Table of Contents

Aya 105 – 122: Nuh

Maana

Kaumu ya Nuh waliwakadhibisha mitume.

Mtume aliyetumwa kwao ni mmoja ambaye ni Nuh, lakini mwenye kumkadhibisha Mtume mmoja ni kama amewakadhibisha mitume wote, kwa vile aliyewatuma ni mmoja na ujumbe ni mmoja.

Alipowaambia ndugu yao Nuh: Je, hamna takua?

Mwenye kuishika takua atakuwa katika amani na atasalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

Alijisifu kwa uaminifu ambao waliujua kwake akiwa mdogo na mtu mzima; sawa na makuraishi walivyomjua Muhammad (s.a.w.) kwa ukweli na uaminifu katika hali zake zote.

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Kwa sababu ninawaita kwenye lile ambalo lina kheri yenu ya dunia na akhera.

Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:90) na Juz. 12 (11:29).

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

Hakuna sababu ya kukaririka jambo la takua (kumcha Mungu) isipokuwa ni jambo muhimu na la msingi.

Wakasema: Je, tukuamini na hali wanaokufuata ni walio duni.

Walimtia ila Nuh, si kwa lolote ila ni kwa kuwa mafukara walimwamini na kwao, hawana thamani. Kwa hiyo utume wa Nuh hauna thamani. Kwa maneno mengine ni kuwa wapenda anasa hawaoni kuwa ufukara ni maisha. Vipi wataamini waliloliamini mafukara? Hivi ndivyo wafanyavyo wapenda anasa; wanakuwa vipofu wa haki na wanakuwa na kiburi.

Akasema: Nayajuaje waliyokuwa wakiyafanya? Hisabu yao haiko ila kwa Mola wangu.

Nuh aliwaambia wale waliomjadili kuhusu ufukara, kuwa thamani ya mtu ni matendo yake na malengo yake, sio kwa cheo na mali. Na mimi sijui kuwa wao walimfanyia ubaya mtu yoyote kwa kauli au vitendo. Siri iko kwa Mwenyezi Mungu. Yeye peke yake ndiye anayejua na kuhisabu.

Lau mngelitambua kwamba thamani ya mtu ni kwa matendo sio kwa mali na dhahiri ni ya watu na batini ni ya Mwenyezi Mungu.

Wala mimi si mwenye kuwafukuza waumini. Sikuwa mimi ila ni muonyaji aliye dhahiri.

Umetangulia mfano wake katika Juz. Juz. 12 (11: 29).

Wakasema: Kama hutakoma ewe Nuh bila shaka utapigwa mawe.

Wameshindwa kuijadili haki wakakimbilia vitisho na mabavu. Hii ndio tabia ya wasiofuta haki, kila mahali na kila wakati.

Akasema: Mola wangu! Hakika kaumu yangu wamenikadhibisha. Basi amua baina yagu mimi na wao uamuzi.

Walipompa vitisho vya kutumia nguvu, alimuomba msaada Mwenyezi Mungu na nguvu zake. Na kwa unyenyekevu akamuomba Mwenyezi Mungu ahukumu, baina yake na yao, hukumu itakayomnusuru mwenye haki na kumwadhibu mwenye batili.

Na uniokoe na walio pamoja nami katika waumini pale itakapowashukia adhabu makafiri.

Basi tukamuokoa na walio pamoja naye katika jahazi iliyosheheni walioamini katika watu wake na wengineo na viumbe wengine wa kiume na wa kike.

Kisha tukawagharikisha baadaye waliobaki.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:64) na Juz. 12 (11:40).
Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya Sura hii.

كَذَّبَتْ عَادٌ الْمُرْسَلِينَ {123}

A’d waliwakadhibisha mitume.

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ هُودٌ أَلَا تَتَّقُونَ {124}

Alipowaambia ndugu yao Hud: Je, hamna takua?

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ {125}

Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ {126}

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ {127}

Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

أَتَبْنُونَ بِكُلِّ رِيعٍ آيَةً تَعْبَثُونَ {128}

Je, mnajenga juu ya kila muinuko ishara ya kufanyia upuuzi?

وَتَتَّخِذُونَ مَصَانِعَ لَعَلَّكُمْ تَخْلُدُونَ {129}

Na mnajenga ngome ili mkae milele.

وَإِذَا بَطَشْتُمْ بَطَشْتُمْ جَبَّارِينَ {130}

Na mnaposhika kwa nguvu mnashika kwa nguvu kwa ujabari.

فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ {131}

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَاتَّقُوا الَّذِي أَمَدَّكُمْ بِمَا تَعْلَمُونَ {132}

Na mcheni ambaye amewapa mnayoyajua.

أَمَدَّكُمْ بِأَنْعَامٍ وَبَنِينَ {133}

Amewapa wanyama na watoto wa kiume.

وَجَنَّاتٍ وَعُيُونٍ {134}

Na mabustani na chemchemi.

إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ {135}

Hakika ninawahofia adhabu ya siku kubwa.

قَالُوا سَوَاءٌ عَلَيْنَا أَوَعَظْتَ أَمْ لَمْ تَكُنْ مِنَ الْوَاعِظِينَ {136}

Wakasema: Ni mamoja kwetu ukitupa mawaidha au kutokuwa miongoni mwa watoao mawaidha.

إِنْ هَٰذَا إِلَّا خُلُقُ الْأَوَّلِينَ {137}

Haya si chochote ila ni hulka ya wa kale.

وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ {138}

Wala sisi hatutaadhibiwa.

فَكَذَّبُوهُ فَأَهْلَكْنَاهُمْ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُمْ مُؤْمِنِينَ {139}

Basi wakamkadhibisha na tukawahilikisha. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ {140}

Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.