read

Aya 8 – 14: Sababu Ya Maarifa Katika Aya Moja

Maana

Na katika watu wapo wanaojadiliana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu wala uongufu wala Kitabu chenye nuru.

Wewe unaona hii ndiyo haki na ile ni batili, lakini ni lipi lililokujulisha kwamba rai yako ni sahihi na salama? Una dhamana gani ya usahihi huo? Inawezekekana kuwa ile unayoiona ni haki kumbe ni batili na ile unayoiona ni batili kumbe ni haki.
Hakuna njia ya kujua maarifa sahihi isipokuwa kwa kurejea kwenye chimbuko lake na sababu iliyotokana nayo. Ikiwa sababu ni sahihi basi maarifa nayo yatakuwa sahihi; vinginevyo yatakuwa batili. Kwa sababu tawi lina- fuata shina.

Swali linarudi tena: Je, ni ipi hiyo sababu ya maarifa sahihi? Utaitambuaje? Jamaa katika wanafalsafa wanasema kuwa sababu ya maarifa sahihi inakuwa kwenye majaribio ya hisia tu. Wengine wakasema ni akili; na hisia ni vyombo tu. Ama Qur’an, katika Aya tunayoifasiri, imetaja sababu tatu za maarifa: Kwanza ni majaribio ya hisiya yaliyotajwa kwa neno ‘ilimu’ Ya pili ni akili iliyoitwa ‘Uongofu’ Ya tatu ni Wahyi iliyokusudiwa kwenye neno ‘Kitabu chenye nuru’.

Majaribo ya hisia yanakuwa ni sababu ya kujua vitu vya kimaada tu. Kwa sababu ndivyo vinavyoweza kuhisiwa na kufanyiwa majaribio. Tena majaribio haya huwa yanahitajia akili, kwa sababu hisia haziwezi kutambua kitu ila kwa msaada wa akili.

Ni akili pekee ndiyo inayoweza kujua na kuthibitisha kuweko Mungu. Ama utume unathibitika kwa akili na kwa miujiza. Ukitaka ibara ya ndani zaidi sema: Utume unathibitika kwa miujiza inayothibitishwa na akili na kuikubali kuwa imetoka mbinguni sio ardhini.

Ama wahyi ni sababu ya kujua kila uliyokuja nayo. Wahyi ndio njia pekee ya kujua mambo ya ghaibu; kama majini, Malaika, Kiyama, namna ya hisabu na na malipo kwenye ufufuo n.k.

Anayegeuza shingo yake ili awapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na siku ya Kiyama tutamuonjesha adhabu ya kuungua.

Kugeuza shingo ni kinaya cha kiburi.

Yeye hajui kitu, anajadili kuhusu Mungu bila ya ujuzi, ana kiburi kinachomuhadaa na ni mpotevu na mpotezaji. Hakuna malipo ya wajinga weneye kiburi isipokuwa kudharaulika na kupuuzwa na watu na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hayo ni kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yako na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja. Kwa sababu amewaondolea udhu- ru kwa kuwapa akili, kuwapelekea mitume na akateremsha vitabu.

Na katika watu wapo wanaomwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemtaja anayemkufuru Mwenyezi Mungu na kumjadili bila ya elimu. Hapa anamtaja yule anayemwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni.

Wafasiri wametofautiana katika makusudio ya kabudu ukingoni. Kuna waliosema kuwa ni kumwabudu Mwenyezi Mungu pamoja na shaka katika dini. Wengine wakasema ni kumwabudu kwa ulimi tu sio kwa moyo na kauli nyingine.

Hakuna haja ya kutofautiana huku wakati Mwenyezi Mungu amekwisha mbainisha anayemwabudu ukingoni kwa kusema:

Ikimfika kheri hutulia kwayo na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake.

Makusudio ya kheri hapa ni mambo ya kufurahisha na misukosuko ni madhara. Kutulia ni kuwa na raha na kuendelea na ibada, na kugeuza uso ni kurtadi dini. Maana ni kuwa anayemwabudu Mwenyezi Mungu ukingoni ni yule anayeweka sharti kwa ibada yake, mpaka apate kitu ndio anaabudu vinginevyo humkufuru Mungu, vitabu vyake na mitume yake.

Na yoyote mwenye kumkufuru basi malipo yake ni Jahannam na ni mwisho mbaya.

Amepata hasara ya dunia na Akhera; hiyo ndiyo hasara iliyo wazi.

Amepata hasara ya nyumba mbili: ambapo mwanzo ni balaa na madhara. Pili, atafika kwa Mola wake akiwa anamkufuru. Kuna hasara kubwa zaidi ya ufukara duniani na adhabu akhera.

Ufafanuzi zaidi wa Aya hii ni riwaya inayosema kwamba baadhi ya mabedui walikuwa wakifika kwa Mtume (s.a.w.) wakihama kutoka ubeduini kwao.

Basi mmoja wao akiwa na mali nyingi huswali na kufunga. Akipatwa na masaibu au akicheleweshewa sadaka basi huritadi. Nimeyashuhudia yanayofanana na haya nilipokuwa nikiishi na baadhi ya wanakijiji.

Baada ya hayo, hakika mumin wa kweli ni yule anayemfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na kumtegemea katika hali zote; anakuwa na subira wakati wa shida na anashukuru wakati wa raha.

Katika Nahjul balagha kuna maelezo haya: “Haiwi kweli imani ya mja mpaka yawe yaliyo mikononi mwa Mwenyezi Mungu anayategemea zaidi kuliko yaliyo mikononi mwake.”

Anaomba, badala ya Mwenyezi Mungu, kile kisichomdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotelea mbali.

Maana ya Aya hii yametangulia kwenye Aya nyingi, yenyewe pia iko wazi.

Anamuomba yule ambaye hakika dhara iko karibu zaidi kuliko nafuu yake. Hakika ni mlinzi mbaya na ni rafiki mbaya.

Unaweza kuuliza kuwa katika Aya ya kwanza Mwenyezi Mungu amekanusha kuweko manufaa na madhara kwa yale wanayoyaabudu washirikina, kisha katika Aya hii anathibitisha kuweko manufaa ya mbali na madhara ya karibu. Je, kuna wajihi gani baina ya Aya mbili hizi?

Jibu: makusudio ya chenye kuabudia katika Aya ya kwanza ni mawe; hayanufaishi wala hayadhuru. Na makusudio katika Aya ya pili ni kuwatii viongozi mataghuti na kuwataka usaidizi kwa kukusudia kupata faida na manufaa, na ukubwa wa manufaa ya duniani si chochote kulinganisha na ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Kwa maneno mengine ni kwamba wao wanamtii kiumbe kwa kumuasi muumba kwa ajili ya manufaa ya dunia, hawajui kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali na kubwa zaidi.

Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema katika bustani zipitazo mito chini yake.

Aya iko wazi na pia imekwishatangulia katika Juz. 1 (2: 25).

Hakika Mwenyezi Mungu hufanya ayatakayo katika kuwapa thawabu wema na kuwaadhibu waovu. Na amekwishapitisha kuwa waliofanya mema atawalipa mema na wabaya atawalipa ubaya kutona na waliyoyafanya.

مَنْ كَانَ يَظُنُّ أَنْ لَنْ يَنْصُرَهُ اللَّهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ فَلْيَمْدُدْ بِسَبَبٍ إِلَى السَّمَاءِ ثُمَّ لْيَقْطَعْ فَلْيَنْظُرْ هَلْ يُذْهِبَنَّ كَيْدُهُ مَا يَغِيظُ {15}

Anayedhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru katika dunia na Akhera, basi na afunge kamba mbinguni kisha aikate, aone je, hila yake itaondoa yale yaliyomghadhabisha?

وَكَذَٰلِكَ أَنْزَلْنَاهُ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ وَأَنَّ اللَّهَ يَهْدِي مَنْ يُرِيدُ {16}

Na namna hiyo tumeiteremsha kuwa ni Aya zilizo wazi na kwamba Mwenyezi Mungu humuongoza anayetaka.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالصَّابِئِينَ وَالنَّصَارَىٰ وَالْمَجُوسَ وَالَّذِينَ أَشْرَكُوا إِنَّ اللَّهَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ {17}

Hakika wale ambao wameamini na ambao ni mayahudi na wasabai na wanaswara na wamajusi na wale washirikishao, hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya kila kitu.

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يَسْجُدُ لَهُ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَمَنْ فِي الْأَرْضِ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ وَالنُّجُومُ وَالْجِبَالُ وَالشَّجَرُ وَالدَّوَابُّ وَكَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ ۖ وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ الْعَذَابُ ۗ وَمَنْ يُهِنِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِنْ مُكْرِمٍ ۚ إِنَّ اللَّهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ ۩ {18}

Je huoni kuwa vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini na jua na mwezi na nyota na milima na miti na wanyama na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahili adhabu. Na anayetwezwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumheshimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.