Table of Contents

Aya 1-9: Huenda Ukaangamiza Nafsi Yako

Maana

Twaa Siin Miim.

Umetangulia mfano wake mwanzo wa Sura Baqara, Juz. 1

Hizo ni Aya za Kitabu kinachobainisha.

Hizo ni ishara ya Aya za Sura hii, kitabu ni Qur’an na chenye kubainisha ni kubainisha haki na kudhihirisha.

Huenda ukaiangamiza nafsi yako kwa kuwa hawawi waumini.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.) kwamba asiikere na kuiumiza nafsi yake kwa sababu ya watu wake kuukataa uongofu na haki. Umetangulia mfano wake katika Juz.7 (6:35) na Juz. 15 (18:6).

Tungelipenda tungeliwateremshia kutoka mbinguni ishara zikainyenyekea shingo zao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamwambia Mtume wake mtukufu: Poa moyo wako! Lau tungelitaka waamini kwa nguvu tungeliteremsha adhabu kutoka mbinguni waione kwa macho na kuwaambia chagueni imani au adhabu; bila shaka wao wangelisalimu amri kwa unyenyekevu.

Lakini je, hii itahisabiwa kuwa ni imani? Hapana! Imani ya kweli inakuwa kwa utashi na hiyari, sio kwa kulazimishwa kwa nguvu. Ndio maana tukawakadiria kheri na shari, tukawaamrisha hili na kuwakataza lile; kisha tukawaachia hiyari, waweze kustahiki thawabu kwa utiifu na adhabu kwa uasi.

Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alifanya hivyo katika zama za Musa (a.s.) kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na tulipoinua mlima juu yao kama kwamba ni kiwingu kilichowafunika na wakadhani kuwa utawaangukia. Tukawaambia: shikeni kwa nguvu tuliyowapa.” Juz. 9 (7: 171).

Jibu: kwa hakika Qur’an Tukufu inafahamisha waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ana muamala maalum na Mayahudi usiofanana na waja wengine. Kwa sababu wao wana tabia za pekee zisizokuwa na mfano. Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi zaidi kwa anuani ya ‘Mayahudi hawana mfano’ katika Juz. 1: (2:63-66).

Na hauwajii ukumbusho mpya kutoka kwa Mwingi wa rehema ila hujitenga nao. Kwa hakika wamekadhibisha, kwa hivyo zitakujawafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai.

Tumewaongoza washirikina, kupitia kwako ewe Muhammad, kwenye yale yaliyo na kheri yao na masilahi yao, wakaachana nayo, wakayadharau na kuyafanyia masikhara. Basi nawe achana nao na watakumbana na adhabu waliyoahidiwa tu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:68).

Je hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri. Hakika katika hayo kuna ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

Alikufuru Mungu aliyekufuru huku akiona dalili na ubainifu wa kupatikana kwake na ukuu wake. Miongoni mwa dalili hizi ni kutoa mimea ya aina na rangi mbali mbali. Kwa maelezo zaidi angalia Juz.7 (6:99) na Juz. 13 (13:3).

Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Kwa nguvu zake anawashinda mataghuti na rehema zake anawapa muda bila ya kuwaharakishia adhabu mpaka awajie mbashiri na muonyaji na kuwapa fursa ya kufikiria vizuri na kutubia.
Imam Ali (a.s.) anasema: “Hasira zake hazimfanyi kuacha huruma yake, wala huruma haimfanyi kupuuza adhabu yake.”

وَإِذْ نَادَىٰ رَبُّكَ مُوسَىٰ أَنِ ائْتِ الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ {10}

Na Mola wako alipomwita Musa kwamba nenda kwa watu madhalimu.

قَوْمَ فِرْعَوْنَ ۚ أَلَا يَتَّقُونَ {11}

Watu wa Firauni. Hawaogopi?

قَالَ رَبِّ إِنِّي أَخَافُ أَنْ يُكَذِّبُونِ {12}

Akasema: Mola wangu! Hakika mimi naogopa watanikadhibisha.

وَيَضِيقُ صَدْرِي وَلَا يَنْطَلِقُ لِسَانِي فَأَرْسِلْ إِلَىٰ هَارُونَ {13}

Na kifua changu kinadhikika, na ulimi wangu haukunjuki vyema, basi mtumie ujumbe Harun.

وَلَهُمْ عَلَيَّ ذَنْبٌ فَأَخَافُ أَنْ يَقْتُلُونِ {14}

Nao wanalo kosa juu yangu basi naogopa wasije wakaniua.

قَالَ كَلَّا ۖ فَاذْهَبَا بِآيَاتِنَا ۖ إِنَّا مَعَكُمْ مُسْتَمِعُونَ {15}

Akasema, sivyo kabisa! Nendeni na ishara yetu. Hakika sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.

فَأْتِيَا فِرْعَوْنَ فَقُولَا إِنَّا رَسُولُ رَبِّ الْعَالَمِينَ {16}

Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wa walimwengu wote.

أَنْ أَرْسِلْ مَعَنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ {17}

Ya kwamba uwaachilie wana wa Israil waende nasi.

قَالَ أَلَمْ نُرَبِّكَ فِينَا وَلِيدًا وَلَبِثْتَ فِينَا مِنْ عُمُرِكَ سِنِينَ {18}

Akasema: Je, hatukukulea utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?

وَفَعَلْتَ فَعْلَتَكَ الَّتِي فَعَلْتَ وَأَنْتَ مِنَ الْكَافِرِينَ {19}

Na ukatenda kitendo chako ulichokitenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?

قَالَ فَعَلْتُهَا إِذًا وَأَنَا مِنَ الضَّالِّينَ {20}

Akasema: Nililifanya hilo nikiwa miongoni mwa wasioelewa.

فَفَرَرْتُ مِنْكُمْ لَمَّا خِفْتُكُمْ فَوَهَبَ لِي رَبِّي حُكْمًا وَجَعَلَنِي مِنَ الْمُرْسَلِينَ {21}

Basi niliwakimbia nilipowahofia. Na Mola wangu akanitunukia hukumu na akanijaalia niwe miongoni mwa mitume.

وَتِلْكَ نِعْمَةٌ تَمُنُّهَا عَلَيَّ أَنْ عَبَّدْتَ بَنِي إِسْرَائِيلَ {22}

Na hiyo ndiyo neema ya kunisimbulia na wewe umewatia utumwani wana wa Israil?