read

Aya 42 -51: Wakikukadhabisha

Maana

Wakikukadhibisha, basi wamekadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh na kina A’d na Thamud na kaumu ya Ibrahim na kaumu ya Lut na watu wa Madyan na Musa alikadhibishwa.

Makuraishi walimkadhibisha Muhammad (s.a.w.) na wakamtoa nyumbani kwake, Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake, kwa kumtuliza na kumpoza moyo, kwamba hakuna la ajabu katika yanayokutokea. Kila Nabii alipambana na hayo uliyopamabana nayo.

Kisha akamtajia idadi ya manabii, kwa njia ya mfano tu; akiwemo Hud na watu wake walioitwa A’d, Swaleh na watu wake walioitwa Thamud. Ama watu wa Madyana hao ni watu wa Shuayb. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:34).

Nikawapa muda makafiri kisha nikawatia mkononi, basi kulikuwaje kukanya kwangu?

Makusudio ya kukanya hapa ni adhabu, kwa maana ya kukanya kwa vitendo sio kwa maneno. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwacheleweshea makafiri adhabu mpaka ulipofika muda wake, akawapatiliza kwa upatilizo wa mwenye uweza asiyeshindwa. Aya inaashiria kwamba mwenye akili hatakikani kuharakisha mambo kabla ya kufikia muda wake.

Na miji mingapai tuliyoiangamiza iliyokuwa ikidhulumu.

Baada ya Mwenyezi Mungu kusema kuwa anawapa muda makafiri mpaka wakati maalum, sasa anaishiria kuangamia kwa miji ambayo watu wake wamedhulumu, ambayo ni mingi, kama inavyoashiria kauli yake: ‘Miji mingapi?’ Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:4).

Ikaangukiana mapaa yake?

Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (2:259) na Juz. 15 (18:42).

Na visima vilivyoachwa na makasri yaliyo madhubuti.

Yote haya yameachwa bila watu; yaani miji ya madhalimu imekuwa mahame, haina watu, ambapo hapo zamani ilikuwa imesheheni wenyeji na wageni wanaoitembelea.

Je, hawatemebei katika ardhi ili wapate akili za kuzingatia na masikio ya kusikilia?

Wanaambiwa wale waliomkadhibisha Muhammad (s.a.w.). Yaani hawapati funzo kwa waliyowafikia wakadhibishaji na kuona jinsi miji yao ilivyokuwa mitupu? Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:137) na Juz. 14 (16: 36).

Kwani hakika si macho yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.

Kuna faida gani ya kusikia na kuona ikiwa moyo umepofuka? Kwa sababu masikio na macho ni nyenzo na akili ndio asili.

Wanakuharakisha ulete adhabu.

Wanaohimiza ni washirikana na anayehimizwa ni Muhammad (s.a.w.). Mtume alikuwa akiwapa kiaga cha adhabu ikiwa watang’ang’ania ushirikina.

Walikuwa wakisema yale waliyosema waliowatangulia kuwaambia mitume kila wanapowakataza ushirikina: “Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni mkweli.”

Na hakika Mwenyezi Mungu hakhalifu miadi yake.

Kuharakisha au kuchelewesha si muhimu madamu ahadi itakuwa. Kuwa hakika ni kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwapa thawabu watiifu ni haki ya wale watiifu, hawezi kuihalifu.

Ama ahadi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ya adhabu kwa waasi, hiyo ni haki yake Mwenyezi Mungu, akitaka anaweza kuitekeleza na akipenda anaweza kusamehe, ila ikiwa imetanguliwa na neno ‘Hatahalifu’ kama ilivyo katika Aya hii tuliyo nayo; ambapo amekanusha kutotekeleza aliyowaahidi makuraishi kutokana na msimamo wao kwa Mtume wa rehema.

Na hakika siku moja kwa Mola wako ni kama miaka elfu mnavyohis- abu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaambia washirikina; kuna haja gani ya kuharakisha adhabu ya Akhera na siku moja kwake ni kali kwenu kuliko adhabu ya miaka elfu katika miaka ya kiduniani? Kwa ufupi ni kuwa miaka elfu ni fumbo la vituko vya siku ya mwisho.

Ni miji mingapi nimeipa muda na hali ilikuwa imedhulumu, kisha nikaitia mkononi? Na kwangu mimi ndio marejeo yote.
Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii na Sura hii tuliyo nayo Aya 45 na pia sehemu hii tuliyo nayo. Mwenyezi Mungu amerudia kwa kusisitiza na kutoa hadhari.

Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni muonyaji kwenu niliye dhahiri.

Huu ndio umuhimu wa mitume, kufikisha ujumbe na kutoa onyo kwa yule mwenye kuupinga. Maana haya yamekaririka kwa mifumo mbalimbali.

Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watapata maghufira na riziki za heshima.

Maana yako wazi, na yametangulia kwenye Aya kadha, ikiwemo Juz. 1 (2:25).

Na wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa motoni.

Yaani washirikina wataingia motoni kwa muda usiokuwa na ukomo kwa sababu ya kumfanyia inadi Mtume na kujitahidi kumpinga kufikisha ujumbe wa Mola wake na kuwazuilia nao watu.

وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ قَبْلِكَ مِنْ رَسُولٍ وَلَا نَبِيٍّ إِلَّا إِذَا تَمَنَّىٰ أَلْقَى الشَّيْطَانُ فِي أُمْنِيَّتِهِ فَيَنْسَخُ اللَّهُ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ ثُمَّ يُحْكِمُ اللَّهُ آيَاتِهِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {52}

Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii anaposoma ila shetani hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayoyatumbukiza shetani; kisha Mwenyezi Mungu huzi- makinisha Aya zake na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, mwenye hekima.

لِيَجْعَلَ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ فِتْنَةً لِلَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ وَالْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَفِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ {53}

Ili alifanye lile alilolitumbu iza shetani ni mtihani kwa wale wenye maradhi katika nyoyo zao na wale ambao nyoyo zao zimesusuwaa. Na hakika madhalimu wamo katika uasi wa mbali.

وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكَ فَيُؤْمِنُوا بِهِ فَتُخْبِتَ لَهُ قُلُوبُهُمْ ۗ وَإِنَّ اللَّهَ لَهَادِ الَّذِينَ آمَنُوا إِلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ {54}

Ili wajue wale ambao wamepewa elimu kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wako na zinyenyekee kwake nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye awaongozaye wale ambao wameamini kwenye njia iliyonyooka.

وَلَا يَزَالُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي مِرْيَةٍ مِنْهُ حَتَّىٰ تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً أَوْ يَأْتِيَهُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَقِيمٍ {55}

Na wale ambao wamekufuru hawataacha kuwa katika wasiwasi katika hilo mpaka saa iwafikie ghafla au iwafikie adhabu ya siku tasa.

الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ لِلَّهِ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ ۚ فَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ {56}

Ufalme siku hiyo ni wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina yao. Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watakuwa katika Bustani zenye neema.

وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَأُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُهِينٌ {57}

Na wale ambao wamekufuru na wakazikadhibisha ishara zetu watapata adhabu ifedheheshayo.