read

Aya 45 – 50: Nawaonya Kwa Wahyi

Maana

Sema: Hakika mimi ninawaonya kwa wahyi tu. Na viziwi hawasikii mwito wanapoonywa.

Aya hii ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَقُلْ إِنِّي أَنَا النَّذِيرُ الْمُبِينُ {89}

“Na, sema: Hakika mimi ni muonyaji niliye dhahiri.” Juz. 14 (15:89).

Mwenyezi Mungu anamwamrisha Mtume wake mtukufu awaambie washirikina kuwa mnakifanyia masikhara Kiyama na vituko vyake na habari hiyo ni wahyi wa Mwenyezi Mungu sio mawazo au njozi. Mimi nawahadharisha kwa amri ya Mwenyezi Mungu sio kwa amri yangu. Lakini mtawezaji kusikia hadhari na maonyo na kwenye masiko yenu kuna uziwi.
Kila asiyeitikia nasaha za Mwenyezi Mungu basi huyo ni kipofu na kizizwi, hata kama ana macho na masikio.

Na watakapoguswa na mpulizo mmoja wa adhabu itokayo kwa Mola wako, bila shaka watasema: “Ole wetu! Hakika tulikuwa ni wenye kudhulumu.

Hapo mwanzo walikuwa wanapoonywa kwa adhabu, wakifanya masikhara na mizaha, lakini itakapowagusa kidogo tu wataanza kulalamika na kunyenyekea huku wakisema: ‘Ole wetu sisi tulikuwa madhalimu.’ Umetangulia mfano wake katika sura hii Aya 14.

Mizani Siku Ya Kiyama

Na tutaweka mizani ya uadilifu kwa siku ya Kiyama. Basi nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu. Hata ikiwa ni chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa wenye kuhisabu.

Makusudio ya mizani hapa ni hukumu ya Mwenyezi Mungu na sharia yake. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anapima matendo ya waja kwa amri zake na makatazo yake. Ambaye atafanya matendo yake kulinga na na amri na makatazo yake, basi ni katika ambao mizani zao zitakuwa nzito.

Imam Jafar As-Sadiq (a.s.) aliulizwa kuhusu mizani za uadilifu, akasema ni manabii wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake; yaani hukumu za Mwenyezi Mungu zinazofikishwa na mitume na mawalii katika waja wake.

Malipo yatakuwa kulingana na misingi hii; hazitapunguzwa thawabu za mwema hata chembe, pengine inawezekana kuzidishwa. Wala haitazidishwa adhabu ya muovu hata chembe, pengine inawezekana kupunguzwa.

Nasi tunatosha kuwa wenye kuhisabu, hatutaziki wala hakitupiti kitu kadiri idadi yake itakavyokuwa.

Mulla Sadra katika Kitabu Al-asfar anasema: “Uwezo wa Mwenyezi Mungu unafichua matendo yote ya waja wake na kipimo cha mema yao, maovu yao na thawabu zake na adhabu yake katika kitambo kidogo, naye ni mwepesi wa kuhisabu”

Kama ataizingatia Aya hii, mwenye kujaribu kuifuatishia Qur’an na sayansi, atasema kianzio cha fikra ya akili ya mashine ni Qur’an. Angalia kifungu cha ‘Qur’an na sayansi’ katika mwanzo wa Juzuu ya kwanza.

Mwenye Al-Asfar amezungumzia kwa urefu kuhusu mizani ya siku ya Kiyama. Kwa kuangalia uwezo wa mtungaji katika falsafa ya itikadi n.k. Tutachukukua baadhi ya ibara zake, kama ifuatavyo, pamoja na nyongeza kidogo kwa ajili ya ufafanuzi:

“Mizani ya Akhera ni ile ambayo hujulikana kwayo usahihi wa elimu, imani ya Mungu, sifa zake, vitendo vyake, malaika wake, mitume wake, vitabu vyake na siku ya mwisho.

Mizani hii ni Qur’an ambayo ameiteremsha mwalimu wa kwanza, ambaye ni Mwenyezi Mungu, kwa mwalimu wa tatu, ambaye ni Mtume, kupita kwa mwalimu wa pili ambaye ni Jibril.

Kwa hukumu ya Qur’an ndio hupimwa elimu ya mtu, akili yake, kauli na vitendo vyake vyote. Vile vile hujulikana mema yake na maovu yake. Ikiwa wema utazidi basi mwenyewe atakuwa ni katika wema na ikiwa uovu utazidi basi atakuwa katika waovu.

Ikiwa mema na maovu yatalingana, basi mwenyewe atangojea mpaka Mungu amuhukumie adhabu au msamaha, lakini upande wa hurumma ndio ulio na nguvu zaidi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu”

Kisha akasema - mweneye Al-asfar – mahali pengine: “Kila kitu kina mizani isipokuwa neno: “Lailaha illa-llah, (Hapana Mola isipokuwa Allah) kwa sababu neno hilo la tawhid halina mkabala na jambo lolote isipokuwa shirk, na shirki haina mizani.”

Akaendelea kusema tena mahali pengine: “Hakika Qur’an ni kama meza yenye aina kwa aina ya vyakula, kuanzia vyakula halisi hadi maganda. Kile halisi ni hekima na dalili na kinahusika na wenye busara. Ama maganda ni ya walio mbumbumbu ambao ni kama wanyama; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

مَتَاعًا لَكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ {32}

“Kwa ajili ya manufaa yenu na wanyama wenu. (80:32).

Kwa haraka haraka mtu anaweza akadhani kuwa ibara ya maganda ni kukikosea adabu Kitabu cha Mwenyezi Mungu na utukufu wake, lakini mwenye Asfar yuko zaidi ya dhana na shakashaka. Mwenye kuyachunguza na kuyataamali maneno yake atajua kuwa makusudio ya maganda ni watu wa hayo maganda, kama wale wanaoganda kwenye dhahiri ya maneno bila ya kuangalia undani wake, hawaoni mbali zaidi ya pua zao, kwa dalili ya yale aliyoyaeleza alipokuwa akifafanua Hadith ya Mtume isemayo: “Qur’an ina dhahiri na batini.”

Hadith hii ameifafanua kwa maneno marefu; miongoni mwa maneno hayo ni haya yafutayo: “Hakika Qur’an ina daraja kama vile watu ambao wako wenye akili na wasiokuwa na akili. Asiye na akili ni kama yule anayechukua mambo kijujuu. Ama roho ya Qur’an na siri yake haigundui isipokuwa mwenye akili na busara. Kwa hiyo mgawanyiko unakuja kutokana na wanavyoifahamu Qur’an sio Qur’an yenyewe.

Na hakika tulimpa Musa na Harun, upambanuzi, mwangaza na ukumbusho kwa wenye takua.

Makusudio ya upambanuzi hapa ni Tawrat, kama alivyoiteremsha Mwenyezi Mungu kwa Musa. Kila Kitabu cha mbinguni ni upambanuzi, kwa sababu kinapambanua uongofu na upotevu, ni mwangaza wa kuondoa giza la ujinga na ukafiri na ukumbusho kwa mwenye kuitafuta takua, kwa sababu kina mkumbusha kuhusu Mwenyezi Mungu na kumbainishia halali na haramu.

Ambao humwogopa Mola wao faraghani na wanaiogopa saa (ya Kiyama).

Haya ndiyo maelezo ya wenye takua, kwamba wao wanamcha Mwenyezi Mungu kwa siri kusiko na watu; sawa na vile wanavyomcha dhahiri. Kwa vile wana imani siku ya Kiyama, hisabu na malipo, huku wakiiogopa siku hiyo na kuifanyia kazi.

Na huu ni ukumbusho uliobarikiwa ulioteremshwa.

Ni ukumbusho kwa mwenye kutaka kukumbuka, ni mawaidha kwa mwenye kuwaidhika na ni kheri kwa mwenye kuamrika na maarisho yake na kukatatiza kwa makatazo yake.

Basi je, mnaukataa?

Na hali hoja na dalili zake ziko wazi.

وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِنْ قَبْلُ وَكُنَّا بِهِ عَالِمِينَ {51}

Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uongofu wake zamani na tulikuwa tunamjua.

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا هَٰذِهِ التَّمَاثِيلُ الَّتِي أَنْتُمْ لَهَا عَاكِفُونَ {52}

Alipomwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayoyanga’ng’ania?

قَالُوا وَجَدْنَا آبَاءَنَا لَهَا عَابِدِينَ {53}

Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.

قَالَ لَقَدْ كُنْتُمْ أَنْتُمْ وَآبَاؤُكُمْ فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {54}

Akasema: Hakika nyinyi na baba zenu mmekuwa kwenye upotofu ulio dhahiri.

قَالُوا أَجِئْتَنَا بِالْحَقِّ أَمْ أَنْتَ مِنَ اللَّاعِبِينَ {55}

Wakasema: Je, umetujia kwa haki au wewe ni katika wafanyao mchezo?

قَالَ بَلْ رَبُّكُمْ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الَّذِي فَطَرَهُنَّ وَأَنَا عَلَىٰ ذَٰلِكُمْ مِنَ الشَّاهِدِينَ {56}

Akasema: Bali Mola wenu ni Mola wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliyeziumba, na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo.

وَتَاللَّهِ لَأَكِيدَنَّ أَصْنَامَكُمْ بَعْدَ أَنْ تُوَلُّوا مُدْبِرِينَ {57}

Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu baada ya kunipa mgogo.

فَجَعَلَهُمْ جُذَاذًا إِلَّا كَبِيرًا لَهُمْ لَعَلَّهُمْ إِلَيْهِ يَرْجِعُونَ {58}

Basi akayavunja vipande vipande isipokuwa kubwa lao ili wao walirudie.

قَالُوا مَنْ فَعَلَ هَٰذَا بِآلِهَتِنَا إِنَّهُ لَمِنَ الظَّالِمِينَ {59}

Wakasema: Ni nani aliyeyafanyia haya miungu wetu? Hakika huyu ni katika madhalimu.

قَالُوا سَمِعْنَا فَتًى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُ إِبْرَاهِيمُ {60}

Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.