read

Aya 61 – 70: Wakasema: Mleteni

Maana

Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia.

Walitaka wamsaili na kumhukumu mbele ya watu wamshuhudie; kisha waone adhabu itakayompata.

Wakasema: Je, wewe ndiwe uliyeifanyia haya mingu yetu ewe Ibrahim?

Walimleta na wakaanza kumhoji. Akasema:

Bali ameyafanya hayo mkubwa wao huyu. Basi waulizeni ikiwa wanatamka.
Kutamka ni katika hali ya kukadiria; ikiwa hawa wana hisia basi aliyefanya ni mkubwa wao. Mfano kusema: ikiwa Mwenyezi Mungu ana mtoto, basi mimi ni wa mwanzo wa wenye kumwabudu.

Kwa ujumla ni kwamba makusudio ni kuwanyamazisha kwa hoja, na kwamba masanamu haya, kama yangekuwa ni Mungu yangelikuwa na utambuzi, kusema na kumvunajilia mbali anayetaka kuyafanyia ubaya.

Basi wakajirudi nafsi zao.

Baada ya kusikia aliyoyasema Ibrahim (a.s.) waliulizana: Vipi tuabudu mawe na kutarajia kheri na kuhofia shari yake na hayo yenyewe hayawezi kujikinga na madhara.

Wakasema: Hakika nyinyi ndio madhalimu.

Waliishia kukiri kuwa wao wako katika ujinga, lakini mara tu wakarudia kwenye hali yao ya mwanzo.

Kisha wakasimamia vichwa vyao.

Makusudio ya kusimamia vichwa hapa ni kurudi kwenye uovu wao. Neno lililotumika ni nukisu lenye maana ya kuweka kichwa chini miguu juu. Yaani kumpa silaha adui yako akuue nayo, au kumpa hoja mtu kutokana na vitendo vyako au kauli yako; kama walivyofanya kaumu ya Ibrahim, waliposema:

Wewe unajua kwamba hawa hawasemi.

Ikiwa hawasemi, basi vipi mnawaabudu. At-Tabariy anasema: “Kupindua jambo ni kulifanya kichwa chini miguu juu na kupindua hoja ni kuifanya hoja ya hasimu wako ndio hoja yako; kama walivyofanya kaumu ya Ibrahim.”

Akasema: Basi nyinyi mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu visivyo wanufaisha kitu wala kuwadhuru?

Nyinyi mnajua kuwa haya masanamu hayana utambuzi wala matamshi, hayadhuru wala hayanufaishi, basi vipi mnayaabudu?

Kefule yenu na na mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Basi hamtii akili?

Utafanya nini na watu wanaong’ang’ania upotevu na wao wanajua kuwa huo ni upotevu. Hakuna cha kuwafanya isipokuwa kuwaaambia: poteleeni mbali, enyi mnaofanana na watu na wala sio watu.

Wakasema: Mchomeni na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo.

Wanusuruni miungu, lakini miungu yenyewe haiwezi kujinusuru, na bado ni miungu tu! Ni sawa na yule aliyesema: ‘Huyo ni paa hata kama ameruka angani.’ Huko ndiko kuweka kichwa chini miguu juu.

Tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!

Walisema na Mwenyezi Mungu naye akasema. Wala hakuna mwenye kurudisha kauli yake.

Unaweza kuuliza: Kwa kawaida moto unaunguza, vipi uwe baridi.

Jibu: Mwenye kuleta athari wa kwanza kwa kila kilichpo ni Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka ukuu wake. Yote hutokana na Yeye, na kwake zinaishia nyenzo zote, ziwe ni sharti, sababu au chochote. Kuunguza kunatokana na moto, moto unatokana na kuni, kuni ni maumbile yaliyotokana na neno lake.

Yeye ndiye aliyeumba moto ambao unaunguza, lakini kwa sharti ya kutouambia ‘kuwa baridi.’ Kwa hiyo kama atauambia hivyo utakuwa kama alivyosema. Kwa maneno mengine ni kuwa kuunguza kwake na kuwa baridi kwake kunafuta matakwa ya Mungu kutokana na kuumba kwake na kuufanya uweko.

Na wakamtakia ubaya, lakini tukawafanya wao ndio wenye kupata hasara.

Waliwasha moto ili umchome Ibrahim, lakini ukawa ni muujiza mkubwa na dalili ya kuthibitisha ukweli wake na utume wake:

وَمَكَرُوا وَمَكَرَ اللَّهُ ۖ وَاللَّهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ {54}

“Na wakapanga hila; na Mwenyezi Mungu akapanga hila; na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga hila” Juz. 3 (3:54).

Katika baadhi ya tafsiri za zamani, imeelezwa kuwa Namrud alipoona moto haumuathiri Ibrahim, aliamuru mali zake zichukuliwe na yeye mwenyewe atolewe nchini.

Ibrahim akasema: Mkichukua mali zangu basi nirudishieni umri wangu nilioumaliza kwenye nchi yenu. Wakaenda mahakamani, hakimu akatoa hukumu ya kunyang’anyawa mali Ibrahim na Namrud amrudishie umri wake. Hapo akasalimu amri na akamwacha Ibrahim na mali zake. Hekaya hii hatukuinukuu kwa kuamini kuwa ni kwali hivyo; isipokuwa inaonyesha kuwa kila mtu ana haki ya umri wake alioumaliza kwa sharti ya kuwa ameutumia kwenye halali.

وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ {71}

Na tukamwokoa yeye na Lut tukawapeleka kwenye ardhi tuliyoibariki, kwa ajili ya walimwengu wote.

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ نَافِلَةً ۖ وَكُلًّا جَعَلْنَا صَالِحِينَ {72}

Naye tukampa Is-haq na Yakub kuwa ni zawadi. Na wote tukawajaalia wawe watu wema.

وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا وَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِمْ فِعْلَ الْخَيْرَاتِ وَإِقَامَ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءَ الزَّكَاةِ ۖ وَكَانُوا لَنَا عَابِدِينَ {73}

Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri na wasimamishe Swala na watoe Zaka na walikuwa wanatuabudu sisi.

وَلُوطًا آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَتْ تَعْمَلُ الْخَبَائِثَ ۗ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمَ سَوْءٍ فَاسِقِينَ {74}

Na Lut tukampa hukumu na elimu na tukamwokoa na ule mji uliokuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa wabaya, mafasiki.

وَأَدْخَلْنَاهُ فِي رَحْمَتِنَا ۖ إِنَّهُ مِنَ الصَّالِحِينَ {75}

Na tukamwingiza katika rehema zetu. Hakika yeye ni miongoni mwa walio wema.

وَنُوحًا إِذْ نَادَىٰ مِنْ قَبْلُ فَاسْتَجَبْنَا لَهُ فَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ {76}

Na Nuh alipoita zamani, nasi tukamwitikia na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa.

وَنَصَرْنَاهُ مِنَ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمَ سَوْءٍ فَأَغْرَقْنَاهُمْ أَجْمَعِينَ {77}

Na tukamnusuru na watu waliozikadhibisha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawagharikisha wote.