read

Aya 92 – 100: Umma Mmoja

Maana

Hakika umma wenu huu ni umma mmoja, na mimi ni Mola wenu kwa hiyo niabuduni.

Lugha

Maana ya neno umma ni watu wenye lugha moja na historia moja. Kisha neno hili likawa linatumika zaidi kwa maana ya dini na mila. Maana haya ndiyo yaliyokusudiwa hapa.

Umma wenu huu ni itikadi ya mitume ambayo ni tawhid pamoja na kufuata amri za Mwenyezi Mungu kwa kauli na vitendo. Msemo ‘wenu’ unaelekezwa kwa watu wote.

Maana ni kuwa enyi watu wote! Shikeni dini ya Tawhidi waliyokuwa nayo Mitume na mumwabudu Mungu mmoja aliye peke na mumfanyie ikhlasi katika kauli na vitendo.

Na wakalivunja jambo lao baina yao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaamrisha wote wawe kwenye itikadi ya tawhidi, lakini wakagawanyika wakawa makundi ya wakana Mungu na washirikina. Hata wale wafuasi wa Mitume nao wanatukanana na kujitenga na wengine; bali hata wafuasi wa Mtume mmoja nao ni hivyo hivyo.

Wote watarejea kwetu.

Haya ni makemeo na hadhari kwa wale wanaofarikiana wakawa vikundi.

Na atendaye mema naye ni mumin, basi haitakataliwa bidii yake na hakika sisi tutamwandikia.

Imani pamoja na matendo mema ni njia ya Peponi na imani bila ya matendo haifai chochote. Hiyo ni kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

لَا يَنْفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِنْ قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ۗ {158}

“Basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake.” Juz. 8 (6:158).

Ama matendo mema bila ya imani, humnufaisha mtendaji kwa namna moja au nyingine na huenda ikamfaa huko Akhera kwa kupunguziwa adhabu. Tumeyafafanua hayo katika Juz. 4 (3:158) kwenye kifungu ‘kafiri na amali njema’ Pia Umepita mfano wake katika Juz. 14 (16: 97)

Na ni haramu kwa mji tuliouangamiza kwamba wao hawatarejea.

Aya hii ni jawabu la swali la kukadiria, kwamba je, washirikina katika watu wa kijiji kilichoangamizwa na Mwenyezi Mungu kwa kufuru yao, watarudishwa tena kuwa hai na kuadhibiwa huko Akhera, kama walivyoadhibiwa duniani?

Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwa watu wote, kesho watarejea kwa Mwenyezi Mungu; hata wale walioangamizwa duniani kwa dhambi zao na ni muhali kukosa kurejea kwa Mwenyezi Mungu baada ya mauti; bali hakuna budi lazima watafufuliwa.

Swali la pili, je inafaa kuadhibiwa akhera baada ya kuadhibiwa duniani? Huko si ni kuadhibu mara mbili kwa kosa moja?

Jibu: Hapana! Kuadhibiwa kwao duniani kulikuwa ni kwa ajili ya kuwakadhibisha kwao Mitume waliowajia na miujuza; kama zinavyofahamisha Aya hizi zifuatazo na nyinginginezo mfano wake:

وَقَوْمَ نُوحٍ لَمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ {37}

“Na kaumu ya Nuh walipowakadhibisha Mitume tuliwagharikisha” (25:37)

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَأَصْحَابُ الرَّسِّ وَثَمُودُ {12}

وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ وَإِخْوَانُ لُوطٍ {13}

وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ وَقَوْمُ تُبَّعٍ ۚ كُلٌّ كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ وَعِيدِ {14}

“Kabla yao walikadhibisha kamu ya Nuh na watu wa Rassi na Thamud na A’d na Firauni na ndugu wa Lut na watu wa vichakani na kaumu ya Tubbai, wote waliwakadhibisha Mitume, kwa hiyo kiaga kikathibitika juu yao.” (50: 12-14).

Ama adhabu ya Akhera ni ya ukafiri wenyewe na madhambi mengineyo; kama dhulma n.k.
Kwa hiyo adhabu zinakuwa nyingi kutokana na dhambi kuwa aina nyingi, sio kwa dhambi moja.

Mpaka watakapofunguliwa Juju na Majuju, wakawa wanateremka kutoka kila mlima.

Katika Juz. 16 (18: 94) tuliwanukuu baadhi ya wafasiri wakisema kuwa Juju ni wa Tatars na Majuju ni Wamongoli. Vile vile tumesema huko kuwa ukuta wa Juju na Majuju hauko tena. Kwa hiyo basi makusudio ya kufunguliwa Juju na Majuju ni kuenea kwao katika mabara.

Vyovyote iwavyo sisi hatujawahi kusoma ya kutegemewa kuhusu Juju na Majuju, si katika tafsiri wala mahali penginepo. Kwa hiyo tutasimama kwenye dhahiri ya nukuu ya Qur’an tu na ufafanuzi tutawachia wengine.

Na miadi ya haki itakaribia, ndipo yatakapokodoka macho ya wale waliokufuru.

Makusudio ya miadi ya haki hapa ni Kiyama, hapo akili za waliokufuru zitapotea na macho yatatoka kutokana na vituko vya siku hiyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (14: 42).

Ole wetu! Hakika tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.

Yaani watasema hivyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:5) na katika juzuu na Sura hii tuliyo nayo Aya 14 na 46.

Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.

Hapa wanaambiwa washirikina wa Makka. Makusudio ya mnayoyaabudu ni masanamu yao. Maana ni kuwa, enyi washirikina! Nyinyi na masanamu yenu mtakutana kwenye Jahannamu kesho. Kuna Hadithi isemayo: “Mtu yuko pamoja na anayempenda.”

Unaweza kuuliza: Kuna faida gani ya kutiwa masanamu kwenye Jahannamu na ni mawe yasiyokuwa na utambuzi wala hisiya?

Wafasiri wamejibu kuwa lengo ni kuwazidishia masikitiko wale wanaoyaabudu, kila watakapoyaona karibu nao. Lakini jawabu hili ni kiasi cha kuchukulia uzuri na hisia tu. Lilio bora ni kuicha Aya nyingine ijibu:

فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ {24}

“Basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, uliowekewa makafiri.” Juz. 1 (2:24).

Kuna riwaya isemayo kuwa Ibn Az-Zab’ariy – mmoja wa washirkina wa kikuraishi na mshairi wao – aliingilia Aya hii kama mayahudi wanamwabudu Uzayr na wanaswara (wakristo) wanamwabudu Masihi na hawa wawili ni watu wa Peponi, kama anavyosema Muhammad, sasa vipi aseme kila kinachoabudiwa ni kuni?

Mtume akamjibu: Ni ujinga ulioje wako wewe kutojua lugha ya watu wako. Kwani huoni herufi ma (ambayo) ni ya visivyo na akili?

Zaidi ya hayo maneno yanawahusu washirikina wa kikurashi, kama tulivyotangulia kusema nao wanaabudu masanamu.

Lau haya yangelikuwa ni miungu yasingeliingia na wote watadumu humo.

Haya ni ishara ya masanamu. Maana ya Aya yako wazi, kwamba lau masanamu yangelikuwa miungu yasingeliiingia motoni. Ni kama kusema: Lau ungelikuwa mwaminifu usingelifanya khiyana, lakini umefanya khiyana kwahiyo wewe si mwaminifu. Mfano huu katika mantiki unaitwa kutoa dalili kwa kipimo cha kuvua (istithnaiyy).

Lao humo ni kupiga mayowe na wala hawatasikika.

Hapa anaambiwa kila mkosaji, awe mwislamu au kafiri. Humo ni humo ndani ya Jahannam. Maana ni kuwa kila mkosaji atakuwa katika Jahannam akilalama kwa machungu; hatasikia neno la upole wala huruma, bali atakayemuona atamtahayariza na kumsema:

وَقِيلَ لِلظَّالِمِينَ ذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَكْسِبُونَ {24}

“Na wenye kudhulumu wataambiwa onjeni yale mliyokuwa mkiyachuma.” (39:24).

إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُمْ مِنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ {101}

Hakika wale ambao umewatangulia wema kutoka kwetu, hao watatenganishwa na hayo.

لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنْفُسُهُمْ خَالِدُونَ {102}

Hawatasikia mvumo wake. Nao watudumu katika yale ambayo nafsi zao zinayatamani.

لَا يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ هَٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنْتُمْ تُوعَدُونَ {103}

Hiyo fazaa kubwa haitawahuzunisha. Na Malaika watawapokea: Hii ndiyo siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.

يَوْمَ نَطْوِي السَّمَاءَ كَطَيِّ السِّجِلِّ لِلْكُتُبِ ۚ كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ {104}

Siku tutakapozikunja mbingu mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika sisi ni wenye kufanya.

وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِي الزَّبُورِ مِنْ بَعْدِ الذِّكْرِ أَنَّ الْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِيَ الصَّالِحُونَ {105}

Na hakika tulikwishaandika katika Zaburi baada ya ukumbusho kuwa Ardhi watairithi waja wangu walio wema.

إِنَّ فِي هَٰذَا لَبَلَاغًا لِقَوْمٍ عَابِدِينَ {106}

Hakika katika haya kuna ujumbe kwa wafanyao ibada.

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ {107}

Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu.