read

Aya 71 – 76: Wanaabudu Asiyekuwa Mungu

Maana

Na wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ambavyo hakuviteremshia dalili na ambavyo hawana ujuzi navyo.

Kujua kitu chochote ni lazima kuwe ama kwa msingi ulio wazi, ambako mtu anapata kujua, kwa kiasi tu cha kuleta picha yake; kwa mfano kujua kuwa pembe tatu sio mraba na mraba sio mduara. Au kuwe kwa nadharia; mfano kuwa ardhi inazunguka kandokando ya jua.

Kwa hiyo makusudio ya dalili hapa ni dalili za nadharia na makusudio ya ujuzi ni misingi iliyo wazi. Yaani washirikina wameabudu masanamu na mengineyo bila ya kutegemea nadharia yoyote au kwenye msingi wowote.

Wamemdhulumu Mwenyezi Mungu kwa kuabudu masanamu kwa kum- fanyia washirika na wamejidhulumu wenyewe kwa kujiweka kwenye ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Na madhalimu hawatakuwa na wakuwasaidia siku ya hisabu na malipo.

Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki katika nyuso za waliokufuru. Hukaribia kuwavamia wale wanowasomea Aya zetu.

Wanaosomewa ni wale wanoabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Walikuwa wanapomsikia Mtume (s.a.w.) au waumini wakiwasomea Qur’an au hoja nyinginezo basi nyuso zao zinageuka kwa chuki na wanakusudia kuwavamia wale wanaowasikia.

Sema: Je, niwaambiye yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni moto Mwenyzi Mungu aliowaahidi waliokufuru, na ni marudio mabaya hayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamuru Mtume wake mtukufu, kuwaambia hao wenye hasira, ikiwa ni uzito kwenu kusikiliza haki, basi moto wa Jahannam kwenu ni mkali na mkubwa zaidi.

Wajihi Na Mtazamo Wa Macho

Hakuna kitu kizito kwa mvunjifu kuliko tamko la haki, na ushindi wa watu wa haki; hasa pale anaposhindwa mvunjifu kuizuwia haki. Atanyamaza huku akijifanya hajali, lakini dalili zinazoakisi usoni mwake na mtazamo wa macho yake zinamfedhehesha.

Mtu anaweza kuwa muongo na kuwadanganya watu katika kauli yake na vitendo vyake, kwa sababu ana uwezo wa kuufanya ulimi wake na kuuzunguusha vile atakavyo. Vilevile mikono yake na miguu yake na huipeleka vile atakavyo. Ingawaje harakati za ulimi kwake ni jambo jepesi, lakini kuna kitu kimoja tu, hawezi kukihukumu vile atakavyo.

Kitu chenyewe ni moyo, uwe mzima au mbovu. Akipenda au kuchukia, athari yake hudhihiri usoni na machoni waziwazi. Haziwezi kufichwa na tabasamu la kutengeneza wala maneno ya kutiwa asali. Ndio maana ikawa kipimo sahihi cha undani wa binadamu sio maneno na vitendo.

Enyi watu! Umepigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu hawatoumba nzi wajapojumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kwamba washirikina wameya- pa masanamu yao sifa za uungu, bila ya dalili, ametaja katika Aya hii, dalili za kihisia kukanusha sifa hii, ambazo anaweza kuzifahamu mjinga na hata mtoto pia: kwamba nzi ni kiumbe dhaifu, lakini lau nzi atachukua kitu kutoka kwenye masanamu, kisha masanamu hayo yakusanyike na yatangaze vita dhidi ya nzi kutaka kurudisha yalichonyang’anywa, nzi angelikuwa ni mshindi; sikwambii tena kuweza kuumba huyo nzi au hata kuumba ubawa wake.

Amedhoofika atakaye naye ni sanamu na anayetakiwa ambaye ni nzi. Kwa hiyo vipi yatakuwa masanamu ni Mungu.

Unaweza kuuliza kuwa masanamu hayo yenyewe tayari ni dalili kuwa sio Mungu, sasa vipi Qur’an imejishughulisha kuyaletea dalili?

Jibu: Ni kweli kuwa kukanusha uungu wa masanamu ni katika mambo yaliyo wazi kiakili, lakini wale walioyaabudu hawakuyaabudu kwa msukumo wa kiakili; isipokuwa ni kwa misukumo mingine; kama vile malezi, uigaji, maslahi na mingineyo ambayo haikubali kukosolewa kwa namna yoyote ile.

Kuhusu Itikadi Ya Tawhdi

Wakati nikifasiri Aya za Qur’an yenye hekima, nimetambua kwamba kila ninapoendelea kufasiri, Mwenyezi Mungu hunifungulia milango mingine ya maarifa ya siri za Qur’an na maajabu yake isiyokuwa na kiasi.

Kuna Aya nyingi zinazokaririka, katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kimatamshi na kimaana ambazo mara ya kwanza ninazifafanua kwa nilivyofahamu kutokana na tamko lenyewe au mfumo wa maneno n.k. Mara ya pili ninaunganisaha Aya iliyokaririka na ile iliyopita huku nikitaja namba yake na Sura yake au ninaifasiri kwa mfumo mwingine.

Ninapoifasiri mara ya pili au ya tatu huwa ninagundua upande ambao ulifichika kwangu hapo mwanzo na kwa wafasiri wengine wote niliowaangalia.

Aya nyingi zaidi zinazokaririka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni zile zinazofahamisha umoja wa Muumba na kupinga ushirikina na watu wake. Hayo Mwenyezi Mungu ameyataja kwa kila mfumo na kwa sura mbalimbali.

Nimezungumzia Tawhid na kukanusha ushirikina katika Juz. 5 (4: 48 – 50) kwa anuani ya ‘Dalili ya umoja na utatu.’ Kisha nikarudia maudhui hayo kwa mfumo mwingine katika Juz. 13 (13: 16), kwa anuani ya ‘Akili za watu haziwatoshelezi.’ Vilevile nimeleta mfumo wa tatu katika Aya ya 31 ya Sura hii tuliyo nayo. Na nitaleta mfumo mwingine wa nne na tano kulingana maudhui yatakavyokuwa. Hivi sasa narudia kwa ubainifu ufuatao:

Hakika lengo kuu la Uislamu ni kumuunganisha Muumba na kiumbe chake, kwa kupata muongozo katika yale anayoyaitakidi na kuyafikiri, kuyasema na kuyafanya na kuelekea kwake katika yote hayo.

Ndio maana Uislamu ukapinga ushirikina na kuuzingatia kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa na kosa lisilosameheka. Kama ambavyo umeichukulia ria na kufanya amali kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni shirk; na ukawapa washirikina adhabu kubwa na kali zaidi.

Hapana mwenye shaka kwamba watu wote wakiamini Mungu mmoja na wakawa na harakati kwa utashi mmoja, basi lazima wote watakuwa kwenye dini na sharia moja; isiyo na mifundo ya kidini wala kelele za utaifa au kuifanyia biashara dini na madhehebu.

Lakini kuweko na miungu wengi na kila mtu na lake, basi matokeo yake ni mfarakano na mvurugano baina ya watu. Kwa hiyo Uislamu unalingania kwenye itikadi ya Tawhid itakayomungoza kwenye misingi ambayo yatajengeka mapenzi, udugu, amani na raha.

Kuongezea kwamba huyo Mungu mmoja, ambaye uislamu unatoa mwito aabudiwe na kufutwa sharia zake, ndiye Mungu wa ulimwengu Mwenye hekima, Mwadilifu na Mwingi wa rehema anayewapenda watu wote kwa usawa. Anachukia aina zote za sharia, atawalipa wema waliotenda mema na atawalipa ubaya kwa yale waliyoyafanya.

Hawakumkadiria Mwenyezi Mungu haki ya kadiri yake kwa vile walimwabudu mwingine wakaasi amri yake.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.

Atawaadhibu na hawatapata mlinzi wala msaidizi zaidi yake.

Mwenyezi Mungu huteua wajumbe miongoni mwa Malaika, kama vile Jibril, kutemsha wahyi kwa manabii.

Na miongoni mwa watu vilevile huteua wajumbe wanaotoa mwito wa yale yanayomridhisha.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

Anasikia kauli zao na anajua yaliyo katika dhamiri zao na yale wayafanyao.

Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao.

Ni kinaya cha kuwa hakifichiki chochote mbele yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ni ufafanuzi wa kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.’

Na kwa Mwenyezi Mungu yatarejeshwa mambo yote.

Kwake ndio mwanzo na ndio mwisho. Kwa maneno mengine: “Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.”

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا وَاعْبُدُوا رَبَّكُمْ وَافْعَلُوا الْخَيْرَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ۩ {77}

Enyi ambao mmeamini! Rukuuni na sujuduni, na muabuduni Mola wenu, na fanyeni kheri huenda mkafaulu.

وَجَاهِدُوا فِي اللَّهِ حَقَّ جِهَادِهِ ۚ هُوَ اجْتَبَاكُمْ وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ مِلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ ۚ هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ مِنْ قَبْلُ وَفِي هَٰذَا لِيَكُونَ الرَّسُولُ شَهِيدًا عَلَيْكُمْ وَتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ ۚ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَاعْتَصِمُوا بِاللَّهِ هُوَ مَوْلَاكُمْ ۖ فَنِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ {78}

Na fanyeni jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu jihadi inayomstahiki. Yeye ndiye ambaye amewachagua. Wala hakuweka juu yenu uzito katika dini. Ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye aliwaita waislamu tangu zamani na katika hii. Ili Mtume awe shahidi juu yenu na nyinyi muwe mashahidi juu ya watu. Basi simamisheni Swala na toeni Zaka na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora na Msaidizi bora kabisa.