read

Aya 37 – 44: Mtu Ameumbwa Na Haraka

Lugha

Kuna tofauti baina ya haraka na upesi upesi (chapuchapu). Haraka ni kufanya jambo kabla ya wakati wake. Upesi upesi ni kulifanya jambo mara tu unapofika wakati wake bila ya ngojangoja. Kulifanya jambo upesi upesi kunasifika. Mwenyezi Mungu anasema:

وَيُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَأُولَٰئِكَ مِنَ الصَّالِحِينَ {114}

Wanafanya upesiupeesi mambo ya kheri na hao ndio miongoni mwa watu wema.” Juz.4 (3:114)

Kuna kauli masuhuri isemayo: ‘Haraka inatokana na shetani1

Maana

Mtu amaeumbwa na haraka. Nitawaonyesha ishara zangu, basi msini- harakishe.

Mtume (s.a.w.) aliwahadharisha makafiri na matokeo ya ukafiri na akawahadharisha na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama wakiendelea, lakini walizidi kiburi na inadi. Wakafanya masikhara ya kuharakisha adhabu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawaambia, ngojeni mtaona ukweli wa Mtume wangu katika yale aliyowapa kiaga na akawahadharisha kuwa msiaharakie jambo ambalo litakuwa. Mara ngapi anayeharakia jambo likimfikia anatamani, lau lisingekuwa. Wafasiri wamesema, wakifafanua Aya hii, kuwa mtu ana maumbile ya kutaka haraka haraka, na kwamba hiyo iko katika mishipa yake na nyama yake.
Lakini kama ingelikuwa sawa hivyo, basi kusingepatikana utulivu wowote; bali kila mtu angelikuwa na haraka haraka katika kauli zake na vitendo vyake vyote, bila ya kubakia.

Ikiwa utamsifia mtu kwa haraka, kufuru au kukata tamaa n.k. utakuwa unafasiri silika yake katika baadhi ya hali zake, lakini sio kuwa ndio maumbile yake yote. Tumeyafafanua hayo kwa urefu, katika Juz. 12 (11:9) na Juz. 13 (14: 34).

Na wanasema: “Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 ( 7:70), Juz. 9 (7:107) na Juz. 12 (11: 32).

Lau wangelijua wale ambao wamekufuru wakati ambao hawatauzuia moto na nyuso zao wala migongo yao na wala hawatanusuriwa.

Makafiri wanaharakia adhabu na wao ni wadhaifu na wako duni kuweza kuizuia au kuweza kuikimbia. Watawezaje, nayo itawagubika kutoka juu yao hadi chini na mbele yao hadi nyuma?

Bali kitawafikia ghafla, na kitawashtua na wala hawataweza kukirudisha wala hawatapewa muda.

Kitakachowafikia ghafla ni Kiyama. Hakuna shaka kuwa kitawajia ghafla bila ya onyo lolote. Hiyo inatokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِنْدَ اللَّهِ ۚ {63}

Wanakuuliza kuhusu saa (ya Kiyama). Sema hakika elimu yake iko kwa Mwenyezi Mungu tu.” (33:63).

Ikiwa kitakuja kwa hali hii basi ni lazima kilete mshtuko na mashangao. Kwa hiyo hawataweza kukizuia wala hakitawapa muda wa kupanga mambo yao.

Na hakika walifanyiwa stihzai Mitume kabla yako, kwa hiyo ya kawazinga wale waliofanya miongoni mwao yale waliyokuwa wakiyafanyia sthizai.

Imetangulia Aya hii katika Juz. 7 (6:10).

Sema, ni nani atakayewalinda usiku na mchana na Mwingi wa rehema.

Kadiri mtu atakavyochukua hadhari na kujificha hawezi kujilinda na mambo ya ghafla, isipokuwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na tawfiki yake. Anawezaje kujilinda mtu na uwezo wa Mungu?

Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao.

Waliwafanyia sthizai Mitume wa Mwenyezi Mungu, wakajiaminisha na adhabu ya Mwenyezi Mungu na wakapuuza dhikri ya Mwenyezi Mungu; kwa nini? Kwa sababu wako kwenye starehe, wakiiona kuwa hiyo ni ngome ya kujihifadhi.

Au wao wana miungu watakaoweza kuwakinga nasi, kutokana na adhabu yetu tukitaka kuwaangamiza na kuwang’oa?

Hao hawawezi kujinusuru wala hawatahifadhiwa nasi.

Hao ni hao miungu wao. Kwa maana kwamba washirikina wanataka hifad- hi kwa masanamu, wakati hayo yenyewe hayawezi kujisaidia, hayawezi kujinufaisha na chochote, yatawezaje kumsaidia mwingine?

Katika Tafsirut-tabari imeelezwa kuwa watu wa taawili wametofautiana katika neno yusbihun. Baada ya kunukuu kauli kadhaa, alichagua maana ya kuhifadhiwa. Maana haya ndiyo yanayoafikiana na kauli yake Mwenyezi Mungu katika (23:88).

Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu.

Mwenyezi Mungu amewapa muda na maisha wakaghurika na muda wakawa wajeuri na wabaya; hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anawangoja na anawavuta polepole bila ya kujijua.

Je, hawaoni kuwa tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake. Basi je, hao ni wenye kushinda?

ImetanguliapamojanatafsiriyakekatikaJuz.13:(13:41).

قُلْ إِنَّمَا أُنْذِرُكُمْ بِالْوَحْيِ ۚ وَلَا يَسْمَعُ الصُّمُّ الدُّعَاءَ إِذَا مَا يُنْذَرُونَ {45}

Sema: Hakika mimi ninawaonya kwa wahyi tu. Na viziwi hawasikii mwito wanapoonywa.

وَلَئِنْ مَسَّتْهُمْ نَفْحَةٌ مِنْ عَذَابِ رَبِّكَ لَيَقُولُنَّ يَا وَيْلَنَا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ {46}

Na watakapoguswa na mpulizo mmoja wa adhabu itokayo kwa Mola wako, bila shaka watasema: Ole wetu! Hakika tulikuwa ni wenye kudhulumu.

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِنْ كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ {47}

Na tutaweka mizani ya uadilifu kwa siku ya Kiyama. Basi nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu. Hata ikiwa ni chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa wenye kuhisabu.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَىٰ وَهَارُونَ الْفُرْقَانَ وَضِيَاءً وَذِكْرًا لِلْمُتَّقِينَ {48}

Na hakika tulimpa Musa na Harun, upambanuzi, mwangaza na ukumbusho kwa wenye takua.

الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ بِالْغَيْبِ وَهُمْ مِنَ السَّاعَةِ مُشْفِقُونَ {49}

Ambao humwogopa Mola wao faraghani na wanaiogopa saa (ya Kiyama).

وَهَٰذَا ذِكْرٌ مُبَارَكٌ أَنْزَلْنَاهُ ۚ أَفَأَنْتُمْ لَهُ مُنْكِرُونَ {50}

Na huu ni ukumbusho uliobarikiwa ulioteremshwa. Basi je, mnaukataa?
  • 1. Waswahili nao wana misemo: ‘Haraka haraka haina baraka’ -Mtarjumu