read

Aya 71 – 77: Tukamwokoa Yeye Na Lut

Maana

Na tukamwokoa yeye na Lut tukawapeleka kwenye ardhi tuliyoibariki, kwa ajili ya walimwengu wote.

Makusudio ya aliyeokolewa hapa ni Ibrahim (a.s.). Lut ni mtoto wa kaka yake. Katika Tafsiri imelezwa kuwa Ibrahim aliondoka akaelekea nchi ya Sham, ambayo ndani ilikuwako Palestina.

Vyovyote iwavyo ni kwamba makusudio ni kumfananisha Muhammad (s.a.w.) na kaumu yake pamoja na Ibrahim (a.s.) na kaumu yake.

Kaumu zote mbili ziliabudu masanamu, zikakataa mwito wa nabii wao na kujaribu kumuua. Manabii wote wawili Mungu aliwaokoa na kuwatengenezea njia ya hijra na kuwaneemesha kwa hijra hiyo.

Naye tukampa Is-haq na Yakub kuwa ni zawadi.

Is-haq ni mtoto wa Ibrahim wa kumzaa, na Yakub ni mjukuu naye ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na wote tukawajaalia wawe watu wema.

Ibrahim, Is-haq , wote walikuwa wema.

Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri na wasimamishe Swala na watoe Zaka na walikuwa wanatuabudu sisi.

Maimamu ndio viongozi wa dini ambao amewateua Mwenyezi Mungu, kuwaongoza waja. Sifa yao kuu ni kwamba wao wanaongoza watu kama alivyoamrisha Mungu, si kama wanavyoamrisha wake zao, watoto wao au wakwe zao; wanahimiza kufanya kheri sio chuki za utaifa; na kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake sio mwenginewe.

Na Lut tukampa hukumu na elimu na tukamwokoa na ule mji uliokuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa wabaya, mafasiki. Na tukamwingiza katika rehema zetu. Hakika yeye ni miongoni mwa walio wema.

Tazama tafsiri yake katika Juz. 8 (7: 80) na Juz 12 (11:77).

Na Nuh alipoita zamani, nasi tukamwitikia na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa. Na tukamnusuru na watu waliozikadhibisha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawagharikisha wote.

Kisa cha Nuh kimetangulia katika Juz. 12 (11:25).

وَدَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ إِذْ يَحْكُمَانِ فِي الْحَرْثِ إِذْ نَفَشَتْ فِيهِ غَنَمُ الْقَوْمِ وَكُنَّا لِحُكْمِهِمْ شَاهِدِينَ {78}

Na Daud na Suleiman walipohukumu juu ya shamba, walipolisha humo mbuzi wa watu usiku. Na sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao.

فَفَهَّمْنَاهَا سُلَيْمَانَ ۚ وَكُلًّا آتَيْنَا حُكْمًا وَعِلْمًا ۚ وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ ۚ وَكُنَّا فَاعِلِينَ {79}

Tukamfahamisha Suleiman na kila mmoja wao tukampa hukumu na elimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imsabihi (Mwenyezi Mungu). Na sisi tulikuwa ni wenye kuifanya.

وَعَلَّمْنَاهُ صَنْعَةَ لَبُوسٍ لَكُمْ لِتُحْصِنَكُمْ مِنْ بَأْسِكُمْ ۖ فَهَلْ أَنْتُمْ شَاكِرُونَ {80}

Na tukamfundisha kutengeneza mavazi ya vita ili kuwakinga katika mapigano yenu. Je, mtakuwa wenye kushukuru?

وَلِسُلَيْمَانَ الرِّيحَ عَاصِفَةً تَجْرِي بِأَمْرِهِ إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا ۚ وَكُنَّا بِكُلِّ شَيْءٍ عَالِمِينَ {81}

Na upepo mkali kwa ajili ya Suleiman, wendao kwa amri yake, katika ardhi tuliyoibariki. Na sisi ndio tunaojua kila kitu.

وَمِنَ الشَّيَاطِينِ مَنْ يَغُوصُونَ لَهُ وَيَعْمَلُونَ عَمَلًا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ وَكُنَّا لَهُمْ حَافِظِينَ {82}

Na katika mashetani kuna wanompigia mbizi na kufanya kazi nyinginezo; Nasi tulikuwa walinzi wao.