read

Aya 78 – 82: Daud Na Suleiman

Maana

Na Daud na Suleiman walipohukumu juu ya shamba, walipolisha humo mbuzi wa watu usiku. Na sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao.

Kuna riwaya iliyo mashuhuri midomoni mwa wapokezi, kwamba watu wawili walikwenda kuamuliwa kwa Daud. Mmoja alikuwa na mimea na wa pili alikuwa na mifugo ya mbuzi na kondoo. Mwenye shamba akasema wanyama wa huyu bwana wamelisha kwenye mimea yangu usiku. Baada ya kumthibitikia hilo, Daud alitoa hukumu kuwa wanyama wawe wa mwenye shamba.

Suleiman alipojua hivyo akasema, ni vizuri mwenye shamba awachukue wanyama, anufaike nao lakini wasiwe wake kabisa, na mwenye wanyama achukue ardhi aishghulikie mpaka iwe kama ilivyokuwa kabla ya kuliwa. Kisha bada ya hapo kila mmoja achukue mali yake. Daud akapendezewa na hukumu ya mwanawe na akaitumia.

Dhahiri ya Aya inaafikiana na riwaya hii. Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwamba yeye amesema: “Linaloafikiana na Qur’an lichukueni na linalokhalifiana nalo liacheni.”

Unaweza kuuliza: Kila mmoja kati ya Daud na Suleiman ni Nabii na Nabii ni maasumu; hasa katika hukumu ya sharia na hukumu ya sawa, sasa je kuna wajihi gani wa kupingana hukumu mbili hizi?

Baadhi wamejibu kuwa kauli ya Daud ilikuwa ni upatanishi sio hukumu. Lakini ijulikane kuwa upatanishi unakuwa kwa baadhi ya mali sio yote na Daud hakumbakishia mfugaji hata mnyama mmoja.

Wengine wakasema kuwa kila mmoja kati ya manabii wawili hao alihukumu kwa ijitihadi yake. Kauli hii vile vile ina kasoro; kwamba Nabii anatumia ijitihadi kama ulama wengine na inajulikana kuwa rai ya ijtihadi inakuwa kwa kukosekana nukuu (Nass) na ilivyo ni kuwa kauli ya Nabii ni nukuu ya haki; na kwamba ijitihadi ina uwezekano wa kupatia na kukosea, jambo ambalo haliswihi kwa maasumu.

Jamaa wamesema kuwa hukumu ilikuwa kama alivyopitisha Daud; kisha ikabadilishwa (naskh), na kauli ya Suleiman1

Kauli hii ina nguvu zaidi kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Tukamfahamisha Suleiman na kila mmoja wao tukampa hukumu na elimu.

Hapo Mwenyezi Mungu anashudia kuwa kila mmoja ni mjuzi wa hukumu. Kwa hiyo basi kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Tukamfahamisha Suleiman’ ni kwamba yeye alimpelekea wahyi wa kubadilisha hukumu ya baba yake. Mafaqihi wametofautiana kuwa je mwenye mifugo atalipa kilichoharibiwa na wanyama wake?

Maliki na Shafi wamesema kuwa atalipa kilichoharibiwa usiku sio mchana. Abu Hanifa akasema halipi kwa hali yoyote; iwe usiku au mchana.

Jamaa katika mafaqihi wa kishia wamesema kama alivyosema Maliki na Shafi na wahakiki katika wao wakasema kuwa litakaloangaliwa ni hali ya uzembe wa mfugaji au la; sio hali ya kuwa usiku au mchana. Ikiwa mfugaji atazembea au kufanya makusudi, basi atalipa. Na ikiwa atajichunga na asipuuze, ikatokea bahati mbaya basi hatalipa.

Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imsabihi (Mwenyezi Mungu). Na sisi tulikuwa ni wenye kuifanya.

Imekuwa mashuhuri kuwa Daud alikuwa na sauti nyororo. Majaribio yamethibitisha kuwa wanyama wengi wanaburudika na aina fulani ya nyimbo na muziki2. Niliwahi kusoma kwenye gazeti kwamba nyoka aliwahi kutoka kwenye tundu yake ili astarehe na nyimbo za Ummu Kulthum, katika moja ya hafla yake. Nyimbo ilipokwisha akarudi sehemu yake.

Ama tasbibih ya mlima ni kwa njia ya majazi na kusifia zaidi tu; kama kusema: Amelichekesha na kuliliza jiwe. Au inawezekana ni kiuhakika hasa. Kwa sababu yule aliyeweza kuufanya moto kuwa baridi na salama kwa Ibrahim, ndiye anaweza pia kulifanya jabali litoe tasbih pamoja na Daud.

Angalia Aya 69 ya Sura hii tuliyo nayo.

Na tukamfundisha kutengeneza mavazi ya vita ili kuwakinga katika mapigano yenu. Je, mtakuwa wenye kushukuru?

Makusudio ya mavazi ya vita hapa ni deraya. Aya inaonyesha kuwa Daud ndiye mtu wa kwanza kutengeneza deraya.

Kuna riwaya inayoelezea kwamba sababu ya hilo ni kuwa Daud alikuwa ni mfalme wa Israil na alikuwa ana desturi ya kupita mitaani kujulia hali za watu, bila ya yeye kujulikana. Siku moja akakutana na mtu akamuuliza kuhusu sera za mfalme Daud.

Yule mtu akasema: Ana sera nzuri sana, kama asingekuwa anakula kwenye hazina ya serikali. Daud akaapa kuwa kuanzia siku hiyo hatakula kitu isipokuwa kilichotokana na mikono yake na jasho lake.

Alipojua Mwenyezi Mungu ikhlasi yake na ukweli wa nia yake, alimalainishia chuma na kumfundisha kutengeneza deraya.

Iwe sahihi riwaya hii au la, ni kwamba inaashria wajibu wa kufanya bidii kubwa kuchunga masilahi ya watu na mali zao. Kuna Hadith mutawatir kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (s.a.w.), alifariki akiwa ameweka rahani deraya yake kwa sababu ya kukopa kiasi fulani cha shayir, huku zikiwa mali za Bara arabu zote ziko mikononi mwake.

Na upepo mkali kwa ajili ya Suleiman, wendao kwa amri yake, kati- ka ardhi tuliyoibariki. Na sisi ndio tunaojua kila kitu.

Dhahiri ya Aya hii inafahamisha kuwa upepo ulikuwa ukimchukua Suleiman kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Wala hakuna haja ya kuleta taawili, maadamu akili inakubaliana na dhahiri hiyo.
Aya iliyo wazi zaidi ya hii ni ile isemayo: “Na Suleiman tukamtiishia upepo mwendo wake asubuhi ni mwezi mmoja na mwendo wake jioni yake ni mwezi mmoja.” (34:12) Yaani asubuhi unakwenda mwendo wa mwezi mmoja kwa kusafiri na ngamia na jioni vile vile.

Makusudio ya ardhi iliyobarikiwa ni ile iliyotajwa kwenye Aya ya 71 ya Sura hii.

Unaweza kuuliza: Hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema upepo mkali na mahali pengine anasema: pole pole: “Na tukamtiishia upepo uendao polepole kwa amri yake.” (38:36). Je, kuna wajihi gani wa Aya zote mbili?

Jibu: Huwa mara unakwenda kwa kasi na mara nyingine polepole kulin- gana na amri yake; sawa na gari au ndege.

Na katika mashetani kuna wanompigia mbizi baharini na kumtolea lulu na marijani.

Makusudio ya mashetani hapa ni majini

Na kufanya kazi nyinginezo; kama kujenga mihirabu na picha:

يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِنْ مَحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَاسِيَاتٍ ۚ {13}

Wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu na picha na masinia makubwa, kama hodhi na masufuria makubwa yasiyoondolewa mahali pake.” (34:13).

Nasi tulikuwa walinzi wao, kwamba wasitoroke na kufanya ukorofi. Hatuna la kuongeza zaidi ya ulivyothibisha wahyi kuwepo majini na kwamba wao walimtumikia Suleiman na akili hailikatai hilo. Kwa hiyo basi hakuna haja yoyote ya kuleta taawili na kuyazungusha maneno. Imam Ali (a.s.) amesema: “Lau kama mtu angeliweza la kumfanya adumu ulimwenguni au kuhepa mauti, basi angelikuwa Suleiman ambaye alitiishiwa ufalme, majini watu, utume na heshima kuu.”

وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنْتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ {83}

Na Ayyub aliopomlingania Mola wake: Hakika mimi imenigusa dhara, nawe ndiye unayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu.

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ فَكَشَفْنَا مَا بِهِ مِنْ ضُرٍّ ۖ وَآتَيْنَاهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُمْ مَعَهُمْ رَحْمَةً مِنْ عِنْدِنَا وَذِكْرَىٰ لِلْعَابِدِينَ {84}

Basi tukamkubalia na tukamuondolea dhara na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema itokayo kwetu na ukumbusho kwa wafanyao ibada.

وَإِسْمَاعِيلَ وَإِدْرِيسَ وَذَا الْكِفْلِ ۖ كُلٌّ مِنَ الصَّابِرِينَ {85}

Na Isamil na Idris na Dhulkifl, wote walikuwa miongoni mwa wanaosubiri.

وَأَدْخَلْنَاهُمْ فِي رَحْمَتِنَا ۖ إِنَّهُمْ مِنَ الصَّالِحِينَ {86}

Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao ni katika watu wema.

وَذَا النُّونِ إِذْ ذَهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَنْ لَنْ نَقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَنْ لَا إِلَٰهَ إِلَّا أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنْتُ مِنَ الظَّالِمِينَ {87}

Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhabika na akadhani kuwa hatutamdhikisha. Basi aliita katika giza kwamba: Hapana Mola isipokuwa wewe, umetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنْجِي الْمُؤْمِنِينَ {88}

Basi tukamkubalia na tukamwokoa kutokana na ghamu. Kama hivyo tunawaokoa wenye kuamini.

وَزَكَرِيَّا إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ رَبِّ لَا تَذَرْنِي فَرْدًا وَأَنْتَ خَيْرُ الْوَارِثِينَ {89}

Na Zakaria alipomwita Mola wake: Ewe Mola wangu! Usiniwache peke yangu na wewe ndiye mbora wa wanaorithi.

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ {90}

Basi tukamwitikia na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi kufanya kheri na wakituomba kwa hofu na walikuwa wakitunyenyekea.

وَالَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهَا مِنْ رُوحِنَا وَجَعَلْنَاهَا وَابْنَهَا آيَةً لِلْعَالَمِينَ {91}

Na mwanamke aliyelinda tupu yake na tukampulizia katika roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni ishara kwa walimwengu.
  • 1. Kama ilivyo katika baadhi ya hukumu kwenye Qur’an –Mtarjumu.
  • 2. Pia waswahili wana msemo wakitaka kuusifia wimbo husema: “Wimbo uliomtoa nyoka pangoni” –Mtarjumu.