read

Aya 1-5: Mwongozo Na Bishara Kwa Waumini

Maana

Twa siin.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1)

Hiyo ni Aya za Qur’an na Kitabu kinachobainisha.

Hiyo ni ishara ya Sura hii. Qur’an na Kitabu ina maana moja. Tofauti ni wasifu tu, sio kwa dhati yake. Ni Qur’an kwa vile inasomwa, kutokana na neno na qiraa lenye maana ya kusoma. Na kitabu kwa vile imeandikwa, kutokana na neno kitaba lenye maana ya kuandika.

Ni chenye kubainisha kwa vile kiko wazi. Pia vilevile ni mwongozo na bishara kwa waumini.

Kinamuongoza mwenye kutafuta uongofu na kumpa habari njema ya Pepo ikiwa ataamini na kutenda mema.

Wale ambao wanasimamisha Swala na wakatoa Zaka na wana yakini na Akhera.

Imani peke yake si kitu mbele ya Mwenyezi Mungu ila zikidhihiri athari zake; miongoni mwa zile zilizo muhimu zaidi ni swala na zaka. Kwa ufupi ni kuwa kuamini haki sio fikra ya kichwani wala maneno ya mdomoni; isipokuwa ni matendo na tabia.

Unaweza kuuliza: Wenye kusimamisha Swala na kutoa Zaka tayari wana yakini na Akhera, sasa kuna wajihi gani wa kusema na wana yakini na akhera?

Jibu: Makusudio ni kuwa wanaiamini Akhera kwa imani isiyo na shaka; kama vile wameiona.

Hakika ambao hawaiamin Akhera, tumewapambia vitendo vyao, basi wao wanamangamanga.

Nyoyo zimepofuka, hazioni matendo yao. Kwa hiyo wanafanya bila ya kuhofia hisabu wala adhabu.
Unaweza kuuliza: Hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametegemeza kupambia kwake yeye mwenyewe na katika Aya nyingine amekutegemeza kwa shetani: “Lakini shetani aliwapambia vitendo vyao.” Juz. 14 (16:63). Sasa je, kuna wajihi gani wa kuunganisha Aya mbili hizi?

Jibu: Kule kumetegemezwa kupamba kwa shetani kwa kuangalia kuwa yeye ni mhalifu na mtia wasiwasi. Hapa kumetegemzwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuangalia kuwa desturi ya Mwenyezi Mungu na matakwa yake yamepitisha kupofuka na uovu wa matendo yake yule asiyeamini Siku ya Mwisho; sawa kama yalivyopitisha matakwa yake Mwenyezi Mungu kufa kwa yule anayefuata njia inayopelekea kifo.

Kwa maneno mengine ni kuwa yule asiyeamini Akhera anafanya haramu huku akiona ni halali, kwa sababu Mwenyezi Mungu amejaalia kukosa imani ni sababu ya kutojua haramu.

Kama mtu atasema, hilo si ni jambo la kawaida? Tutajibu: Vitu vyote vya kawaida ya maumbile na sababu vinakomea kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu yeye ndiye aliyeleta hayo maumbile ya kawaida na ulimwengu kwa ujumla.

Hao ndio watakaopata adhabu mbaya, na wao katika Akhera ni wenye kupata hasara.

Wamepata hasara duniani kwa sababu wameiacha na wamepata hasara Akhera ya thawabu na kupata adhabu. Hiyo ndiyo hasara ya dhahiri.

وَإِنَّكَ لَتُلَقَّى الْقُرْآنَ مِنْ لَدُنْ حَكِيمٍ عَلِيمٍ {6}

Na kwa hakika wewe unapewa Qur’an kutoka kwake Mwenye hekima, Mwenye ujuzi.

إِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِأَهْلِهِ إِنِّي آنَسْتُ نَارًا سَآتِيكُمْ مِنْهَا بِخَبَرٍ أَوْ آتِيكُمْ بِشِهَابٍ قَبَسٍ لَعَلَّكُمْ تَصْطَلُونَ {7}

Musa alipowaambia ahli zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda kuwaletea habari au kuwaletea kijinga kinachowaka ili mpate kuota.

فَلَمَّا جَاءَهَا نُودِيَ أَنْ بُورِكَ مَنْ فِي النَّارِ وَمَنْ حَوْلَهَا وَسُبْحَانَ اللَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ {8}

Basi alipoufikia, pakanadiwa kwamba umebarikiwa uliomo katika moto huu na aliyeko pembezoni mwake na ametakasika Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.

يَا مُوسَىٰ إِنَّهُ أَنَا اللَّهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {9}

Ewe Musa! Hakika mimi ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

وَأَلْقِ عَصَاكَ ۚ فَلَمَّا رَآهَا تَهْتَزُّ كَأَنَّهَا جَانٌّ وَلَّىٰ مُدْبِرًا وَلَمْ يُعَقِّبْ ۚ يَا مُوسَىٰ لَا تَخَفْ إِنِّي لَا يَخَافُ لَدَيَّ الْمُرْسَلُونَ {10}

Na itupe fimbo yako! Alipoiona inatingishika, kama kwamba ni nyoka, aligeuka kurudi nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usihofu! Hakika mimi hawagopi mbele yangu mitume.

إِلَّا مَنْ ظَلَمَ ثُمَّ بَدَّلَ حُسْنًا بَعْدَ سُوءٍ فَإِنِّي غَفُورٌ رَحِيمٌ {11}

Ila aliyedhulumu kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi hakika mimi ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

وَأَدْخِلْ يَدَكَ فِي جَيْبِكَ تَخْرُجْ بَيْضَاءَ مِنْ غَيْرِ سُوءٍ ۖ فِي تِسْعِ آيَاتٍ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَقَوْمِهِ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ {12}

Na ingiza mkono wako katika mfuko wako utatoka mweupe pasipo ubaya. Ni katika ishara tisa kwa Firauni na watu wake. Hakika wao ni watu mafasiki.

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ آيَاتُنَا مُبْصِرَةً قَالُوا هَٰذَا سِحْرٌ مُبِينٌ {13}

Zilipowafikia ishara zetu zionyeshazo, walisema: Huu ni uchawi dhahiri.

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنْفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا ۚ فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ {14}

Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa wafisadi.