sharti ya kuwa sehemu zote za mbele ya mwili wake zielekee Qibla.

Njia bora ni kumchinja ngamia kwa namna ilivyoelezwa katika Riwaya ambayo ni kusimamishwa ngamia na kufungwa mmoja wa miguu yake ya mbele na asimame mchinjaji kuelekea Qibla vile vile kisha amchome kwenye maungio ya shingo na kifua. Riwaya hii inaweza kufaa kuwa ni tafsiri ya neno ‘wanaposimama safu.’
Na wanapoanguka ubavu, yaani wanapoanguka chini na kukata roho, basi kuleni na mlisheni aliyekinai na aombaye.

Aliyekinai ni yule anayeridhia unachompa bila ya kuomba.Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mpate kushukuru.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewafanya wanyama tuwatumie, hata kuwachinja pia. Kwa hiyo ni wajibu wetu kushukuru.

Nyama zao hazimfikii wala damu zao.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosha na walimwengu, hawahitajii, sikwambii nyama zilizochinjwa na damu; bali haihitajii chochote. Imesemekana hii ni kuwarudi washirikina ambao walikuwa wakitapakaza damu ya dhabihu kwenye masanamu yao na kuta za Al-Kaaba.

Lakini inamfikia takua kutoka kwenu.

Unaweza kuuliza kuwa maana ya takua ni kumcha Mungu katika yale aliyoyaharamisha; ambapo thawabu yake na manufaa yake yanarudi na kumfikia mtendaji tu. Sasa nini maana ya kuwa inafika kwa Mungu?

Jibu: Makusudio ya takua hapa ni kumridhisha Mwenyezi Mungu, na radhi ya Mwenyezi Mungu haiepukani na mwenye takua, zinakwenda sambamba. Kwa hiyo maana ni kinachomfikia Mwenyezi Mungu katika dhabihu zenu ni kule kuridhiwa na Mungu sio kukasirikiwa. Inafanana na kumwambia mwanao: kufaulu kwako darasani kunanifanya ni kupende na kukuridhia, na haya ndiyo ninayoyapata kutokana na masomo na kufaulu kwako.

Kama hivyo tumewafanya hawa wawe dhalili kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyowaongoa.

Amewadhalilisha wanyama kwa waja wake na akawaongoza kujikurubisha kwake kwa kuwachinja ili wamsifu kwa sifa zake njema, wamuad- himishe kwa ujuzi wake na uweza wake, wahofie adhabu yake na kutumai thawabu zake.

Wabashirie wenye kufanya mema wote; wawe wamefanya mema kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuchinja au kwa jambo jinginelo. Kwani aina za wema hazina idadi. Bora zaidi ni kupigana jihadi na madhalimu na wapotevu japokuwa kwa tamko la haki na uadilifu.

إِنَّ اللَّهَ يُدَافِعُ عَنِ الَّذِينَ آمَنُوا ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ خَوَّانٍ كَفُورٍ {38}

Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini, mwenye kukufuru sana.

أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا ۚ وَإِنَّ اللَّهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ {39}

Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.

الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِنْ دِيَارِهِمْ بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّا أَنْ يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّهُ ۗ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّهِ النَّاسَ بَعْضَهُمْ بِبَعْضٍ لَهُدِّمَتْ صَوَامِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَاتٌ وَمَسَاجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا اسْمُ اللَّهِ كَثِيرًا ۗ وَلَيَنْصُرَنَّ اللَّهُ مَنْ يَنْصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ {40}

Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila tu kwa kuwa wanasema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu. Na lau Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu kwa watu, basi yangelivunjwa mahekalu na makanisa na (sehemu) za kuswalia na misikiti ambayo ndani yake hutajwa jina la Mwenyezi Mungu kwa wingi. Na hakika Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.

الَّذِينَ إِنْ مَكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنْكَرِ ۗ وَلِلَّهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ {41}

Wale ambao tukiwamakinisha katika ardhi husimamisha Swala na wakatoa Zaka na wakaamrisha mema na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.