read

Aya 77 – 78: Fanyeni Kheri Ili Mfaulu

Maana

Enyi ambao mmeamini! Rukuuni na sujuduni, na muabuduni Mola wenu, na fanyeni kheri huenda mkafaulu. Na fanyeni jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu jihadi inayomstahiki.

Hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaambia wale walimwamini Yeye na Mtume wake, kwamba kuamini tu hakufai kitu; ila kukiweko mambo mane:

1. Kuchunga Swala kwa ajili yake tu. pale aliposema: ‘Rukuuni na sujuduni.’

2. Kujiepusha na yale aliyoyaharamisha, kama hiyana, unafiki, kuleta fitna, kuwazuilia watu wema na kupanga njama kuleta uharibifu na ufisa- di. Hayo ndio makusdio ya kusema kwake: ‘Na muabuduni Mola wenu.’

3. Kufanya mambo ya kheri, kama kuwakoa wenye kuangamia, kusu- luhisha, na kusaidia kwenye masilahi ya umma. Ndio makusudio ya kuse- ma: ‘na fanyeni kheri.’

4. Kupigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu kwa hali na mali.

Yakipatikana mambo haya kwa mtu basi yeye ni katika waliofaulu na watu wema. Yametangulia maelezo kwamba neno ‘huenda,’ kwa Mwenyezi Mungu, linamaanisha uhakika wa kuwepo, lakini likitumika kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi linakuwa na maana ya kuweko uwezekano na matarajio.1

Yeye ndiye ambaye amewachagua.

Yeye ni Mwenyezi Mungu na maneno yanaelekezwa kwa waislamu. Wajihi wa kuwa wamechaguliwa ni kule kuhusika kwao na Bwana wa Mtume aliye mwisho wa manabii na sharia yake ya kudumu.

Wala hakuweka juu yenu uzito katika dini.

Huu ndio msingi katika misingi ya sharia za kiislamu, kudhihiri upana, kuwa mororo na ulaini wake. Kuna Hadith isemayo: “Hakika dini ya Mwenyezi Mungu ni nyepesi,” haina uzito wala mashaka na ndiyo dini ya maumbile.

Ni kutokana na msingi huu ndio mafakihi wametoa fatwa na hukumu katika milango yote ya fiqh. Katika ndimi zao na vitabu zimeenea kanuni hizi zifuatazo:

• Dharura huondoa vizuizi.

• Dharura hupimwa kwa kiwango chake.

• Dharura kali huondolewa na dharura hafifu.

• Huvumiliwa dharura binafsi kwa kuondoa dharura ya umma.

Miongoni mwa yanayoonyesha kuwa Uislamu ni mwepesi, ni kule kutokuwako kipingamizi chochote baina ya mtu na muumba wake; kama zilivyo dini nyingine.

Ni mila ya baba yenu Ibrahim.

Makusudio ya mila ni dini. Dini ya Ibrahim inaingia katika Uislamu kwa misingi yote na sharia zake nyingi na tanzu zake. Ibrahim (a.s.) ndiye baba wa hakika wa manabii na roho ya watu wa dini za mbinguni kwa kuangalia kutangulia kwake, na kuafikiana wote juu ya unabii wake na ukuu wake.

Yeye aliwaita waislamu tangu zamani na katika hii.

Imesemekana kuwa yeye, hapa ni Ibrahim, na kwanye neno ‘hii ‘ kuna maneno ya kukadirwa kuwa ‘na katika hii kuna utukufu wenu.’

Pia imesemekana kuwa yeye hapa ni Mwenyezi Mungu na ‘katika hii’ ni Qur’an; kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu aliwaita nyinyi umma wa Muhammad waislamu katika vitabu vilivyotangulia, na vilevile amewaita waislamu katika hii Qur’an.

Tafsri zote mbili zinfaa, kwa sababu Ibrahim (a.s.) anazungumza mazungumzo ya Mwenyezi Mungu. Tazama Juz. 3 (3:19) kifungu cha ‘Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu.’

Ili Mtume awe shahidi juu yenu na nyinyi muwe mashahidi juu ya watu.

Kesho hakimu ni Mwenyezi Mungu, shahidi wa kwanza ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na shahidi wa pili ni ulama.

Mtume atakuwa shahidi juu ya wenye elimu kwamba aliwafikishia kutoka kwa Mungu nao wafikishe kwa umma wa Muhammad (s.a.w.) na wengineo. Akizembea mmoja wa maulama kufikisha ujumbe, basi atakuwa amestahili ghadhabu za Mwenyezi Mungu na makazi yake ni Jahannam ambayo ni makazi mabaya. Umetangulia mfano wake katika Juz. 2 (2:143).

Basi simamisheni Swala na toeni Zaka.

Huu ni msisitizo wa yaliyopita katika Aya ilyotangulia.

Na shikamaneni na Mwenyezi Mungu.

Shikamaneni na twaa yake na mjiweke mbali na kumwasi katika Nahjul- balagha imesemwa “Kujiepusha na maasi ni katika aina za isma.”

Yeye ndiye Mlinzi wenu, ikiwa mtamtii na mkawa na msimamo.

Mlinzi bora na Msaidizi bora kabisa kwa yule atakayemfanya ni mlinzi wake na akamtegemea yeye tu, si mwingine.

  • 1. Ndio maana mara nyingine tunafasiri ‘ili’, kama wafanyavyo wafasiri wengi wa kiswahili -Mtarjumu