read

Aya 38 – 41: Mwenyezi Mungu Huwakinga Walioamini

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini mwenye kukufuru sana.

Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anazuia ukafiri na utaghuti kwa waumini katika maisha haya na siku ya mwisho. Aya iliyo wazi zaidi katika hilo ni: “Hakika bila shaka tutawanusuru Mitume wetu na walioamini katika uhai wa duniani na siku watakaposimama mashahidi.” (40:51).

Pamoja na hayo Mwenyezi Mungu ameashiria kwenye Aya kadhaa, kwamba mayahudi walikuwa wakiwaua manabii bila ya haki. Miongoni mwazo ni: Juz.3 (3: 21), Juz. 4 (3:112, 181) na Juz 6 (4:154). Kuongezea Historia ya mwanadamu, tangu zamani na sasa, imejaa dhulma na kufanyiwa uadui wale wenye takua na ikhlasi.

Sasa je, kuna wajihi wa kukusanya baina ya zinazofahamisha kuuliwa watu wema na zile zinazofahamisha kunusuriwa watu wa haki?

Jibu: Kwanza: Aya za nusra zinawahusu baadhi ya mitume; kama vile: Nuh, Hud, Swaleh, Lut na Muhammad. Hayo yanaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na Mwenyezi Mungu humuunga mkono kwa nusra yake amtakaye.” Juz.3 (3:13).

Na Aya hii tuliyo nayo inafahamisha kuwa Muhammad (s.a.w.) na maswahaba ndio wanokusudiwa kwenye kauli yake ‘Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamni.’ Kwa sababu wao ndio waliotolewa majumbani mwao si kwa lolote ila ni kwa kuwa wamesema: ‘Mola wetu ni Mwenyezi Mungu.”

Katika vitabu vya Hadith (As-sihah) imeelezwa kwamba Aya hizi zilishuka wakati Mtume alipofanya hijra (kuhama) kutoka Makka kwenda Madina.

Pili: Mwenye haki na ikhlasi hawezi kukosa wa kumuunga mkono na kumsaidia kwa mkono wake, mali yake au ulimi wake. Wala hatujawahi kusikia jamii ambayo kwa pamoja imekuwa dhidi ya mwenye kutamka tamko la haki na uadilifu.

Ndio, ni kweli kwamba watetezi wa haki wengi wameuawa, wakatekwa na wakafukuzwa, lakini Mwenyezi Mungu anawapa wasaidizi wanotangaza misimamo yao na kuwatukuza na wakiwakabili maadui zao kwa hoja na dalii mkataa. Hii ni aina ya nusra. Kusema kwake Mwenyezi Mungu: ‘Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini’ ni sababu ya kauli yake: ‘Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamni.’

Sababu hii inafahamisha kuwa ni wajibu kwa anayemwamini Mwenyezi Mungu kumsaidia mumin kwa kila alichonacho kinachoweza kumsaidia, angalau kumtetea anapotajwa kwa ubaya; vinginevyo atakuwa ni mhaini mwingi wa kukanusha. Kuna Hadith sahih isemayo: “ Mwenye kuinyamazia haki ni shetani bubu.

Tatu: Lau ingekuwa mtu akiamini tu, basi anaondokewa na muadui na matatizo, basi wangeliamini watu wote imani ya kibiashara; kama vile anayeiuza dhamiri yake kwa kila mwenye kutoa thamani.

Nne: Imani ya haki ni kumtii Mwenyezi Mungu katika maamrisho yake na hukumu zake zote. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametuamrisha, tukitaka kufanya jambo, tufuate sababu za kimaumbile ambazo amezifanya zitekeleze matakwa yetu. Ameziweka sababu za ushindi kuwa ni umoja na kuandaa nguvu, akasema: “Wala msizozane, msije mkavunjika moyo na zikapotea nguvu zenu.” Na akasema: “Na waandalieni nguvu vile muwezavyo.” Juz. 10 (8: 46, 60).

Katika Futuhatul-Mkkiya, Ibnul A’arabiy ameziletea sababu hizi ibara ya mkono wa Mungu. Ameichukua ibara hii katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Je, hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono yetu wanyama wa mifugo wakawa wenye kuwamiliki.” (36:71). Tazama maelezo kwa anuani ya ‘Dini haioteshi ngano’ katika Juz.3 (8: 1-4).

Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.

Waislamu kule Makka walikuwa ni wanyonge, wakipata kila aina ya maudhi na ukandamizwaji kutoka kwa washirikina; na walikuwa hawawezi kujitetetea. Walikuwa wakimjia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na wakimshitakia dhulma, naye akiwa hana lolote la kuwaambia isipokuwa kuwausia subra. Miongoni mwa aliyokuwa akiwaambia ni: “Mimi sijaamriwa kupigana.”

Mtume alikatazwa kupigana na washirikina katika zaidi ya Aya 70, alipokuwa Makka. kwa sababu kupigana wakati huo ilikuwa ni sawa na kujimaliza. Tazama Juz.5 (4:77).

Baada ya Mtume na Waislamu kuhamia Madina, wakawa na nguvu, ndipo ikashuka Aya hii. Inasemekana kuwa ndio Aya ya kwanza kushuka kuhu- siana na vita.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebainisha sababu ya kutoa ruhusa hii; kwamba washirikina wamewachokoza waislamu, wakawatoa kwenye miji yao kwa dhulma na kwa uadui na akawaahidi waislamu ushindi kwa maadui zao, pale aliposema: “Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.”

Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa kosa pekee la Mtume na swahaba zake kwa washirikina ni kule kusema: “Hakuna Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu.” Dhahiri hii ndio walioichukua wafasiri wote; bali mmoja wa wafasiri wapya alisema, ninamnukuu: “Hakuna upinzani kuliko kupinga maisha haya yaliyojikita kwenye tamaa, kupingana masilahi, kutofautiana mielekeo na kugongana matamanio.”

Mara nyingi tumeashiria huko nyuma kwamba utaghuti wa kishirikina uli- upiga vita ujumbe wa Muhammad na neno la Tawhid si kwa lolote isipokuwa linataka kuondoa manufaa, matamanio, masilahi yao na kuwe- ka usawa baina ya watu. Angalia tuliyoyaandika kwa anuani ya ‘Masilahi ndio sababu’ katika Juz. 1 (2: 92-96).

Na lau Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu kwa watu, basi yangelivunjwa mahekalu na makanisa na (sehemu) za kuswalia na misikiti ambayo ndani yake hutajwa jina la Mwenyezi Mungu kwa wingi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwaruhusu waumini, wanaochokozwa, kupigana na washirikina, sasa anabainisha sababu ya ruhusa hiyo; kwamba lau si kuweko na nguvu ya upinzani, basi ingeenea vurugu na ufisadi katika ardhi kwa sababu ya unyang’nyi, uporaji na kumwagika damu; hasa baina ya vikundi na watu wa dini.

Mwenyezi Mungu ameielezea fitna baina ya mataifa kwa ibara ya kuvunjwa sehemu zake za kuabudu. Kwa sababu ndio sehemu muhimu kwa mataifa; na zina alama maalum zinazotofautiana na nyingine. Mahekalu ni ya mayahudi, makanisa ni ya wanaswara (wakiristo), na sehemu za kuswalia ni zamataifa mengineyo. Msikiti unatofautiana na sehemu nyingine kwa kuwa Swala humo ni mara tano, usiku na mchana.
Kundi la wafasiri wamesema kuwa makusudio ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu anawazuwiya waumini na makafiri. Kama itakuwa ni sawa tafsiri hiyo, haiwezi kufaa kila wakati. Usahihi hasa ni tuliouelezea, kuwa ili kuhifadhika amani na nidhamu ni lazima kuweko na nguvu ya upinzani; ni sawa nguvu hiyo iwe mikononi mwa waumini au makafiri.

Imam Ali (a.s.) anasema: “Hapana budi watu wawe na kiongozi mwema au muovu, atatumiwa na mumin na kafiri, Mwenyezi Mungu atafikisha kwaye muda. Watu watajikusanya kwake waweze kumpiga adui, nia zitakuwa na amani kwaye, mwenye nguvu atakamatwa kwa ajili ya kumuonea mnyonge ili astarehe na kila muovu.”

Kauli hii ya Imam Ali, ilikuwa ni kuwarudi Khawariji waliposema: “Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu.” Angalia tuliyoyaandika kwa anuani hii, kwenye Juz. 12 (12:40).

Na hakika Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.

Hiki ni kichocheo cha kupigana jihadi ya kuinusuru haki na watu wake.

Wale ambao tukiwamakinisha katika ardhi husimamisha Swala na wakatoa Zaka na wakaamrisha mema na wakakataza mabaya.

Makusudio ya kumakinishwa hapa ni utawala. Mwenyezi Mungu ameapa kwa msisitizo kwamba Yeye atawasaidia watawala, kwa sharti ya kuweko mambo mawili:

Kwanza, wao wenyewe watekeleze haki ya ibada kwa ukamilifu; kama vile Swala, Saumu na kuamrisha mema na kukataza maovu. Ibada ya kimwili ameileta kwa ibara ya Swala na ibada ya kimali kwa Zaka.

Jambo la pili, ni kufanya uadilifu baina ya watu, kuisimamisha haki na kuibatilisha batili. Hayo ndio makusudio ya kuamrisha mema na kukataza maovu. Akivunja moja tu ya mawili haya, Mwenyezi Mungu humpuuza na humwacha.

Unaweza kuuliza: Tumewaona watawala wengi wasiomwamini Mungu kabisa, sikwambii kumwabudu kwa kuswali na kutoa Zaka, lakini pamoja na hayo utawala wao umestawi na kufuatwa na raia kwa vile wametimiza malengo ya raia na kuwatumikia, wala raia hawaangalii imani yao. Kwa hiyo, inaonyesha, suala la imani sio sharti la kudumu utawala na ustawi wake?

Jibu: Makusudio ya nusra ya Mwenyezi Mungu, katika Aya, ni kuustawisha utawala katika dunia na thawabu za akhera; bali hii ndio nusra ya kiuhakika. Kwa sababu ufalme wa dunia unaondoka, lakini neema za akhera ni za kudumu bila ya kuwa na ukomo na ni msafi na wa raha kwa pande zake zote.
Mtawala wa dunia anaweza kuustawisha utawala wake duniani akiwa mwadilifu, lakini Akhera akapata adhabu ya kuungua kwa kukufuru kwake dalili za kilimwengu ambazo zinaonyesha kuweko mtengenezaji.

Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.

Yeye peke yake ndio Mfalme wa wafalme, huumpa ufalme amtakaye na humnyima ufalme amtakaye, na yeye ni Muweza wa kila kitu.

وَإِنْ يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَعَادٌ وَثَمُودُ {42}

Wakikukadhibisha, basi wamekadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh na kina A’d na Thamud.

وَقَوْمُ إِبْرَاهِيمَ وَقَوْمُ لُوطٍ {43}

Na kaumu ya Ibrahim na kaumu ya Lut.

وَأَصْحَابُ مَدْيَنَ ۖ وَكُذِّبَ مُوسَىٰ فَأَمْلَيْتُ لِلْكَافِرِينَ ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ {44}

Na watu wa Madyan na Musa alikadhibishwa. Nikawapa muda makafiri kisha nikawatia mkononi, basi kulikuwaje kukanya kwangu?

فَكَأَيِّنْ مِنْ قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ فَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَبِئْرٍ مُعَطَّلَةٍ وَقَصْرٍ مَشِيدٍ {45}

Na miji mingapi tuliyoiangamiza iliyokuwa ikidhulumu. Ikaangukiana mapaa yake na visima vilivyoachwa na makasri yaliyo madhubuti?

أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌ يَعْقِلُونَ بِهَا أَوْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا ۖ فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَٰكِنْ تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ {46}

Je, hawatembei katika ardhi ili wapate akili za kuzingatia na masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.

وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَلَنْ يُخْلِفَ اللَّهُ وَعْدَهُ ۚ وَإِنَّ يَوْمًا عِنْدَ رَبِّكَ كَأَلْفِ سَنَةٍ مِمَّا تَعُدُّونَ {47}

Wanakuharakisha ulete adhabu na hakika Mwenyezi Mungu hakhalifu miadi yake. Na hakika siku moja kwa Mola wako ni kama miaka elfu mnavyohisabu.

وَكَأَيِّنْ مِنْ قَرْيَةٍ أَمْلَيْتُ لَهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ ثُمَّ أَخَذْتُهَا وَإِلَيَّ الْمَصِيرُ {48}

Ni miji mingapi nimeipa muda na hali ilikuwa imedhu- lumu, kisha nikaitia mkononi? Na kwangu mimi ndio marejeo yote.

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّمَا أَنَا لَكُمْ نَذِيرٌ مُبِينٌ {49}

Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni muonyaji kwenu niliye dhahiri.

فَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ مَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ {50}

Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watapata maghufira na riziki za heshima.

وَالَّذِينَ سَعَوْا فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ {51}

Na wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa motoni