read

Aya 7 – 15: Waulizeni Wenye Kumbukumbu

Maana

Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi. Basi waulizeni wenye kumbukumbu, ikiwa nyinyi hamjui.

Imekwishatangulia kwa herufi zake katika Juz. 14 (16:43).

Na hatukuwafanya miili isiyokula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.

wao wenyewe.

Manabii sio roho bila ya miili wala wao hawatakaa maisha hapa duniani. Wao ni kama watu wengine, hawana tofauti isipokuwa kwa kufikisha neno la Mungu na kwamba wao ni wakamilifu. Angalia Juz. 16 (20: 35) kifungu ‘Hakika ya Utume’.

Kisha tukawatimizia miadi na tukawaokoa wao na tuliowataka na tukawaangamiza waliopita mipaka.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaishiria kwenye kauli yake hii pale aliposema:

كَتَبَ اللَّهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي ۚ إِنَّ اللَّهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ {21}

“Mwenyezi Mungu amekwishaandika: Hakika nitashinda mimi na Mitume wangu.“Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.” (58:21).

Na akasema tena:

إِنَّا لَنَنْصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ {51}

“Hakika bila shaka tutawanusuru mitume wetu na walioamini katika maisha ya duniani na siku watakaposimama mashahidi. (40:51).

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaahidi mitume na wau- mini kuokoka na makafiri kuangamia. Alitekeleza ahadi yake. Ni nani kuliko Mwenyezi Mungu katika utekelezaji ahadi?

Muhammad Na Waarabu

Hakika tumewateremshia Kitabu, ndani yake mna ukumbusho wenu. Je, hamtii akili?

Kabla ya Muhammad (s.a.w.) na Qur’an waarabu hawakuwa ni chochote. Baada ya vitu viwili hivyo wakawa ni watu mashuhuri, ikatajwa historia namaendeleo yao, wakawa ni watu wa hali ya juu.
Anasema: W.L. Dewarnet katika Ensaiklopidia yake ya Historia ya kisa cha maendeleo katika ulimwengu: “Muhammad ni mkuu miongoni mwa wakuu wa Historia. Aliwainua watu walioishi katika giza la ushenzi, anga ya joto na ukame wa jangwa, kwenye ustawi wa kiroho na kimaadili. Alifaulu kwenye lengo hili kwa namna ambayo hajawahi kuifikia kiongozi yeyote katika historia yote.

Alipoanza mwito wake miji ya waarabu ilikuwa ni jangwa tupu linalokaliwa na makabila ya waabudu mizimu yenye watu wachache wasiokuwa na umoja wowote. Lakini kufikia kufa kwake wakawa ni umma wenye mshikamano, wakiwa wamekiuka ubaguzi na upuuzi.

Wakawa juu ya uyahudi na ukiristo na dini ya nchiyake ikawa wazi na nyepesi. Ikajengeka misingi ya kijasiri, utukufu na uzalendo. Kwenye kizazi kimoja tu ikaweza kushinda vita mia moja na katika karne moja ikaweza kuanzisha dola kuu na kubakia hadi leo kuwa ni nguvu kuu ulimwenguni”

Na miji mingapi iliyokuwa ikidhulumu tumeiteketeza na tukawaumba baada yao watu wengine.

Haya ni makemeo na kiaga kwa wale wanaomkadhibisha Muhammad (s.a.w.) kwamba wao yatawapata yaliyowapata waliokuwa kabla yao katika umma zilizowakadhibisha mitume wao. Kisha Mwenyezi Mungu awalete wengine wasiokuwa na uhusiano wowote na walioangamizwa; awarithishe milki zao na majumba yao. Wajenge upya na wastarehe na kheri zake na baraka zake.

Basi walipohisi adhabu yetu mara wakaanza kukimbia.

Hii ni taswira ya hali ya washirikina inapowafikia adhabu kutoka mbinguni, wanajaribu kuikimbia, lakini wapi! Inawezekana vipi kuukimbia utawala wa Mwenyezi Mungu na hukumu yake? Kama hapo mwanzo wangelikimbilia kwa Mwenyezi Mungu wangelikuta amani. Ama kumkimbia yeye Mwenyezi Mungu ni sawa na mtu kukimbia kivuli chake.

Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu na maskani zenu mpate kusailiwa.

Kabla ya kuteremshwa adhabu washirikina walikuwa hawajishughulishi na lolote zaidi ya mali na starehe zao, lakini ilipowashukia adhabu, nyoyo na akili zao zilipofuka na wakatupilia mbali kila kitu. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawaambia kwa kuwatahayariza: Mnaenda wapi? Rudini kwenye mali zenu na watoto wenu.

Leo mnaziacha na jana mlikuwa mkiziabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Haya ndio malipo ya anayeacha uongofu na asiongoke kwenye uongofu.

Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhalimu.

Walitulia na starehe zao, wakaitikia matamanio yao na wakamtuhumu anayewapa nasaha, lakini walipoiona adhabu walijuta na wakaita ole wetu, lakini majuto ni mjuukuu hayarudishi yaliyopita.

Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya wamefyekwa wamezimika.

Wanalia ole wetu na adhabu iko kichwani mwao ikiendelea. Haikufaa mali wala jaha. Huo ndio mwisho wa wakosefu.

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ {16}

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa mchezo.

لَوْ أَرَدْنَا أَنْ نَتَّخِذَ لَهْوًا لَاتَّخَذْنَاهُ مِنْ لَدُنَّا إِنْ كُنَّا فَاعِلِينَ {17}

Kama tungelitaka kufanya mchezo tungelijifanyia sisi wenyewe, kama tungekuwa ni wafanyao mchezo.

بَلْ نَقْذِفُ بِالْحَقِّ عَلَى الْبَاطِلِ فَيَدْمَغُهُ فَإِذَا هُوَ زَاهِقٌ ۚ وَلَكُمُ الْوَيْلُ مِمَّا تَصِفُونَ {18}

Bali tunaitupa haki juu ya batili ikaivunja na mara ikatoweka. Na ole wenu kwa mnayoyasifia .

وَلَهُ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَمَنْ عِنْدَهُ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ {19}

Ni vyake vilivyoko mbinguni na ardhini na walioko mbele yake hawafanyi kiburi wakaacha kumwabudu wala hawachoki.

يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ {20}

Wanamsabihi usiku na mchana wala hawanyog’onyei.

أَمِ اتَّخَذُوا آلِهَةً مِنَ الْأَرْضِ هُمْ يُنْشِرُونَ {21}

Au wamepata miungu katika ardhi inayofufua.

لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّهُ لَفَسَدَتَا ۚ فَسُبْحَانَ اللَّهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ {22}

Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu basi zingefisidika. Ametasika Mwenyezi Mungu, Mola wa arshi, na hayo wanayoyasifu.

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ {23}

Yeye haulizwi kwa ayatendayo na wao ndio waulizwao kwa wayatendayo.