Table of Contents

Aya 123 – 140: Hud

Maana

Kisa cha Hud kimetangulia katika Juz. 8 (7:65 – 72) na Juz. 12 (11:50 – 60).

A’d waliwakadhibisha mitume. Alipowaambia ndugu yao Hud: Je, hamna takua? Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Zimetangulia Aya kwa herufi zake katika sehemu iliyopita ya Sura hii Aya 105 – 110, bila ya mabadiliko yoyote isipokuwa jina tu. Kule imesemwa kaumu ya Nuh na hapa ni Hud na A’d.

Siri ya hilo ni kuwa risala ya mitume wote ni moja, ikilingania kwenye umoja wa Mwenyezi Mungu na kutii amri yake na makatazo yake.

Je, mnajenga juu ya kila muinuko ishara ya kufanyia upuuzi?

Makusudio ya ishara hapa ni jengo. Kila jengo linalotekeleza haja ya maisha hilo ni la kheri na ni katika dini. Kwa sababu dini ya Mwenyezi Mungu ni dini ya maisha. Ama jengo lisilokuwa na faida zaidi ya kujionyesha na kujifaharisha, hilo ni shari kidini na kiakili. Aina hii ndio inayokusudiwa hapa kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu ‘ya kufanyia upuuzi’ kwa sababu upuuzi ni ule usiohitajika.

Na mnajenga ngome ili mkae milele.

Makusudio ya ngome hapa ni jengo lisilokuwa na manufaaa yoyote.

Na mnaposhika kwa nguvu mnashika kwa nguvu kwa ujabari. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

Kutumia nguvu kwa ujabari ni kudhulumu kwa hali ya juu, na inakuwa kubwa dhulma kwa kumdhulumu mnyonge. Lililothibiti katika dini ya Mwenyezi Mungu ni kuwa dhulma ni miogoni mwa madhambi makubwa; bali ni sawa na kumkufuru Mungu.
Tumelithibitisha hilo huko nyuma kwa nukuu ya Qur’an.

Aya hii ilishuka wakati ambao hakukuwa na silaha za maangamizi wala hakukuwa na matajiri wanaotoa mamilioni ya pesa ili waangamizwe wanawake kwa ujumla. Ilishuka wakati ambao kutumia nguvu kulikuwa ni kwa kutumia mkono zaidi - upanga mshale na mkuki.

Ikiwa Mwenyezi Mungu amesifu kuwa ni ubaya na uovu mkubwa kutumia nguvu kwa kiganja cha mkono, basi atawalipa nini wale wanaowanyeshea wanyonge mvua ya makombora, mabomu ya sumu na silaha za nuklia? Au wale ambao wameijaza ardhi na anga kwa vikosi vya majeshi. Wameijaza maroketi ya kijeshi; si kwa lolote ila wanataka kuhukumu roho za waja na nyenzo za nchi kulingana na hawa zao na masilahi yao tu.

Na mcheni ambaye amewapa mnayoyajua. Amewapa wanyama na watoto wa kiume na mabustani na chemchemi. Hakika ninawahofia adhabu ya siku kubwa.

Hud aliwalingania kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu na akawakumbusha neema yake juu yao na anavyowapa muda na pia akawahadharisha na mwisho mbaya wa dhulma. Lakini hilo halikuwazidisha kitu isipokuwa kiburi na wakasema: Ni mamoja kwetu ukitupa mawaidha au kutokuwa miongoni mwa watoao mawaidha sisi hatutakuamini. Mawaidha yako hayatatuzidishia isipokuwa kuachana nawe.

Haya si chochote ila ni hulka ya wa kale wala sisi hatutaadhibiwa.

Haya ni ishara ya dini yao na masanamu yao wanayoyaabudu; na kwamba wao hawatayaacha kwa sababu wameyarithi kutoka jadi na jadi. Hiyo ndiyo hoja yao; hawana zaidi ya ‘tumewakuta nayo baba zetu na sisi tunafuata nyayo zao.’

Basi wakamkadhibisha na tukawahilikisha.

Hud aliwaonya watu wake kwa dalili na hoja, lakini hawakujali, wakawa miongoni mwa walioangamia.

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya Sura hii na pia sehemu iliyopita.

كَذَّبَتْ ثَمُودُ الْمُرْسَلِينَ {141}

Thamud waliwakadhibisha mitume.

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ صَالِحٌ أَلَا تَتَّقُونَ {142}

Alipowaambia ndugu yao Swaleh: Je, hamna takua?

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ {143}

Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ {144}

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ {145}

Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

أَتُتْرَكُونَ فِي مَا هَاهُنَا آمِنِينَ {146}

Je, mtaachwa salama katika haya yaliyopo hapa?

فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ {147}

Katika mabustani na chem- chem?

وَزُرُوعٍ وَنَخْلٍ طَلْعُهَا هَضِيمٌ {148}

Na mimea na mitende yenye makole yalioiva?

وَتَنْحِتُونَ مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا فَارِهِينَ {149}

Na mnachonga majumba mlimani kwa ustadi

فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ {150}

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَلَا تُطِيعُوا أَمْرَ الْمُسْرِفِينَ {151}

Wala msitii amri za waliopituka mipaka.

الَّذِينَ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ {152}

Ambao wanafanya ufisadi katika ardhi wala hawaiten- genezi.

قَالُوا إِنَّمَا أَنْتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ {153}

Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa tu.

مَا أَنْتَ إِلَّا بَشَرٌ مِثْلُنَا فَأْتِ بِآيَةٍ إِنْ كُنْتَ مِنَ الصَّادِقِينَ {154}

Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

قَالَ هَٰذِهِ نَاقَةٌ لَهَا شِرْبٌ وَلَكُمْ شِرْبُ يَوْمٍ مَعْلُومٍ {155}

Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalum.

وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَظِيمٍ {156}

Wala msimguse kwa ubaya isije ikawashika adhabu ya siku kubwa.

فَعَقَرُوهَا فَأَصْبَحُوا نَادِمِينَ {157}

Lakini wakamuua wakawa wenye kujuta.

فَأَخَذَهُمُ الْعَذَابُ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُمْ مُؤْمِنِينَ {158}

Basi ikawashika adhabu. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ {159}

Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.