read

Aya 52 -57: Kusoma Kwa Mtume Na Kujiingiza Shetani

Maana

Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii anaposoma ila shetani hutumbukiza katika masomo yake.

Wametofautiana wafasiri kuhusu neno Nabii na Mtume, (Nabiy na Rasul)1 kuwa je, ni ibara zenye maana moja au kila moja ina maana yake?

Kauli iliyo karibu zaidi ni ile isemayo kuwa hakuna tofauti baina yake; kwa vile kila mmoja kati yao anatanabahishwa na Mwenyezi Mungu kwa lile analolitaka. Kwa hiyo akitanabahishwa na kuamrishwa kufikisha yale aliyotanabahishwa, huyo anaitwa Nabii kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtanabahisha na pia anaitwa Mtume kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtumma kufikisha.

Ikiwa amemtanabahisha tu bila ya kumwamuru kufikisha, basi huyo atakuwa ni Nabii tu. Hiyo ni kusema kuwa kila Mtume ni Nabii, lakini sio kila Nabii ni Mtume.

Kuna riwaya inayosema kuwa sababu ya kushuka Aya hii ni kwamba Mtume (s.a.w.) aliwasomea makuraishi Sura Najm, alipofikia kwenye Aya isemayo:

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ {19}

وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ {20}

“Je, mmewaona Lata na Uzza na Manata mwingine wa tatu” (53: 19 20)

basi shetani aliingiza katika kisomo cha Mtume maneno haya: “Hao ni wazuri watukufu na kwamba maombezi yao bila shaka yanatarajiwa,” yani haya masanamu ni mazuri na uombezi wao unatarajiwa kwa Mwenyezi Mungu.

Maulama wahakiki wamekanusha riwaya hii na wakakata kauli kuwa hiyo ni miongoni mwa uzushi wa wazandiki wanaotaka kukitia ila Kitabu cha Mwenyezi Mungu na utume wa Muhammad (s.a.w.).

Wametegemea, katika hilo, kwenye dalili mkataa za kiakili na kinakili. Mtume ambaye ametumwa na Mwenyezi Mungu kupiga vita ushirikina na kuabudu mizimu, halafu huyo huyo arudi kuisifia kwa sifa za ukamilifu! Vipi iwe hivyo na ulimi wa Mtume unamtarjumu na kumbainisha Mwenyezi Mungu? Shetani anaweza kupata nafasi kwenye ubainifu na tafsiri hii ya kimungu?

Usahihi wa maana ya Aya ni kuwa ukomo wa usomaji wa Mtume yeyote, ni kuwafahamisha watu uhakika wa risala yake ili waweze kuifahamu na kuongoka nayo, lakini wenye tamaa wanaingilia kati kwa kuvungavunga na kueneza kila aina ya propaganda.

Haya tumeyashuhudia na kuyaona hasa. Haya ndio maana ya kutumbukiza shetani katika usomi wa Nabii. Nabii anawatakia heri watu na shetani muharibifu anawazuia wasiipate.

Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayoyatumbukiza shetani; kisha Mwenyezi Mungu huzimakinisha Aya zake na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, mwenye hekima.

Wabatilifu wanaunda njama na kuzitangaza, lakini Mwenyezi Mungu huondoa ubatilifu wao na kuufedhehi uwongo wao kwenye ndimi za wakweli na mikononi mwa wapigania jihadi. Aya nyingine yenye maana hii ni ile isemayo:

يُرِيدُونَ أَنْ يُطْفِئُوا نُورَ اللَّهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّهُ إِلَّا أَنْ يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ {32}

Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywavyao. Na Mwenyezi Mungu amekataa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wamechukia.” Juz.10 (9:32).

Ili alifanye lile alilolitumbukiza shetani ni mtihani kwa wale wenye maradhi katika nyoyo zao na wale ambao nyoyo zao zimesusuwaa.

Wenye maradhi katika nyoyo ni wezi wanaoishi kwa unyang’anyi, uporaji, ghushi na utapeli. Ama waliosusuwaa nyoyo zao ni wale ambao ni bendera hufuata upepo. Maana ni kuwa kampeni za uwongo hazina nafasi isipokuwa kwa wezi na walio na bendera.

Popote utakapoelekea utakuta picha hii waziwazi; hasa kwenye magazeti, idhaa, vitabu, michezo ya kuigiza na katika mazungumzo ya vibaraka na wale wanaodanganywa ambao wanaamini kila wanayoambiwa bila ya kuchunguza; tena ni wengi.

Kisha kampeni za uwongo, hata kama zitakuwa zina madhara kwa upande fulani, lakini zina manufaa kwa upande mwingine. Kwa sababu zinamtambulisha muhaini na mwenye ikhlasi, vile vile mjinga na mjuzi. Haya ndio makusudio ya neno mtihani.

Na hakika madhalimu wamo katika uasi wa mbali.

Kila mwenye kuvungavunga na akafanya uzushi basi ni dhalimu, na kila mwenye kuusadikisha uwongo na uzushi bila ya kuuchuunguza pia huyo ni dhalimu.

Ili wajue wale ambao wamepewa elimu kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wako na zinyenyekee kwake nyoyo zao.

Neno ‘hiyo’ hapa ni hiyo Qur’an. Pia inaweza kufasirika ‘huyo’ kwa maana ya huyo Nabii. Maana ni kuwa, ikiwa mtu atasadikisha uwongo juu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi wenye maarifa na ikhlasi, wanajua hakika ya uwongo na uzushi huo; jambo ambalo linawazidishia imani na mshikamano kwa Mwenyezi Mungu, mitume yake na vitabu vyake na pia unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu.

Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye awaongozaye wale ambao wameamini kwenye njia iliyonyooka.

Anawaongoza Mwenyezi Mungu kwenye njia yake na kuifuata kwa kujikurubisha kwake hata kukiwa na kampeni za uwongo na vikwazo kiasi gani.

Na wale ambao wamekufuru hawataacha kuwa katika wasiwasi kati- ka hilo mpaka saa iwafikie ghafla au iwafikie adhabu ya siku tasa.

Makusudio ya saa ni ile saa ya kutoka watu kuelekea kwa Mola wao wakitokea makaburini (Kiyama). Siku tasa ni siku ya hisabu. Utasa ni kinaya cha makafiri kukata tamaa ya kuokoka.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kueleza, katika Aya iliyotangulia, kuwa wenye elimu wanaamini Qur’an na utume wa Muhammad (s.a.w.), kwenye Aya hii anasema kuwa makafiri wako katika shaka kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu na watendelea kuwa katika shaka hiyo mpaka siku ya kufufuliwa kwao makaburini au siku ya kusimama kwao mbele ya Mwenyezi Mungu kwa hisabu.

Na hapo ndipo itawafichukia hakika yao na watajua kuwa wao walikuwa kwenye upotevu.

Ufalme siku hiyo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake, hakuna kadhi au amiri wala raisi au waziri; kama ilivyo katika maisha haya ya duniani. Atahukumu baina yao. Yaani baina ya makafiri na waumini.

Basi wale ambao wameamini na wakatenda mema, watakuwa katika Bustani zenye neema. Na wale ambao wamekufuru na wakazikadhibisha ishara zetu watapata adhabu ifedheheshayo.

Hawa watapata hizaya na moto na wale watapata Pepo na raha. Mfano wa Aya hizi umekwishatangulia mara nyingi.

وَالَّذِينَ هَاجَرُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ ثُمَّ قُتِلُوا أَوْ مَاتُوا لَيَرْزُقَنَّهُمُ اللَّهُ رِزْقًا حَسَنًا ۚ وَإِنَّ اللَّهَ لَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ {58}

Wale ambao wamehajiri katika njia ya Mwenyezi Mungu, kisha wakuawa au wakafa, bila shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mbora wa wanaoruzuku.

لَيُدْخِلَنَّهُمْ مُدْخَلًا يَرْضَوْنَهُ ۗ وَإِنَّ اللَّهَ لَعَلِيمٌ حَلِيمٌ {59}

Bila shaka atawaingiza mahali watakapoparidhia, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mpole.

ذَٰلِكَ وَمَنْ عَاقَبَ بِمِثْلِ مَا عُوقِبَ بِهِ ثُمَّ بُغِيَ عَلَيْهِ لَيَنْصُرَنَّهُ اللَّهُ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌ {60}

Ndivyo hivyo. Na anayelipiza mfano wa alivyoadhibiwa, kisha akadhulumiwa, bila shaka Mwenyezi Mungu atamnusuru. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Mwingi wa maghufira.

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّهَ يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَأَنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ {61}

Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huuingiza mchana katika usiku na huuingiza usiku katika mchana na kwamba Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia, mwenye kuona.

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِنْ دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ {62}

Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na kwamba wale wanaowaomba badala yake ni batili, na hakika Mwenyzi Mungu ndiye aliye juu, Mkubwa.

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ أَنْزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَتُصْبِحُ الْأَرْضُ مُخْضَرَّةً ۗ إِنَّ اللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ {63}

Je huoni kwamba Mwenyezi Mungu huteremsha maji kutoka mbinguni na mara ardhi inakuwa chanikiwiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye habari.

لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَإِنَّ اللَّهَ لَهُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ {64}

Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosha, Mwenye kusifiwa.
  • 1. Neno nabiy linamaana ya kutanabaishwa na rasul lina maana ya kutumwa - Mtarjumu.