read

Aya 83 – 91: Na Ayyub Aliopomlingania Mola Wake

Maana

Na Ayyub aliopomlingania Mola wake: Hakika mimi imenigusa dhara, nawe ndiye unayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu. Basi tukamkubalia na tukamuondolea dhara.

Makusudio ya dhara ni madhara ya nafsi, kama vile maradhi, kutokana na neno la kiarabu dhurr.

Likisomwa dharr ndio linakuwa na maana ya madhara ya kila kitu. Wafasiri na wapokezi wengi wamepokea riwaya nyingi zinazomuhusu Ayyub. Tunalolifahamu sisi, kutokana na Aya zinazomzungumzia kwa uwazi na kwa ishara hapa na pia katika Sura Swad (38), ni kwamba Ayyub alikuwa na afya yake nzuri akiwa hana matatizo yoyote. Kisha mabalaa yakaanza kumwandama kila upande, akawa ni wa kupigiwa mifano.

Masaibu yalimpata yeye mwenyewe binafsi; akavumilia uvumilivu wa kiungwana; na akabakia na yakini yake na kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu. Huzuni wala machungu hayakumfanya aache kumtii Mwenyezi Mungu. Lakini muda ulivyomzidi na machungu nayo yakazidi, alimshtakia

Mwenyezi Mungu mambo yake kwa maneno mawili tu: “Imenigusa dhara, nawe ndiye unayerehemu zaidi kuliko wanaorehemu,” na wala hakulalamika kwa kusema balaa gani hii iliyoniandama.

Ndipo Mwenyezi Mungu akamwitikia maombi yake na akamuondolea mabalaa na kumrudisha katika hali nzuri zaidi ya alivyokuwa.

Na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema itokayo kwetu na ukumbusho kwa wafanyao ibada.

Mwenyezi Mungu alimruzuku watoto na wajukuu zaidi ya wale aliowakosa, ikiwa ni rehema na malipo ya uvumilivu wake; na pia kukumbusha kwamba mwenye kuwa na subra na uvumilivu kama wa Ayyub, basi mwisho wake utakuwa kama wa Ayyub. Mwenyezi Mungu amehusisha kuwataja wenye kuabudu kwa kuashiria kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na mwenye subra aliye na ikhlasi kwa kauli yake na vitendo vyake.

Huu ndio ujumla wa maelezo ya Aya zinazofungamana na Ayyub; bila ya kuingilia ufafanuzi walioutaja wapokezi na wasimulizi. Kwani huo hauam- batani na itikadi wala uhai kwa mbali wala karibu. Miongoni mwa njia za Qur’an ni kukitaja kisa kwa yale yaliyo na mazingatio yenye kunufaisha na mawaidha ya kukanya.

Na Isamil Na Idris Na Dhulkifl, wote walikuwa miongoni mwa wanao- subiri. Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao ni katika watu wema.

Ismail alifanya subra ya kukubali kuchinjwa na akawa na uvumilivu wa kukaa katika nchi isiyokuwa na mimea wala kinywewa. Idris tumemueleza katika Juz. 16 (19:56).

Ama Dhulkifl wengi wamesema alikuwa Mtume; na baadhi wakasema alikuwa ni mja mwema tu na sio Mtume. Sisi tunaamini kwamba yeye ni miongoni mwa waliokuwa na subira na waja wema, kwa kufuata Qur’an ilivyosema, na wala hatutaulizwa zaidi ya hayo.

Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhabika na akadhani kuwa hatutamdhikisha. Basi aliita katika giza kwamba: Hapana Mola isipokuwa wewe, umetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.

Dhun-Nun ni Yunus. Maana ya neno ‘Nun” ni samaki. Mwenyezi Mungu anasema:

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تَكُنْ كَصَاحِبِ الْحُوتِ{48}

“Na vumilia hukumu ya Mola wako wala usiwe kama sahibu wa samaki” (68:48).

Hali ameghadhibika ni kuwaghadhibikia watu wake. Neno kudhikishwa limefasiriwa kutokana na neno Naqdira alyh; kama lilivyotumika mahali pengine:

وَمَنْ قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ{7}

“Na yule ambaye imekuwa dhiki riziki yake” (65:7).

Makusudio ya katika giza hapa ni ndani ya tumbo la samaki.

Maana kwa ujumla ni: kumbuka ewe Muhammad habari ya Yunus alipowalingania watu wake, lakini hawakumwitikia mwito wake, akawaondokea kwa kuwakasirikia, akadhani kuwa hatutamdhikisha kwa kumzuia n.k. Alipomezwa na samaki akataka uokovu kutoka kwetu, basi tukamkubalia na tukamwokoa kutokana na ghamu. Kama hivyo tunawaokoa wenye kuamini.

Makusudio ya ghamu hapa ni tumbo la samaki; na kuokoka, ni kutolewa humo hadi kwenye nchi kavu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:98).

Na Zakaria alipomwita Mola wake: Ewe Mola wangu! Usiniwache peke yangu na wewe ndiye mbora wa wanaorithi. Basi tukamwitikia na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 ( 3: 38) na Juz. 16 (19:7).

Hakika wao walikuwa wepesi kufanya kheri na wakituomba kwa hofu na walikuwa wakitunyenyekea.

Wao ni Zakariya, mkewe na Yahya au wale Mitume waliotangulia kutajwa. Wote walifanya kheri kwa kutaka thawabu za Mwenyezi Mungu na kuhofia adhabu yake na walikuwa wakimfuata Mwenyezi Mungu katika kila jambo.

Na mwanamke aliyelinda tupu yake na tukampulizia katika roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni ishara kwa walimwengu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (3: 45) na Juz. 16 (19: 16).

إِنَّ هَٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ {92}

Hakika umma wenu huu ni umma mmoja, na mimi ni Mola wenu kwa hivyo niabuduni.

وَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُمْ بَيْنَهُمْ ۖ كُلٌّ إِلَيْنَا رَاجِعُونَ {93}

Na wakalivunja jambo lao baina yao. Wote watarejea kwetu.

فَمَنْ يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَا كُفْرَانَ لِسَعْيِهِ وَإِنَّا لَهُ كَاتِبُونَ {94}

Na atendaye mema naye ni mumin, basi haitakataliwa bidii yake na hakika sisi tutamwandikia.

وَحَرَامٌ عَلَىٰ قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا أَنَّهُمْ لَا يَرْجِعُونَ {95}

Na ni haramu kwa mji tuliouangamiza kwamba wao hawatarejea.

حَتَّىٰ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُمْ مِنْ كُلِّ حَدَبٍ يَنْسِلُونَ {96}

Mpaka watakapofunguliwa Juju na Majuju, wakawa wanateremka kutoka kila mlima.

وَاقْتَرَبَ الْوَعْدُ الْحَقُّ فَإِذَا هِيَ شَاخِصَةٌ أَبْصَارُ الَّذِينَ كَفَرُوا يَا وَيْلَنَا قَدْ كُنَّا فِي غَفْلَةٍ مِنْ هَٰذَا بَلْ كُنَّا ظَالِمِينَ {97}

Na miadi ya haki itakaribia, ndipo yatakapokodoka macho ya wale waliokufuru. Ole wetu! Hakika tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa ni wenye kudhulumu.

إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنْتُمْ لَهَا وَارِدُونَ {98}

Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.

لَوْ كَانَ هَٰؤُلَاءِ آلِهَةً مَا وَرَدُوهَا ۖ وَكُلٌّ فِيهَا خَالِدُونَ {99}

Lau haya yangelikuwa ni miungu yasingeliingia na wote watadumu humo.

لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌ وَهُمْ فِيهَا لَا يَسْمَعُونَ {100}

Lao humo ni kupiga mayowe na wala hawatasikika.